Mramba: Mkapa aliniruhusu kusamehe kodi

Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam imeambiwa na Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba (74), kwamba alitoa msamaha wa kodi kwa kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation kabla ya kuliwasilisha suala hilo katika Baraza la Mawaziri.

Kadhalika, Mramba alidai katika kesi hiyo inayomkabili kama mshitakiwa wa kwanza wa kuisababishia hasara serikali ya Sh. bilioni 11.7 kuwa alipokea maagizo kutoka kwa Rais (wakati huo Benjamin Mkapa) kwa njia ya mdomo ya kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo. 

Mramba alitoa madai hayo jana wakati akihojiwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Osward Tibabyekomya, mbele ya jopo la 

mahakimu watatu linalowajumuisha Mwenyekiti John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela wanaosikiliza kesi hiyo.

Mshtakiwa huyo na wenzake wawili wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka, kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Tibabyekomya na Mramba:

Wakili: Juni 12, mwaka 2003 ulipoagiza Gavana aainishe mkataba, uchunguzi wa kujua nchi jirani zinafanyaje kazi na kampuni za ukaguzi za madini ulikuwa umefanyika?

Mramba: Ndiyo.

Wakili: Uchunguzi ulifanyika lini na nchi gani waliangalia?

Mramba: Sikumbuki.

Wakili huyo aliomba mahakama kumruhusu mshtakiwa kusoma barua ambayo ni kilelezo katika kesi hiyo iliyoonyesha kwamba kulikuwa na majadiliano kati ya Wizara ya Fedha, Mwanasheria Mkuu (AG), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Wizara ya Nishati na Madini.

Wakili: Je, mlijadiliana nao kama barua ilivyosema?

Mramba: Sijawahi kufanya majadiliano yoyote.

Wakili: Kwa mujibu wa maandishi ya barua hiyo inaonyesha kuwapo kwa majadiliano kweli au siyo kweli?

Mramba: Ndiyo, kwa mujibu wa maandishi kunaonyesha kuwapo kwa majadiliano kati ya Wizara ya Fedha, Nishati na Madini, BoT na AG.

Wakili: Rais alitoa maelekezo ya kushughulikia kampuni hiyo?  

Mramba: Ndiyo.

Wakili: Wakati unatoa maelekezo kwa Gavana, ulijua uwapo wa barua ya Mei 13, mwaka 2003 kutoka kwa Katibu wa Rais na Waziri wa Nishati na Madini?

Mramba: Hapana.

Mramba alionyeshwa barua ya Mei 21, mwaka 2003 kutoka kwa Gavana (wakati huo marehemu Daudi Balali) kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha.

Wakili: Kwa mujibu wa barua hiyo, Wizara ya Fedha ilikuwa inaombwa kumteua mjumbe atakayeshiriki kwenye majadiliano ya mkataba wa uteuzi wa mkaguzi wa madini. Je, ni kweli?

Mramba: Ndiyo kama barua inavyosema.

Wakili: Taratibu za kutafuta malipo zilianza hata kabla ya majadiliano ya mkataba huo?

Mramba: Ndiyo taratibu zilishaanza.

Wakili: Je, ulipeleka lini nakala ya mkataba kwenye Baraza la Mawaziri?

Mramba: Februari mwaka 2004.

Wakili: Je, shahidi utakubaliana na upande wa Jamhuri katika kesi hii wakati unatoa msamaha wa kodi ulikuwa haujaliarifu baraza?

Mramba: Ndiyo

Wakili: Rais (Mkapa) alitoa kwa njia gani suala la kuilipa fedha kampuni hiyo ya ukaguzi?

Mramba: Kwa njia ya mdomo.

Kesi hiyo itaendelea kusikiliza mahojiano kati ya upande wa Jamhuri na Mramba Aprili 9 hadi 12, mwaka huu.  Katika kesi ya msingi, washitakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri na katibu mkuu walitumia vibaya madaraka.

Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa ukaguzi wa madini kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart 

( ASSAYERS) Government Business Corporation waliingia mkataba kukagua kiwango cha uzalishaji wa madini ya dhahabu kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Washitakiwa wengine ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Hazina, Gray Mgonja.

No comments:

Post a Comment