Watengeneza matofali katika Jiji la Dar es
Salaam, wamezilalamikia Kampuni za saruji nchini kwa madai kwamba mifuko
ya kilo 50 mara nyingi inakuwa na uzito pungufu tofauti na uliotajwa
kwenye mfuko.
Kauli hiyo ilitolewa kwenye mafunzo ya uhifadhi
wa mazingira kwa watengenezaji wa matofali iliyofanyika kwenye Kiwanda
cha Saruji cha Twiga (TPCC) yakiwashirikisha watu 50.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Mohamed Mkumbo
akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema mifuko mingi ya saruji
inawafikia ikiwa na uzito pungufu na kutoa mwito kwa kampuni hizo
kurekebisha kasoro zinazojitokeza. Akijibu hoja hizo, Meneja Mazingira
wa TPCC, Richard Magoda alisema mifuko yote inatoka kiwandani ikiwa na
kilo 50.
Magoda alisema wanaopunguza uzito ni
wasafirishaji wakiwamo madereva na wasaidizi wao ama mawakala wakiwa
njiani kuelekea kwa wateja waliohitaji. Alisema vitendo hivyo vinapingwa
na kampuni za saruji, lakini wezi hao wanafanya kwa kula njama na
madereva ama wauzaji wa jumla ili kuwaibia wateja wa mwisho.
“Kuna wizi unafanywa kwani mifuko yote ya saruji
hujazwa katika uzito stahiki wa kilo 50 hadi inapopakiwa kwenye magari
ya wasafirishaji, lakini wao wanapokuwa njiani hufanya ujanja ambao
wanauoita ‘kupiga bomba’ kwa lengo la kupata faida zaidi” alisema.
Magoda alisema tayari kuna mawakala wa usafirishaji kadhaa tumekwisha
vunja mikataba nao baada ya kugundulika kuwa wafanyakazi wa magari yao
hufanya uchakachuaji huo maarufu kama kupiga bomba.
No comments:
Post a Comment