Mali za mfanyabiashara aliyekamatwa kwa tuhuma za ujambazi zakamatwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman
Sakata la Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kunasa
watuhumiwa wa mtandao wa majambazi jana lilisababisha kundi la wakazi wa
Jiji la Mbeya kujikusanya eneo Mwanjelwa katika maeneo ya maduka ya
nguo, ili kumwona mfanyabiashara maarufu wa eneo hilo, Ghati Mbilinyi
(32), aliyekamatwa na Polisi akihusishwa na mtandao huo.
Umati huo ulijitokeza baada ya Polisi kuongozana na mfanyabiashara
huyo kwenda dukani kwake kwa ajili ya kufanya upekuzi na kuchukua baadhi
ya mali zinazodaiwa kuwa ni za wizi kama kielelezo wakati
atakapofikishwa mahakamani.
Mbilinyi akiwa chini ya ulinzi mkali, aliamuliwa kukusanya bidhaa
karibu zote zilizokuwa ndani ya duka lake na kuzipakia katika gari la
Polisi kisha kuondoka nazo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alisema kuwa
walilazimika kwenda dukani kwa mtuhumiwa huyo na kuchukua mali zake
kutokana na maelezo yake baada ya kukiri kuwa anajihusisha na matukio ya
kupora mali na kufanya mauaji.
“Ni kweli kwamba tumelazimika kwenda na mtuhumiwa mwenyewe hadi
dukani kwake na kuchukua mali alizokuwa nazo, tumefanya hivyo kutokana
na mazingira yanayoonekana kuwa alikuwa anajihusisha na matukio ya
ujambazi ya uporaji, utekaji, na mauaji,” alisema Kamanda Diwani.
Hata hivyo alisema kuwa Jeshi la Polisi halisemi moja kwa moja kuwa
mali zote alizokuwa nazo ndani ya duka zilitokana na uporaji, lakini
mtuhumiwa mwenyewe alitaja baadhi ya mali alizozipata kwa kufanya
uhalifu.
Akizungumzia hatma ya watuhumiwa 13 wanaoshikiliwa na Polisi kwa
kujihusisha na mtandao huo, Diwani alisema tayari watuhumiwa saba
wamesafirishwa kwenda mkoani Iringa ambako ndiko watashtakiwa kwa tuhuma
za kuteka na hatimaye kuwaua wamiliki wa gari lililokuwa likisafirisha
mali za wafanyabiashara wa Mbeya.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kukamilisha taratibu za
kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wengine sita waliobakia mkoani hapa.
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya juzi lilitangaza kunasa mtandao
watuhumiwa wa ujambazi uliokuwa ukifanya uhalifu katika mikoa ya Mbeya,
Iringa, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, ambao uliwahusisha askari
mmoja wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mmoja wa Kikosi Kutuliza Ghasia
(FFU) mkoani Mbeya.
No comments:
Post a Comment