Mradi wa gesi Kilwa ‘kuzaa’ hospitali ya kisasa ya kimataifa
Ramani ya hospitali hiyo
WASWAHILI husema, ‘mgeni njooo , mwenyeji apone’.
Usemi
huu una maana nyingi, lakini mojawapo ni ile ya kuona kwamba mara
nyingi mgeni afikapo, ujio wake huwa zawadi hata kwa wenyeji.
Kwa Watanzania ,wengi wao wanaposafiri kwenda kutembelea jamaa zao ni kawaida yao kubeba zawadi.
Utaratibu huu unaweza kushabihiana na utakaotokea katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ambako imegundulika gesi.
Kampuni
ya Statoil kutoka Norway ikishirikiana na Exxon Mobil iligundua gesi
katika Visiwa vya Zafaran na Lavan vilivyopo Kitalu 2, Ukanda wa Pwani
ya Tanzania, hususan Pwani ya Kilwa.
Mradi huo una gharama kubwa pia utafanywa na wageni ambao wana utalaamu wa miaka mingi katika biashara ya gesi duniani.
Kutokana na ujio wa wageni hao, Watanzania
hususan wakiwamo wakazi wa Kilwa, Lindi na Mtwara kwa jumla hawana budi
kupata faida za moja kwa moja na zingine zisizo za moja kwa moja.
Miongoni mwa faida zisizo za moja kwa moja ni gesi hiyo kutumika
kutengeneza umeme utakaopatikana kwa uhakika na kuuzwa kwa wananchi
wote.
Hata hivyo, ujio wa mradi huo kwa upande mwingine una faida kwao kutokana na kutoa ajira ambayo itazingatia uwezo.
Je wakazi wa Halmashauri ya Kilwa watapata faida gani ya kudumu kutokana na gesi hiyo?
Hili
ndilo swali ambalo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Adoh
Mapunda anasema walijiuliza baada ya kufika kwa wageni hao.
Mapunda anasema madiwani, watendaji na mkuu wa
wilaya walikaa na kutafakari kwa kina juu ya faida ya kudumu
itakayoonekana wilayani mwao kutokana na ujio wa mradi wa gesi.
“Sisi tulikataa kauli za kusaidiwa madawati kwenye shule zetu, ama kupewa dawa kwenye hospitali na zahanati zetu
Hii ni kwa sababu tuna uwezo nazo, badala yake
tukabuni mradi mkubwa wa kimataifa ambao utakuwa na faida ya kudumu kwa
Kilwa na taifa kwa ujumla”, anasema.
Anafafanua kwamba mradi huo ni
ujenzi wa hospitali ya kimataifa itakayolingana na ile ya Apollo nchini
India ambayo viongozi mbalimbali duniani hukimbilia kwenda kutibiwa.
Hospitali
ya aina hiyo itajengwa na mwekezaji na itaendeshwa na taasisi nyingine
ya kimataifa huku halmashauri ikiwa na hisa za kupata gawio la kila
mwaka kutokana na faida.
‘’Tulizungumza na wawekezaji, Statoil , kwamba
watujengee hospitali ya aina hiyo ambayo itakuwa na uwezo wa kutoa tiba
kwa viongozi wakiwamo marais wa Afrika na wakuu wa kampuni mbalimbali
Afrika zikiwamo kampuni za uwekezaji katika gesi , madini na hata
usafirishaji na wafanyabiashara wa nchi mbalimbali,’’ anafafanua.
Mapunda anasema mpango huo unatekelezwa
kupitia utaratibu uliopo kwenye mikataba kwa wawekezaji kuhusu
uwajibikaji na ushiriki katika masuala ya kijamii, Social Co-operation
Responsibility (SCR).
Anasema tayari Statoil imetenga Sh18 bilioni
kuanza ujenzi wa hospitali hiyo mjini Kilwa wakati wowote kuanzia mwaka
huu. Anafafanua kuwa michoro ya hospitali hiyo ipo tayari na imechorwa
kama lilivyokuwa jengo la kifalme yaani Kasri lililojengwa eneo la Kilwa
Kisiwani enzi za Sultan wa Kiarabu aliyekuwa akimiliki kisiwa hicho.
‘’Tunatarajia kwamba taasisi ya kimataifa ya
Aga Khan Foundation ndiyo itakayoendesha hospitali hii kwa kiwango cha
kimataifa . Tulikaa na kuzungumza pande zote tatu, yaani Kilwa, Statoil
na Aga Khan Foundation na kukubaliana kuanzisha hospitali hiyo, hivyo
tuna imani itaendeshwa kama ile ya Apollo,’’ anasisitiza Mapunda.
Anasema hospitali hiyo itaajiri madaktari
mabingwa kutoka ndani na nje ya nchi, itakuwa na wafanyakazi wataalamu ,
pamoja na wahudumu ambao wengi watatoka Halmashauri ya Kilwa.
Kutokana na hali hiyo, Halmashauri ya Kilwa inatoa wito kwa
wakazi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili malengo hayo
yatimie.
“Hospitali hiyo itaongeza majengo mengi ya
kisasa yakiwamo makazi ya wafanyakazi, hivyo ni jukumu la wakazi wa
Kilwa kujiandaa kwa kulima mazao mengi na kujenga nyumba za kisasa,’’
anahamasisha
Hadi sasa, Kilwa ina hospitali mbili, vituo vya afya vitano na zahanati 43, anaeleza mkurugenzi huyo.
No comments:
Post a Comment