Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa
KATIKA kuonyesha hali si shwari ndani ya
Chadema, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) wa chama hicho,
Juliana Shonza amesema ameamua kumshtaki Mwenyekiti wake, John Heche
kwa kumuita kuwa ni msaliti wa chama na kwamba anatumiwa na CCM na
kuamua kumfukuza nafasi yake bila kutoa nafasi ya kusikilizwa.
Pia, amemlipua Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk
Willibrod Slaa akidai kuwa amefanya ufisadi ndani ya chama kwa
kujikopesha Sh140 milioni ambazo hajazilipa hadi sasa.
Mbali na hilo,
amemshukia Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa kudai kuwa
anatoa kauli za kukurupuka ambazo zinakiyumbisha chama hicho kikuu cha
upinzani nchini.
Shonza alitoa kauli hizo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juu ya tuhuma
zilizotolewa na mwenyekiti wa Bavicha na kuhusu kufukuzwa kwake ndani ya
chama akiwa na wenzake Mtela Mwampamba na Habibu Mchange.
“Heche na Mbowe wamenifedhehesha kwa kauli zao
na wamenichafua na kunidhalilisha mbele ya umma wa Watanzania, hivyo
nitapambana nao kuhakikisha haki yangu inapatikana,” alisema Shonza.
Shonza alisema kwamba yeye bado ni makamu
mwenyekiti wa Bavicha na mwanachama halali wa Chadema kwa kuwa hadi
anazungumza hakuwa amepewa barua ya kufukuzwa kwa kuwa kikao kilichotoa
uamuzi huo ni batili.
Alisema kikao kilichoitwa ni cha kamati
tendaji na kufikia maamuzi ya kumfukuza kilikuwa batili kwa kuwa katiba
pamoja na mwongozo wa Bavicha ulikiukwa, kitu kinachosababisha aeleze
kuwa uamuzi uliotolewa na kikao hicho yalikwishapangwa na viongozi wa
kitaifa.
“Nasisitiza kwamba ni ukweli uliowazi kwamba
ajenda na maazimio ya kikao hicho yalikwishaamuliwa hata kabla ya kikao
hicho, kwa sababu taarifa za kufukuzwa kwetu zilikwishaanza kusikika
kwenye mitandao ya kijamii kabla hata ya kamati tendaji batili,”alisema
Shonza.
Alisema mkakati wa Heche na vibaraka wake
umejikita kutukuza ukanda ndani ya chama waziwazi, akieleza kuwa watu
waliofukuzwa ndani ya chama hicho wanatokea Ukanda wa Nyanda za Juu
Kusini haswa Mbeya wakati vijana wa Kaskazini wameachwa kwa madai kuwa
wametoa ushirikiano.
“Natarajia kuomba ufafanuzi wa kikatiba juu ya
shutuma zilizotolewa dhidi yangu na Heche kwa kuwaaminisha Watanzania
uongo wake,”alisema Shonza.
Kuhusu Mbowe
Alisema kuwa amesikitishwa na
kauli ya kiongozi wake huyo katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba,
madai aliyoyatoa ni ya kitoto kwani ni kitu cha kushangaza kwa kuwa yeye
Juliana hayajui ni madai gani hayo.
Alisema kama madai ambayo Mbowe anadai ni ya
kitoto ni ya yeye kuhoji kwa nini chama hakiweki akiba kwenye akaunti
kwa ajili ya uchaguzi wa 2015 kama ilivyokubaliwa kwenye baraza kuu basi
itakuwa ni ajabu.
Kuhusu Dk Slaa
Alisema inashangaza kwa
mwenyekiti wa chama anafumbia macho hatua ya Dk Slaa kujikopesha pesa ya
ruzuku ya Watanzania zaidi ya Sh140 milioni, kwani ni kinyume na
utaratibu uliopo.
Shonza alisema Dk Slaa kama katibu mkuu wa chama ndiye mtendaji,
hivyo fedha hizo hakukopeshwa bali amejikopesha mwenyewe kwa masilahi
yake binafsi. Katika hali isiyokuwa ya kawaida aliibuka kijana mmoja
katika mkutano huo jana akidai kuwa ametumwa kuwasilisha barua za
kufukuzwa kwa Shonza kwenye chama lakini hazikupokewa na wahusika.
Akizungumzia suala hilo, Heche alisema uamuzi
ulishafanywa na kamati tendaji ya baraza na kwama vielelezo vya kwamba
Juliana ni msaliti vipo na hali ya usaliti itamwandama milele.
“Rufaa
ya Chadema haikatwi kwenye vyombo vya habari, angekuwa na nidhamu
angeenda kukata rufaa kwenye vikao vingine vya chama,”alisema Heche.
Alipopigiwa
Dk Slaa ili kujibu tuhuma zilizotolewa na Shonza, simu yake ilipokelewa
na mtu ambaye hakujitambulisha akieleza kuwa Dk Slaa yuko kwe mkutano
wa hadhara.
“Dk yuko kwenye mkutano,”alisema.
Kwa upande wake, Mbowe hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani
Januari 9 mwaka huu, Mkurugenzi wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa na gazeti hili akieleza kuwa wao
hawahusiki na hujuma yoyote ndani ya Chadema, hivyo chama hicho kitafute
mchawi wake chenyewe.
Nape alisema CCM haihusiki na mgogoro wowote ndani ya Chadema hivyo kijipange na kutafuta mchwi wake.
No comments:
Post a Comment