Siri Mauaji Iringa Zaanza Kufichuka
POLISI
WALIOTEKELEZA OPERESHENI WADAIWA KUSAFIRISHWA KUTOKA MIKOA MINGINE,
WAANDISHI WA HABARI IRINGA WASUSIA MKUTANO WA DCI MANUMBA
INADAIWA
kwamba askari waliokuwa katika operesheni ya kuzuia mkutano wa Chadema
katika eneo la Nyololo wilayani Mufindi, Iringa na ambayo ilisababisha
kifo cha Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi walitolewa katika mikoa ya
Dodoma, Morogoro na Mbeya.
Tayari
tukio hilo limeibua mjadala mzito kiasi cha kumfanya Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kuunda tume huru kubaini chanzo cha
tukio hilo. Marehemu Mwangosi alizikwa juzi nyumbani kwao Tukuyu, mkoani
Mbeya.
Habari
za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kuwa polisi hao
kutoka mikoa hiyo mitatu wakiwa wamesheheni vifaa mbalimbali likiwamo
gari la maji ya kuwasha, walisafiri siku moja kabla ya mkutano huo wa
Chadema na baadaye kuzuka vurugu zilizosababisha kifo hicho.
Marehemu Mwangosi aliuawa kwa mlipuko unaodhaniwa kuwa ni wa bomu ambao ulisambaratisha vibaya sehemu kubwa ya mwili wake.
Chanzo
cha habari kutoka mkoani Dodoma kilisema: “Hapa kwetu kuna askari 10 na
tunawafahamu kwa majina. Waliondoka hapa siku moja kabla ya tukio hilo
wakiwa na gari la washawasha.”
Chanzo
hicho kilisema kwamba awali, hawakuwa wakifahamu kama baadhi ya wenzao
walichukuliwa na kupelekwa Iringa. “Tulikuja kuona kwenye gazeti picha
na tulipofuatilia tukaelezwa kuwa ni kweli Dodoma ilitoa askari kwenda
Iringa.”
Askari
mwingine aliyekuwa katika operesheni hiyo ambaye jina lake
tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma, alikiri kuwa hadi jana baadhi yao
walikuwa bado wako Iringa na kwamba walikwenda kwa agizo la wakubwa
wake wa kazi.
“Sisi
ni Watanzania, lakini tumelazimika kuyafanya hayo kwa sababu ya mkate
(malipo). Kwa kweli haikuwa haki, kuwatoa askari na silaha kutoka mikoa
mitatu kana kwamba wanakwenda kupigana vita!”
Alidokeza
kwamba, askari wote waliotoka Dodoma walikuwa njiani kurudi mkoani
humo, jana lakini gari la maji ya kuwasha liliendelea kubaki huko Iringa
likiwa na dereva wake na askari mmoja mwenye cheo cha inspekta. Askari
huyo alisema kwamba gari hilo lililazimika kubaki kutokana na hitilafu.
“Wengine
wamerudi lakini, kuna wengine wenye gari la kuwasha bado walikuwa
Iringa, gari lao limepata hitilafu kidogo,” kilisema chanzo hicho kutoka
mjini Dodoma.
Mmoja
wa askari hao alidaiwa kwamba hiyo inaweza kuwa moja ya sababu ya
askari hao kumshambulia marehemu Mwangosi wakati mwenzao anayemfahamu
akijaribu kuwazuia. "Hii inaonyesha kuwa askari hao waliompiga walikuwa
hawamjui na huyu aliyekuwa akiwazuia, alimjua.”
Makamanda watupiana mpira
Alipoulizwa
kuhusu taarifa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen
hakukubali wala kukanusha na badala yake alisema: “Mambo yote hayo
yanatakiwa kujibiwa na Kamanda wa Iringa.”
Aidha,
alisema sakata la kifo cha mwandishi huyo kwa sasa liko katika vyombo
vya uchunguzi hivyo asingekuwa tayari kulizungumzia.
“Siwezi
kusema kama askari wangu walikwenda huko au hawakwenda, isipokuwa
ninachoweza kusema ni kwamba suala hilo lipo katika vyombo husika hivyo
waachiwe wao au Kamanda wa Iringa ndiye mwenye majibu.”
Alipotajiwa
jina la mmoja wa askari aliyeonekana katika picha za video na magazeti
za tukio hilo kwamba anatokea katika moja ya vituo vyake, kamanda huyo
alisema: “Mimi yakitokea Dodoma nitazungumza wala siyo mtu mwingine kwa
hiyo, mambo ya Iringa siwezi kuyazungumza na kama tutaanza kila Kamanda
kuzungumza jambo hilo hamuoni kuwa itakuwa ni kama vurugu?”
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alipopigiwa simu yake iliita tu bila kupokewa.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile
alisema kwa kuwa tukio hilo limefanywa na polisi, mambo mengi
yatazungumzwa lakini akasisitiza kwamba hajapeleka askari Iringa.
Alisema
hakukuwa na agizo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi wala ombi
kutoka Polisi Iringa kutaka askari wa kuongeza nguvu... “Taarifa hizo ni
za uzushi kwani hazina ukweli wowote.”
