Nimesikitishwa
na kauli za jazba na mwangwi wa kiwewe za Mhe Dr. W Slaa alipokuwa
Iringa juzi hadi kuniita mnafiki, mwongo, mtu wa hatari n.k Hali
hii inatia mashaka juu ya uwezo wa kiongozi huyo wa kisiasa kuhimili
kukosolewa ambayo ni sifa muhimu ya maisha ya mwanasiasa yeyote
hususani anapojinadi kuwa anaweza kuchukua madaraka ya kuiongoza nchi.
Kauli zisizo na staha alizozitoa Dr Slaa dhidi yangu kama vile sifai hata uongozi wa kata zinadhihirisha mambo mawili:
-Dr Slaa ni dicteta. Hana uvumilivu. Ana hulka ya kujiskia kwamba mawazo yake hayapingwi.
-Ni
mzushi asiyeogopa kusema na kupindisha mantiki ya jambo ili tu
kushinda hoja. Iweje mtu aliyenibembeleza nigombee uraisi kupitia chama
chake mwaka juzi leo aseme sifai kuongoza hata kata kwasababu tu
nimetamka ukweli juu ya udhaifu wa chama chake cha siasa?
Niliyoyasema
pale Karagwe majuzi katika uchambuzi wangu wa vyama vya siasa nchini
ni kwamba CHADEMA wamekuwa hodari wa kukosoa na kuishambulia CCM na
serikali zake lakini wanasau kuwa ili wawe mbadala kwa kuiongoza nchi
hawana budi kurutubisha safu yao ya uongozi nawe na watu wakutosha
kuweza kushika madaraka ya ngazi mbalimbali za uongozi wa Taifa.
Kuukataa ukweli kwamba safu ya uongozi wa CHADEMA ni nyembamba ni
kujidanganya tu.Kupita mikoani kutangaza kwamba matatizo yote ya
wananchi yanatokana na CCM ni kazi rahisi na ina mvuto wake kisiasa
lakini mwanasiasa makini hana budi kwenda mbele zaidi ya hapo. Hana
budi kutuambia wapiga kura mipango ya chama chake inayoeleweka na
inayotekelezeka na iliyo makini kukabiliana na changamoto mbalimbali za
maendeleo ya nchi. Ahadi za alinacha za tiba bure, elimu bure bila
kuonyesha vyanzo halisi vya mapato ni porojo tu. Kusema kwamba
raslimali za nchi kama vile gesi asilia, madini, makaa ya mawe, utalii
zinatosha kuondoa umaskini ni nadharia tupu ambayo uhalisia wake hauna
budi kubainishwa kwa mikakati dhahiri na thabiti ya kiutawala
(uendeshaji) inayoweza kuchuma utajiri huo kwa ufanisi, kwa uendelevu
na kwa faida ya wengi 1. Kuhusu mwenyekiti Mh Mbowe – MB
Katika hotuba yangu sikukejeli
uzoefu wa Mhe Mbowe, wala sijasema Mhe Mbowe ni mcheza disko.
Niliuchambua wasifu wa viongozi wa CHADEMA na kutamka uzoefu wa Mhe
Mbowe katika vitega uchumi vya burudani hii siyo kudharau bali ni
kutamka ukweli tu.Huwezi kuuelezea wasifu wa Mhe Mbowe bila kuelezea
mchango wake mkubwa katika tasnia ya burudani.Mmoja wa maraisi maarufu
wa marekani (USA)alikuwa ni mcheza sinema Ronald Reagan.Na hapa Tanzania
tulikuwa na mzee R. Kawawa ambaye alianzia katika tasnia ya uigizaji,
kwa hiyo Mhe Mbowe au Dr.W. Slaa anaweza akawa Rais wetu kwa maana ya
kupigiwa kura za uchaguzi wa demokrasia.Kumudu au kutoyamudu madaraka
hayo ni suala tofauti. Tathmini yangu ilihusu safu nzima ya uongozi wa
CHADEMA kwa ujumla wao.Ni safu nyembamba mno.
2. Kujiunga na CHADEMA
Kama alivyosema Dr. Slaa Chadema
walifanya jitihada ya kunishawishi niingie CHADEMA 2010 na niwe mgombea
wao wa Urais. Jambo hili nililitafakari na kutafuta ushauri kwa watu
wangu wa karibu na nikabaini kwamba:-
-CHADEMA wana migawanyiko yao ya uongozi tena ni ya hatari kwasababu ni ya kikanda za nchi – yaani nani anatoka wapi.
