WALIMU WAGOMEA SIKU YAO
CHAMA
cha Walimu Tanzania (CWT) kimegoma kushiriki maadhimisho ya Siku ya
Walimu Duniani inayoadhimishwa leo kwa madai kina huzuni na hakina
mafanikio yoyote ya kuwaambia walimu.
Aidha, chama hicho kimetoa
mwito kwa Serikali kukubali ushauri wa Bunge na uamuzi wa Mahakama, ili
warudi katika meza ya majadiliano kwa ajili ya kuendeleza walipoachia.
Katibu
wa CWT, Ezekiel Oluoch alisema hayo jana Dar es Salaam wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo ambayo
kaulimbiu yake ni ‘Kuwatetea walimu’.
“Kesho (leo) ni Siku ya Walimu
Duniani, kwa bahati mbaya hatutakuwa na sherehe ama maadhimisho kwani
hakuna chochote cha kuelezea … hatuwezi kusherehekea tukiwa na matatizo
mengi ambayo hayajafikia suluhu,” alisema Oluoch na kuongeza kuwa
wataadhimisha siku yao wakiwa kazini na wamekata tamaa.
Alisema
mwajiri wao ambaye ni Serikali hajalipa madai ya wakufunzi wa vyuo vya
ualimu, hajashughulikia madai ya walimu ambayo hayajalipwa na kutoajiri
walimu waliohitimu ingawa fedha zimetengwa na Bunge.
Alisema katika
siku hiyo, CWT inatoa mwito kwa Watanzania na jumuiya za kimataifa
kujitokeza kutetea walimu dhidi ya manyanyaso wanayopata kutokana na
mishahara duni isiyokidhi mahitaji muhimu ya kila siku.
Pia alitaka
walimu kushikamana katika kudai maslahi bora zaidi kama watumishi
wengine wa umma na Serikali ilipe madeni yote wanayodai walimu,
wakufunzi wa vyuo vya ualimu nchini pamoja na wakaguzi wa shule.
Kuhusu
kurudi katika meza ya majadiliano, Rais wa CWT, Gratian Mukoba alidai
Serikali imegoma kukutana na chama hicho kama ilivyoagizwa na Mahakama
na Bunge.
Alisema pamoja na leo kuwa Siku ya Walimu, Serikali
imekataa mapendekezo ya CWT ya kuteua timu ya majadiliano nje ya chombo
cha majadiliano ya pamoja kwenye utumishi wa ualimu ili madai ya walimu
yashughulikiwe ndani ya mwaka huu wa fedha.
“Hadi sasa Serikali
imekiuka amri ya Mahakama ya Kazi ambayo iliagiza pande zote, yaani CWT
na Serikali zirudi kwenye meza ya majadiliano… kwa uelewa wetu, meza
iliyokuwa inatumika kwa majadiliano kabla ya mgomo ndiyo inayostahili
kutumika kuendeleza mazungumzo kati ya pande hizi,” alisema Mukoba.
Alisema
CWT inalaani kwa nguvu zote ukaidi huo wa Serikali ambao hauna tija kwa
nchi, bali unazidi kuwasababishia walimu kuishi maisha magumu yasiyo na
mfano na kudhulumu wanafunzi haki yao ya kupata elimu.
Akijibu hoja
ya Serikali kukaidi uamuzi wa Mahakama na Bunge, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alisema Serikali
inapanga tarehe mwafaka ya kukutana na kwamba haijakaidi agizo hilo.
Alisema baada ya CWT kuwaandikia wako katika majadiliano na kwamba wameahidi kukutana ili kuzungumza.
CHANZO: HABARILEO
No comments:
Post a Comment