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani alikanusha pia kuwapeleka
askari wake Iringa akisema: “Hizo taarifa siyo za kweli. Hakuna askari
yeyote aliyekwenda Iringa wakati wa vurugu zile.”
Mkutano wa DCI wavunjika
Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba hakutaka
kuzungumzia suala hilo akisema: “Hayo yote yameundiwa tume ngoja
tuiachie ifanye kazi yake.”
Awali,
DCI Manumba aliitisha mkutano na waandishi wa habari mkoani Iringa,
ambao hata hivyo, ulivunjika baada ya kutokea kutoelewana baina yao.
Manumba
alitaka kueleza ripoti ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, lakini
waandishi hao walikataa kumsikiliza wakisema hawauamini uchunguzi huo
kwa kuwa ulifanywa na polisi peke yao.
Kabla
Manumba, hajaanza kuzungumza, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari
Iringa (IPC), Frank Leonard alisema kutokana na msimamo wa waandishi wa
habari wa mkoa huo hakutakuwa na uhusiano wa kikazi na polisi hadi pale
tume zilizoundwa kuchunguza kifo hicho zitakapotoa taarifa sahihi juu ya
mauaji hayo.
“Msimamo
wetu ni kusitisha uhusiano wa kikazi baina yetu na jeshi la polisi
hususan Mkoa wa Iringa, tumekuja hapa kwa sababu DCI umetuita na kama
unataka kutupa taarifa ya kifo cha ndugu yetu basi waambie hao maofisa
wa jeshi wa Iringa watoke nje,” alisema Leonard.
Akijibu
madai hayo Manumba alisema: “Nia yangu ni kutoa taarifa ya uchunguzi wa
kifo cha Mwangosi, ndiyo maana niliwasiliana na mwenzenu ili tuweze
kuzungumza, Polisi Iringa wataendelea kuwepo na waandishi wa habari
mtaendelea kuwepo, matukio kama haya yapo na yataendelea kuwepo.”
Licha ya maelezo hayo, hakuna mwafaka uliofikiwa na mkutano huo ukavunjika.
Akizungumza
kwa simu na gazeti hili baadaye, DCI Manumba alisema: "Ni vyema wao
wangenisikiliza kujua ninataka kuwaambia nini. Lakini, kwa kuwa kuna
mkanganyiko, nimeona ni vyema jambo hili lisubiri tume ndipo watakuja
kulizungumza.”
Waikataa Tume ya Nchimbi
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeiponda tume ya Dk Nchimbi
kikieleza kuwa imeundwa ili kurudisha uhusiano kati ya Polisi na
waandishi wa habari na si kutafuta chanzo cha tatizo.
Juzi,
Dk Nchimbi alitangaza kamati ya kuchunguza mauaji hayo inayoongozwa na
Jaji Mstaafu, Steven Ihema na wajumbe, Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), Theophil Makunga, Mwakilishi wa Baraza la Habari
Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, Mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa
Polisi (DCP), Isaya Mngulu.
Mkurugenzi
wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu alisema
Dar es Salaam jana kwamba: “Hii si tume ya kuchunguza mauaji, bali ina
lengo la kurudisha uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na waandishi
wa habari ili kuwasahaulisha wananchi kwa sababu imeundwa na waziri
ambaye naye anatakiwa kuhojiwa.” “Tunamwomba Rais Jakaya Kikwete ateue
tume kama anavyoelekezwa na Sheria ya Tume za Uchunguzi ya mwaka 1992,
ambayo inaruhusu kumhoji yeyote kasoro yeye Rais.”
Lissu
alisema Rais Kikwete angeunda tume hiyo na Waziri Nchimbi na IGP Said
Mwema wanatakiwa kujiuzulu ili kupisha uchunguzi akidai kwamba kuna
uwezekano mkubwa kwamba walitoa amri ya mauaji hayo.
“Dk
Nchimbi anatakiwa kumuiga Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi
ambaye alijiuzulu akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya kutokea
mauaji, akijiuzulu atajijengea heshima tofauti na sasa kwani wananchi
wamesikitishwa na mauaji hayo,” alisema Lissu.
Mwanasheria
wa Chadema, Mabere Marando alidai kwamba kuna mkakati uliowekwa na
Serikali wa kukidhoofisha Chadema baada ya kuonekana kwamba ni tishio
kwa CCM.
Mbali
na Chadema, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), pia
limesema halina imani na kamati hiyo likisema imekuwa kawaida kwa
Serikali kuunda tume ambazo hazileti ripoti kwa wananchi.
“Tume
zimekuwa zikiundwa bila faida yoyote, huku zikipewa muda kuchunguza
yaliyotokea lakini matokeo yake huwa hakuna ripoti wanayorudisha,”
alisema Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya.
Kaaya
alisema tume zimekuwa zikiundwa na kuigharimu Serikali fedha nyingi za
walipa kodi, lakini ripoti zake zinaendelea kuwa siri.
Imeandikwa na Habiel Chidawali, Dodoma, Hamida Sharrif Morogoro, na Tumaini Msowoya, Iringa na
Lasteck Alfred na Juliana Malondo.
No comments:
Post a Comment