Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
Zaidi ya wanafunzi 72 wa Shule ya Sekondari ya
Edmund Rice, inayomilikiwa na Kanisa Katoliki la Jimbo Kuu la Arusha,
wamenusurika kuteketea kwa moto huku wengine 70 vifaa vyao vyote
vikiteketea baada ya mabweli yao kuungua juzi usiku.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo iliyopo maeneo ya
Engusheratoni, Kata ya Sokoni 1, Francis Nkwabi, mabweni yaliyoshika
moto ni ya wanafunzi wa kidato cha tano.
Alisema chanzo cha moto huo ulioanza saa 1:15 usiku na kufanikiwa kuzimwa saa 4, bado hakijafahamika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema kuwa
polisi kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na
Kikosi cha Zimamoto, wameanza uchunguzi ili kubaini chanzo.
Aidha, Nkwabi alisema wanafunzi 20 walipatwa na mshtuko na kuzimia
na walikimbizwa hadi hospitali ya Mtakatifu Elizabeth, maarufu kama kwa
Father Babu kwa matibabu na wengine waliwekewa hewa ya oksijeni.
Wanafunzi watatu kati yao bado wanaendelea kupatiwa matibabu.
Walisema mali na vifaa vyote vya watoto hao vimetetekea kwa moto na watoto 70 hawana kitu kabisa.
Alisema baada ya kuzuka kwa moto huo waliwasiliana na Kikosi cha
Zimamoto ambao walifika eneo la tukio baada ya dakika 10, na kwa pamoja
na wananchi wa jirani walisaidiana kuuzima moto huo.
Nkwabi alisema jana alipokea mamia ya wazazi waliofika shuleni hapo
baada ya kusikia kuwapo kwa moto huo na taarifa kwamba wanafunzi 20
walikuwa wamekufa wakati haikuwa kweli.
No comments:
Post a Comment