Wajumbe Wa Baraza La WaWakilishi Waitembelea Tume Ya Katiba
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imesisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali
wakiwemo wanasiasa, asasi za kiraia na kidini kuwaacha wananchi kutoa
maoni yao binafsi kuhusu Katiba Mpya.
Akizungumza
na Wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza la
Wawakilishi Zanzibar leo (Jumatatu, Septemba 17, 2012), Mwenyekiti wa
Tume hiyo Jaji Joseph Warioba alisema katika mikutano ya ukusanyaji wa
maoni inayoendelea, na kukusisitiza kuwa makundi na taasisi mbalimbali
vitapata nafasi ya kukutana na Tume na kutoa maoni yao.
Aidha
Jaji Warioba alisema kuwa changamoto kubwa ambayo Tume hiyo
inakabiliana nayo ni wananchi kupewa mawazo ya kuzungumza na watu
wengine, jambo ambalo haliwasaidii wananchi .
“Makundi
ya watu, Taasisi za kirai na hata vyama vya siasa vimekuwa mstari wa
mbele kuwalisha wananchi mambo ya kuzungumza “ alisisitiza Jaji
Warioba.
Mwenyekiti
huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliwataka wawakilishi hao
kuisaidia Tume kuwaelimisha wananchi kuwa tayari kutoa maoni yao ya
moyoni na kukataa kabisa kupokea mawazo ya watu wengine ili katiba
itakayopatikana iwe inawakilisha mawazo yao.
Jaji
Warioba alikuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia
ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Ali Abdalla Ali ambaye
alitaka kujua changamoto ambazo Tume inakutana nazo katika utekelezaji
wa majukumu yake.
Jaji
Warioba amesisitiza kuwa viongozi wa makundi mbalimbali na vyama vya
siasa wana wajibu wa kuwaelimisha wananchi kutoa maoni yao binafsi
badala ya kuwaelekeza aina ya maoni wanayopaswa kuyatoa.
Akizungumzia
kuhusu muda uliopangwa katika kutekeleza kazi hiyo, Jaji Warioba
alieleza kuwa pamoja na changamoto hiyo lakini Tume imejipanga
kumaliza kazi yake ndani ya muda iliopewa kisheria.
“Tume
imejipanga kuhakikisha ifikapo April 26 2014 katiba mpya inakuwa
tayari. Kimsingi mazingira ya hali ya kisiasa nchini yanalazimisha
kuwepo na katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ili kuweka
maelewano ya kitaifa” alifafanua.
Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi wapo katika ziara ya taasisi mbalimbali za Muungano zilizopo Dar es Salaam.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ali Abdallah Ali amesema
Wajumbe wa Kamati watatumia uzoefu na elimu waliyoipata katika ziara yao
ili kuisaidia Tume kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Wajumbe
hao walipata nafasi ya kutembelea vitengo vya Utafiti na Taarifa
Rasmi (Hansard) ambapo waliweza kuona jinsi maoni yanavyopokelewa na
na kufanyiwa kazi .
Ismail Ngayonga,
Information officer,
Constitutional Review Commission (Tanzania),
PO Box 1681,
Dar es Salaam,
Tel: +255 (0) 22 2133425,
Fax: +255 (0) 22 2133442,
Mobile: +255 (0) 717 084252
Email: ngayongaismail@yahoo.com,
Website: www.katiba.go.tz
No comments:
Post a Comment