Wabunge waagiza CAG kukagua hesabu TTB

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),Ludovick Utoh. 



KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imeiagiza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), baada ya kuonekana kuna mtiririko wa fedha usioeleweka kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kwenye bodi hiyo.


Ofisi ya CAG imetakiwa kufanya ukaguzi huo kwa hesabu za TTB kwa miaka mitano iliyopita, kwani kuna Sh500 milioni zimekuwa hazina mtiririko unaoeleweka kutoka wizarani kwenda TTB.


Kabla ya kutolewa kwa agizo hilo, wajumbe wa kamati ya POAC wakiongozwa na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola walihoji sababu za TTB kupata fedha kutoka wizarani kwa ajili ya kushiriki maonyesho ya Sabasaba na Nanenane, wakati mfumo wa serikali hauruhusu hilo.


Lugola alimbana Mwenyekiti wa Bodi ya TTB, Balozi Charles Sanga akitaka atoe ufafanuzi kuhusu fedha hizo zinazoingizwa kutoka wizarani kwenda TTB, kwani inaonyesha huwa zinakwenda kinyume na utaratibu.


“Fedha zinazofichwa TTB kutoka wizarani ni za nini, kwa nini Serikali inahamisha fedha na kuingiza kwenu kinyume na utaratibu?” alihoji Lugola na kuongeza:
“Unajua kiasi cha Sh500 milioni ni nyingi sana.”


Aliendelea kutaka ufafanuzi zaidi akitaka TTB ieleze kama mfumo unaotumika unaruhusu TTB kupata fedha kutoka serikalini au la.


Akijibu hoja hizo, Balozi Sanga alisema mfumo huo siyo sawa kwani mfumo wa serikali na mashirika ya umma ni tofauti, hivyo kilichotokea ni makosa.


“Wizara ndiyo inaweza kutusaidia ufafanuzi kuhusu hili, lakini nikuhakikishie ni kwamba tunafanya kazi kwa karibu na wizara,” alisema Balozi Sanga.


Alisema hawezi kutoa jibu la wizara kupeleka fedha TTB, kwa sababu hana majibu.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Utalii kutoka wizarani, Ibrahim Mussa alikiri kuna fedha zimekuwa zikipelekwa TTB kwa ajili ya maonyesho hayo, ila kosa ni kwamba sekretarieti ya maandalizi huwa iko wizarani, hivyo kusababisha kuwa na kasoro za hapa na pale.


“Mwaka ujao tutazirekebisha kasoro hizo na kuhamishia shughuli zote TTB, kuna upungufu huo mwenyekiti nakiri,” alisema Mussa.


Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe licha ya masuala hayo, alihoji kama TTB ina mkataba na wizara wa kuwa wakala wao katika maandalizi ya Sabasaba na Nanenane, wakati TTB ikijua ina uwezo wa kutangaza utalii yenyewe.


Mkurugenzi wa TTB, Dk Aloyce Nzuki alisema huwa wanapewa maelezo kutoka wizarani kufanya kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment