Mabasi ya kasi Dar kuajiri 80,000
BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia (WB),
imeidhinisha Dola za Marekani 100 milioni kwa ajili ya Mradi wa Mabasi
yaendayo Kasi (BRT) jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya benki hiyo iliyopatikana Dar es
Salaam jana imeeleza kuwa mradi huo utakaozalisha ajira 80,000 kwa
Watanzania, utasaidia abiria 300,000.
“Ajira hizo 80,000 zitapatikana hadi mwaka
2015 na zitatokana na kazi zinazotarajiwa kuwapo, ikiwa ni pamoja na
ujenzi wa barabara, vituo vya abiria, vituo vidogo na vituo vya kuratibu
barabara hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Philippe
Dongier alisema kiasi hicho cha fedha kimelenga kukamilisha awamu ya
pili ya mradi huo.
Dongier ambaye pia ni msimamizi wa Benki ya
Dunia kwa nchi za Uganda na Burundi, alisema mradi huo utagharimu jumla
ya Dola za Marekani 290 milioni.
“Dar es Salaam inakuwa kwa kasi, msongamano wa
magari ni tatizo kwa ukuaji wa uchumi kwa sababu unapunguza uzalishaji
kwa kupoteza muda wa watumiaji wa barabara. Hali hiyo inatishia ukuaji
wa baadaye wa mji na nchi kwa jumla na unaongeza uharibifu wa
mazingira,” ilisema taarifa ya WB na kuongeza:
“Mfumo wa BRT utasimamiwa kwa ushirikiano kati
ya Serikali na sekta binafsi kwa Dola za Marekani 40.9 milioni
ukihusisha wasimamizi binafsi wawili wa mabasi na mkusanya nauli mmoja.
Mfumo huo mpya utatekelezwa kwa mabasi yapatayo 148 yatakayokuwa na
uwezo wa kubeba abiria 140 kila moja kwa safari za haraka na za kawaida.
“Mabasi mengine 100 yenye uwezo wa kubeba
abiria 60 kila moja yatatembea katika barabara ndogo. Kutakuwa na
kilometa 20.9 zitakazokuwa na njia za waendesha baiskeli na wapita kwa
miguu kila upande na vituo vya mabasi kwa kila umbali wa wastani wa mita
500.”
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka
alisema hana taarifa za benki hiyo kuidhinisha fedha hizo, lakini
akasema atafuatilia ili kujua idadi ya ajira, hasa zitakazowanufaisha
wazawa.
“Kwa kweli hizo taarifa ndiyo kwanza nazisikia
kwako, labda unipe muda nizifuatilie ili nije na majibu ya uhakika.
Lakini kama kawaida, ajira za kampuni kama hizo huwa na wataalamu wa nje
na wa ndani, kwa hiyo tutahakikisha kuwa sheria zinalindwa,” alisema
Kabaka.
Mtaalamu wa usafiri katika Benki ya Dunia,
Yonas Mchomvu alisema: “Tunafurahishwa na kasi ya utekelezwaji wa mradi
wa mabasi yaendayo kasi, hasa kwa kuwa makandarasi wote wanaotakiwa
wameshapewa fedha na ujenzi unaendelea,” alisema Mchomvu.
Daladala wachekelea
Licha
ya taarifa hiyo kueleza kuwa mradi huo utasababisha kuondolewa kwenye
mzunguko daladala 1,800, bado wamiliki wa magari hayo wamepokea mradi
huo kwa furaha.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam
(Darcoboa), Sabri Mabrouk alisema hiyo ni fursa kubwa kwao ambayo hawako
tayari kuikosa.
“Siyo kwamba mradi huo utatuathiri na siyo
daladala 1,800 tu zitakazoondolewa, ni daladala 3,000. Sisi ndiyo
walengwa wa mafanikio hayo kwani hayo mabasi yanayokwenda haraka
tutamilikishwa. Hapa ndipo tunahimizana kujiunga ili tujue tutayamiliki
vipi,” alisema Mabrouk.
Mabrouk alisema daladala zitakazoondolewa kwenye mzunguko
zitahamishiwa kwenye barabara nyingine, hivyo akaitaka Sumatra
kutosajili daladala nyingine wakati mradi huo utakapoanza kazi.
“Mradi huu siyo kwamba utaishia Barabara ya
Morogoro tu, utakwenda pia Barabara ya Kilwa na baadaye Barabara ya
Nyerere na nyinginezo. Mwenzako akinyolewa wewe nywele zako tia maji.
Kwa hiyo kila mmiliki wa daladala atafaidika, cha msingi tujiweke tayari
kwani tukiipoteza nafasi hii itachukuliwa na watu wengine,” alisema
Mabrouk.
Mkandarasi wa mradi
Meneja wa mradi huo
kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Strabag ya Ujerumani inayojenga barabara
hiyo, Frank Rohde alisema mradi umegawanyika katika vipindi tofauti.
Alisema
awamu ya kwanza itakuwa ni maendeleo ya barabara kutoka Magomeni hadi
Kimara ambayo itajengwa vituo 15 vya mabasi... “Katika awamu hii, vituo
vikuu viwili vitajengwa ambavyo ni Kimara na Ubungo.”
Anasema awamu ya pili itajumuisha uboreshaji
wa barabara kutoka Magomeni, Kivukoni, Barabara ya Kawawa kutoka
Magomeni hadi Morocco na Barabara ya Msimbazi kutoka eneo la Faya hadi
Kamata kupitia Kariakoo.
“Katika maeneo hayo yote, kutajengwa vituo 14 vya mabasi hadi Kituo cha Morocco,” alisema.
Rohde alisema ujenzi wa barabara za mabasi
hayo utajumuisha barabara za mabasi ya kawaida ya umma na zitapanuliwa
ili kuwekwa njia mbili zaidi kwa waenda kwa miguu na waendesha baiskeli.
“Vituo vitajengwa katikati ya barabara hizo (za mabasi ya kasi) katika kila mita 500-700 na vituo vikuu ni vitano,” alisema.
Mradi huo umefadhiliwa na Benki ya Dunia,
mwajiri mkuu akiwa ni Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), washauri
wa ujenzi ni Kampuni ya SMEC kutoka Australia.
Kutakuwa na huduma za
haraka safari za kutoka Kimara Mwisho hadi Posta Mpya zitakazochukua
dakika 25 na kwa huduma za kawaida safari zitachukua dakika 30 hadi 40.
Shughuli nyingine zitakazofanywa katika mradi
huo ni pamoja na kutengeneza mabomba ya maji ya kunywa, kuimarisha
mitandao ya simu, taa za barabarani na za kuongozea magari.
Mradi huo
ulioanza Februari, 2012 utachukua miaka mitatu kukamilika. Kilomita 17
za awali zinatarajiwa kumalizika katika kipindi cha miaka miwili.
Kuhusu ajira, Ofisa Habari wa SMEC, Amina Juma
alisema Strabag na SMEC walitafuta vijana wenye taaluma kwa ajili ya
kufanya kazi katika mradi huo, akisema kampuni yake ilihakikisha kuwa
wanaopata ajira zaidi ni wazawa ambao wanaielewa nchi yao.
No comments:
Post a Comment