Hatimaye ripoti ya tuhuma za rushwa ya Wabunge yatua kwa Spika


Spika wa Bunge, Anne Makinda

Spika  wa Bunge, Anne Makinda amepokea taarifa ya uchunguzi kuhusu tuhuma zilizowahusu Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya Wabunge ya kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini (2012/2013).

Ripoti hiyo inafuatia Spika Makinda kuunda Kamati ndogo ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuchunguza tuhuma hizo wakati wa Mkutano wa Nane wa Bunge uliofanyika Juni – Agosti, 2012.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge jana kwa vyombo vya habari, ilisema kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge (2007), Spika atatoa mwongozo kuhusu utaratibu wa kufuata kuhusu uwasilishaji wa Taarifa hiyo Bungeni ambapo Spika akatoa uamuzi ama Kamati kuwasilisha Taarifa hiyo Bungeni.

Kamati hiyo ndogo ilikamilisha kazi yake kama ilivyoelekezwa kwenye Hadidu za Rejea na kukabidhi Taarifa ya Uchunguzi huo kwa Spika wa Bunge.

“Spika atatoa taarifa ya kukamilika kwa uchunguzi huo Bungeni wakati wa Mkutano wa Tisa wa Bunge unaotarajia kuanza Oktoba 30,” ilisema taarifa hiyo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment