Chuo kimoja
kikuu kimefungwa nchini Nigeria baada ya ghasia kuzuka kuhusiana na
tukio la kuuawa kwa wanafunzi wanne, waliodaiwa kuiba komputa na simu za
mkononi.
Kanda ya video ya kuogofya kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube, ilionyesha wanne hao wakiuawa kinyama.
Wanafunzi wanasema kuwa wanne hao waliuawa baada ya kudhaniwa kuwa wezi kutoka katika kijiji cha Aluu.
Chuo kikuu cha Port Harcourt (Uniport)
kiliwaamuru wanafunzi kwenda nyumbani,baada ya maandamano yaliyokuwa
yanafanyika kukumbwa na ghasia huku Nyumba na maduka zikichomwa.
Waandishi wa habari wanasema kuwa polisi wa
kupambana na ghasia pamoja na wanajeshi, wameenda katika chuo hicho,
ambacho maafisa wakuu wanasema kitasalia kufungwa hadi hali
itakapotulia.
13 wakamatwa
Wanafunzi waliziba barabara moja kuu karibu na
chuo kikuu kwa masaa kadhaa siku ya Jumanne na kuzuia magari kwenda
ndani au kutoka nje ya mji wa Port Harcourt.
Punde wakaanza kuelekea katika eneo la Aluu, ambako wanafunzi waliuawa na genge la watu mnamo siku ya Ijumaa.
Nyumba zilizovamiwa zilikuwa za baadhi ya washukiwa wa mauaji ya wanafunzi hao.
Kanda ya video,iliyotumwa katika mtandao wa
YouTube mwishoni mwa wiki, inaonyesha wanaume wanne wakivuliwa nguo na
kutembezwa uchi kabla ya kuteketezwa.
Mmoja wa wanafunzi mwenzao Paul Irabor, aliambia
BBC kuwa wanne hao walikuwa wameenda kuchukua pesa walizokuwa wanadai
mdeni wao, wakati waliposhambuliwa kwa dhana ya kuwa wezi.
Wanafunzi hao inaarifiwa walichukua simu za
mkononi na komputa baada ya mdeni wao kukosa kuwalipa ndiposa
wakadhaniwa kuwa walikuwa wameiba vitu hivyo.
Watu kumi na tatu akiwemo kiongozi mmoja wa
kijiji cha Aluu, ambacho kinapakana na chuo kikuu katika eneo
linalojulikana kama Choba , wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment