Wanawake wanaotumia njia za kisasa uzazi wa mpango waongezeka
Idadi wanawake wanaotumia njia za kisasa za muda
mrefu za uzazi wa mpango, zinazotolewa na Shirika la PSI imeongezeka
mara mbili kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Akizungumza na Wahariri na Waandishi waandamizi kutoka vyombo vya
habari nchini, Mkurugenzi wa Programu ya Afya ya Uzazi ya PSI Tanzania,
Dk. Nguke Mwakatundu, alisema ongezeko hilo ni zaidi ya asilimia 100
katika kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema kipindi cha mwaka jana, jumla ya wanawake waliopatiwa huduma
hiyo ilikuwa 102,778 wakati mwaka 2011 waliopatiwa huduma ya uzazi wa
mpango walikuwa 48,518.
Dk. Mwakatundu alisema kwa upande wa programu yao ni mafanikio ya
kujivunia ingawa wangependa kuona idadi hiyo inaongezeka zaidi mwaka
huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Romanus Mtung’e, alisema
wamejipanga kuhakikisha wanawake nchini wanapatiwa huduma bora na za
kisasa za uzazi wa mpango.
Alisema ni kipindi mwafaka kwa wananchi kutambua umuhimu wa kupanga
familia zao ili watoto wanaozaliwa wapate malezi mazuri na huduma bora
toka kwa wazazi, jamii na serikali.
No comments:
Post a Comment