-Kutokana
na yaliomo katika ilani yao ya uchaguzi 2010 – 2015 nilibaini mambo ya
kiitikadi ambayo siyakubali kama vile sera ya majimbo. Sera ya majimbo
inawezekana katika nchi ambazo ni tajiri na pia isiyo na tofauti kubwa
ya hali ya maisha baina ya kanda mbalimbali za nchi kama vile Marekani
(USA). Kuleta majimbo Tanzania ambako kuna tofauti kubwa za
kimaendeleo baina ya Kaskazini, Mashariki, kati, Kusini na Magharibi ni
kusababisha nchi ichanike vipande vipande. Huduma bure za elimu
kuanzia chekechea hadi chuo kikuu na huduma bure za afya kwa wote ni
ndoto na ni ghilba kwa wananchi. Isitoshe siamini kwamba kazi ya
Serikali yoyote Duniani ni kuwalea Wananchi kwa umaskini huku
ukiwaahidi huduma za bure badala ya kuwaendeleza wajitume na waongeze
kipato ili wamudu gharama za maisha. Kwa hiyo nisingeweza kuwa mgombea
Uraisi ndani ya chama ambacho itikadi zake za msingi sikubaliani nazo.
Baada ya hapo nisingeweza eti baada ya uchaguzi Mkuu niombe kugombea Uspika kupitia chama cha CHADEMA.
3. Kuhusu CCJ
Kama
ilivyo kawaida kwa vyama vya siasa kutafuta wagombea bora, CCJ ni
miongoni mwa vyama vilivyonifuata mimi na baadhi ya wanasiasa wakati wa
maandilizi ya uchaguzi mkuu. jambo hili si la siri wala la ajabu na
Nimelizungumza hili mara nyingi. Isitokee katika mfumo wa vyama vingi
vya siasa mtu kutoka chama kumoja cha siasa na kujiunga na chama
kingine haiwezi kusemwa kuwa ni uhaini. Na kama Ningeridhika na mambo
yao ningejiunga na CCJ mwaka 2010 lakini sikufanya hivyo. Pia ni uzushi
usio na msingi kunihusisha na uanzishaji wa chama hicho. Waanzilishi
wa chama hicho cha siasa wanajulikana na wapo hai, ni haki ya kikatiba
ya kila Mtanzania kuanzisha au kujiunga Binafsi na chama chochote cha
siasa.
4. Madai mengine
Eti
nilitamka kwamba ningehamia chadema na Wabunge wa CCM 55 ni porojo za
Dr. Slaa kama ulivyo usemi ningeihama CCM siku chache kabla ya kuvunjwa
Bunge la 9.
Inashangaza
kwa Dr Slaa kukejeli uendeshaji wa bunge la 9 ambalo ndilo lililowapa
fursa watu kama yeye kujulikana na kujipatia umaarufu.
Haya
madai ya mimi nikiwa Spika kukwamisha uchunguzi wa Meremeta na
Richmond ni kutokana na hisia tu za chuki. Taratibu za Kibunge
hazimwezeshi Spika kuwa Dikteta anayeamua nini kijadiliwe na nini
kisijadiliwe. Yote yapo katika kanunu za Bunge. Maamuzi ya Bunge si
lazima yawe ni ya Spika.
Kuhusu
ofisi ya Mbunge jimboni Urambo mahasimu wangu ndani ya CCM na nje yake
wameng’ang’ania kwa makusudi maalum kuiita ofisi ile kuwa ni ya Spika.
Michoro yake na gharama zake hata ukijumuisha samani haifikii tarakimu
za ajabu wanazotaja mahasimu wangu kujenga hoja istoshe ofisi hiyo
haina maslahi yeyote binafsi kwangu Aidha viongozi wengine waliofikia
hadhi za juu mathlani ya uwaziri mkuu nao wamejengewa majimboni ofisi
zinazolingana na hiyo
Porojo
nyingine binafsi kama vile kumuhusisha mke wangu kumpigia simu Dr Slaa
kumsihi anisaidie kisiasa ni upuuzi wa aina yake unaodhihirisha
umahiri wa Dr.Slaa katika siasa za kiwango cha chini.
5. HITIMISHO
Mimi
nikiwa mwanasiasa mzoefu na mkongwe nimetoa ushauri na nitaendelea
kutoa ushauri kwa makundi mbalimbali nchini.Kuniambia naingilia mambo
ya CHADEMA ni kichekesho.Wakiwa wao ni chama cha siasa kinachoendesha
harakati za kuwania kuchukua madaraka ya kuongoza nchi ambayo mimi ni
raia wasitazamie kuwa sisi wapiga kura tutaacha kuwachambua.Wanalo
tatizo kubwa la safu nyembamba mno ya uongozi, Kulingana na majukumu ya
kuendesha nchi. Kujilinganisha na safu ya uongozi ya Baba wa Taifa Mwl
Julius Nyerere ni mzaha wako wapi akina R.M Kawawa, Pauli Bomani,
George Kahama, Amir Jamal, Solomoni Eliufoo, Tewa Saidi, Tewa Abdallah,
Fundikira wa CHADEMA? Kutembea nchi nzima kuhamasisha chuki dhidi ya
serikali iliopo madarakani ni jambo jepesi lakini Watanzania walio
makini wanahitaji maelezo ya mipango mbadala ya uchumi kuinua hali za
maisha yao na kuiona safu ya uongozi itakayowezesha kwa dhati kubuni na
kusimamia mikakati endelevu ya kuondoa umaskini kujenga uchumi imara na
kuimarisha umoja wa watanzania
No comments:
Post a Comment