.Awatahadharisha vijana dhidi ya rushwa
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye
Waziri Mkuu
Mstaafu, Frederick Sumaye, amewatahadharisha vijana kujiepusha na
rushwa, hususani inayolenga kununua uongozi wa nchi, ukiwemo urais.
Amesema, ili vijana waishi kwa ustawi na maendeleo wanayostahili,
wanatakiwa kukataa mambo machafu yanayofanywa na baadhi ya viongozi,
likiwemo la rushwa kipindi cha uchaguzi.
Sumaye alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika mdahalo
ulioandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ikiwa ni
adhimisho la miaka 13 baada ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere.
Pamoja na mambo mengine, washiriki waliangalia moja ya hotuba za Mwalimu Nyerere iliyoelezea, 'nyufa katika Muungano na rushwa.'
Hii ni mara ya pili katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja kwa Sumaye
kulalamikia rushwa, ikiwa ni baada ya kushindwa katika uchaguzi wa
ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwenye uchaguzi huo kupitia wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, Sumaye
alishindwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na
Uwezeshaji), Dk Mary Nagu.
Sumaye alieleza kushangazwa na baadhi ya wanaotaka kuwania urais (bila
kuwataja majina), wakiwatumia vijana kwa kuwapa rushwa ili waweze
kuwapigia kura.
"Kwa nini umtumie kijana ukitaka urais, ukiona mtu anazunguka na pesa
kutaka uongozi huyo sio kiongozi, ukiona mtu anakununua kwa madaraka
ujue naye kanunuliwa na atawahudumia watu waliomnunua, waogopeni watu
hawa wapo kwa maslahi yao binafsi na sio ya Taifa," alisema na kuongeza:
"Hii imefanya badala ya kusema huyu ni kiongozi tunayemtaka, tunaishia
kusema ana nini, ana fedha au anatoa rushwa, mkifanya hivi mtamuweka mtu
asiye na uwezo na sifa madarakani,” alisema.
Alisema hali hiyo inapotokea, raia hasa vijana wanabaki kulalamika bila kujua chanzo ni rushwa iliyotolewa.
“Sio kweli Watanzania wanapenda rushwa na ipo siku watalipuka, sisi
tunaopinga rushwa hadharani tunataka Watanzania wasilipuke, vijana
mkasimamie haki katika taifa,” alisema.
Alitoa mfano wa chaguzi ndani ya Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM),
kwamba wenye fedha wamefanikiwa kuwagawa (vijana) kama ilivyokuwa kwa
watesi walivyogawana vazi la Yesu Kristu.
Sumaye alisema Mwalimu Nyerere alilisimamia Taifa lakini sasa linateketezwa na kueleza kuwa ipo siku Watanzania watajuta.
Alisema vijana wana nafasi ya kuliokoa Taifa lisiende kubaya zaidi na kuwataka wapige vita rushwa hadharani.
Alihoji, “tujiulize, angefufuka Mwalimu leo, ungekuwa mmoja wa wenye
furaha kwenda kumlaki au wataokimbia na kutokomea porini ili uso wake
usikutane na wako.”
MATUMIZI MABAYA YA URAIS
Sumaye alisema matumizi mabaya ya taasisi ya urais ni tatizo kubwa
Afrika, hivyo kuwa sababu ya machafuko na kutokuridhika kwa wananchi
nchi nyingi.
Alisema utawala wa Mwalimu Nyerere ulifanikiwa kutoa elimu ya bure kwa
misingi ya usawa, lakinihivi sasa shule za umma zimesahaulika hivyo
kutoa kiwango duni cha elimu.
Akielezea kuhusu ajira kwa vijana, alisema Mwalimu Nyerere alipoanzisha
elimu ya kujitegemea lengo lake lilikuwa ni Watanzania wasitegemee ajira
za maofisini, lakini sasa suala hilo limekuwa kero.
Mkuu wa chuo hicho, Dk. John Magotti, alisema Mwalimu Nyerere alipinga
dhuluma, ukandamizaji, ubaguzi wa rangi na aliacha misingi muhimu utu,
uhuru na misingi ya kujitegemea.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment