Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu
Waandishi Wetu
MBIO
za uchaguzi ndani ya CCM zimefikia patamu, baada ya Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu kuenguliwa
kugombea nafasi ya Ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Hanang', huku Mke wa
Rais, Salma Kikwete akiwa mgombea pekee wa nafasi hiyo Lindi Mjini.
Mkoani
Dar es Salaam, mbio hizo zimeonekana kuwaweka pabaya Mwenyekiti wa UWT
wa mkoa huo Zarina Madabida na Katibu wake, Tatu Maliaga baada ya
Mwenyekiti wa CCM Mkoa, John Guninita kueleza kuwa viongozi hao
watafikishwa kwenye kamati ya maadili kueleza kwa nini wamesitisha
uchaguzi wilayani Kinondoni.
Habari
kutoka Hanang' zimeeleza kuwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo
imemwengua Dk Nagu na kuwabakiza wagombe wawili, Waziri Mkuu Mstaafu,
Frederick Sumaye na Leonsi Marmo.
Taarifa
kutoka kwenye kikao hicho kilichofanyika juzi katika Ofisi ya CCM ya
wilaya hiyo na kuhudhuriwa na wajumbe 12 zimeeleza kuwa Dk Nagu
ameenguliwa kutokana na maelezo kuwa kanuni hazimruhusu kugombea.
Chanzo
cha habari kimeeleza kuwa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu kwenye
kinyang’anyiro hicho ni ile inayowataka viongozi wenye kazi za kila
siku; ubunge na uwaziri kutogombea.
Imeelezwa
kuwa jitihada za wajumbe watano waliojipambanua katika kikao hicho
kumtetea Dk Nagu ziligonga mwamba, baada ya wenzao saba kuunga mkono
uamuzi huo.
“Kikao
kilikuwa kizito, lakini tulitazama zaidi kanuni, sifa za wagombea na
uwezo wa wagombea hasa katika nafasi hii nyeti ya Nec kuelekea Uchaguzi
Mkuu wa 2015,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Alisema
mapendekezo ya kikao hicho, tayari yamefikishwa ngazi ya CCM mkoa kwa
uamuzi zaidi na baadaye yatafikishwa Kamati Kuu (CC) ya CCM.
“Sisi tumemaliza kazi yetu, tunaamini kuwa tumetenda haki kwa manufaa ya chama chetu Wilaya ya Hanang’,” alisema kiongozi huyo.
Hata
hivyo, mjumbe mwingine wa kikao hicho alisema, mgawo wa mkopo wa
matrekta ambao umekuwa ukiendelea Hanang’ umechangia kumwengua waziri
huyo.
“Hapa
kuna mambo mengi, nadhani hao waliokuwa na taarifa hizi, wameshindwa
kueleza zaidi. Kuna mambo ya chinichini hasa baada ya baadhi ya viongozi
kutounga mkono uamuzi wa Waziri Nagu kusaidia baadhi ya wanaCCM
wakiwamo viongozi kukopeshwa matrekta,” alisema mjumbe huyo.
Kiongozi
mmoja wa CCM Wilaya ya Hanang’ ambaye hakutaka jina lake litajwe,
alikiri kufanyika kwa kikao hicho na kueleza kuwa tatizo la Dk Nagu ni
kutoombewa kibali na kamati ya siasa wilaya au mkoa kama kanuni
zinavyotaka.
Alieleza
kuwa kanuni za CCM zinataka viongozi wenye majukumu ya kila siku
kuombewa kibali kwanza na Kamati ya Siasa ya Wilaya au Mkoa kabla ya
kugombea jambo ambalo halikufanyika kwa Dk Nagu.
“Hadi
kikao hicho kinafanyika, Dk Nagu alikuwa hajaombewa kibali hicho na
hili limetokana na migogoro ya kisiasa iliyoko wilayani Hanang’,”
alisema.
Alipoulizwa
kuhusu hilo, Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang’, Allan Kingazi alisema:
“Ni kweli kikao kilifanyika, lakini mapendekezo yetu ni siri na hao
waliokuambia wamekiuka kanuni. Sisi baada ya kumaliza kikao chetu,
mapendekezo yetu tumeyapeleka ngazi ya mkoa ambako pia yataendelea kuwa
siri hadi majina yatakapotangazwa rasmi,” alisema.
Uamuzi
wa Dk Nagu kuamua kugombea NEC kupambana na Sumaye ambaye ndiye
alimwachia jimbo hilo, ulitabiriwa kuibua mgawanyiko mkubwa ndani ya
wana CCM wa Hanang’.
Jitihada
za gazeti hili kumpata Dk Nagu kuzungumzia uamuzi huo zilishindikana
baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila kupokewa.
Kuenguliwa
kwa Dk Nagu kunatokana na sababu za kuwa na kazi za muda wote kumeibua
hofu kuhusu hatima ya viongozi wengine waliochukua fomu ambao kwa mujibu
wa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu nao hawakupaswa kugombea.
Hao
ni pamoja na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Viwanda, Biashara na
Masoko, Dk Abdallah Kigoda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Emmanuel
Nchimbi.
Wengine
ni Wabunge Deo Filikunjombe (Ludewa), Mussa Azzan Zungu (Ilala), Dk
Hamis Kigwangalla (Nzega) na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi).
Salma akosa mpinzani Lindi
Katika hatua nyingine Mke wa Rais, Salma Kikwete amerudisha fomu ya kuwania ujumbe wa Nec Taifa kupitia Wilaya ya Lindi Mjini.
Katibu
wa CCM Wilaya ya Lindi Mjini Mohamed Kateva, alisema jana kwamba Salma
ni mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo katika wilaya yake.
Kateva
alisema mwisho wa kurudisha fomu ilikuwa Agosti 28, mwaka huu na mpaka
tarehe hiyo hakukuwa na mtu mwingine aliyekuwa amejitokeza kuwania
nafasi hiyo....
www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment