Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai, Yasinta Assey akionyesha
baadhi ya nguo na viatu vya wanafunzi vilivyokutwa katika eneo
linalodaiwa kuwa danguro linalotumiwa na wanafunzi wa shule hiyo, jana.
Dar es Salaam. Baadhi ya
wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Majani ya Chai iliyopo Kipawa
jijini Dar es Salaam, wametajwa kujiingiza katika kashfa ya ngono,
kuvuta na kuuza bangi katika moja ya nyumba zinazozunguka shule hiyo.
Hilo ni tukio lingine jipya, kwani mwishoni mwa
mwaka jana, kuliibuka matukio ya ajabu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi,
Ruaruke, Rufiji mkoani Pwani ambao walielezwa kujihusisha na uvutaji
bangi hata kukonyeza na kubaka walimu wao.
Mkuu wa Sekondari hiyo, Jasinta Assey alikiri na
kusema kwamba vitendo vya uvutaji bangi na biashara ya ukahaba kwa
wanafunzi wake, vinachangiwa na askari wa Kituo kidogo cha Stakishari
ambao alidai wanachukua rushwa kwa wauzaji wa bangi na nyumba bubu za
wageni. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Shule hiyo,
Jasinta Assey alisema ni kawaida ya polisi hao kwenda kwenye nyumba hizo
kunakofanyika biashara hizo na kuchukua rushwa badala ya kutatua
tatizo.
Alisema ongezeko la utoro katika shule hiyo ni
tatizo kubwa na wanafunzi wa kidato cha nne wanaosoma masomo ya sanaa
ndiyo wanaoongoza kwa kuvuta bangi na kwenda kufanya ngono katika nyumba
zilizo jirani na eneo la shule hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema hajapata taarifa za hali hiyo.
“Ngoja
nimtume Mkuu wa Kituo cha Polisi Stakishari afuatilie kwa karibu,”
alisema Minangi na kuongeza: “Lakini ngoja nikwambie, hili suala
nakumbuka liliwahi kuripotiwa 2011 wakati nikiwa mkuu wa kituo hicho;
nililishughulikia na tulibaini kuwa hakuna mwanafunzi ambaye alikuwa
anaenda kwenye nyumba hizo kuvuta bangi wala kufanya ngono.
“Kilichotokea kwa wakati huo ni kwamba,
tuliwachukua baadhi ya wanafunzi ili watupeleke mahali walipokuwa
wakifanyia vitendo hivyo kutokana na maelezo na vielelezo vyao, lakini
hatukubaini hizo sehemu.
“Inawezekana basi haya mambo yameibuka upya baada ya kuona kuna mkuu wa kituo mwingine mpya,” alisema Kamanda Minangi.
Kutokana na matendo hayo, wanafunzi wengi walifanya vibaya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka jana.
“Walifeli sana mwaka jana hawa, walimu wapo,
tunawapa nyenzo lakini hawataki, ninaiomba Serikali kuingilia kati suala
hili kwani ni la muda mrefu na ni faida ya vijana hawa,” alisema.
Shule ya Majani ya Chai ilishika nafasi ya 61
kimkoa kati ya shule 226 wakati ngazi ya taifa, ilishika nafasi ya 543
kati ya shule 3,392.
Wanafunzi 274 walijisajili kufanya mtihani wa
kidato cha nne mwaka jana na kati yao 130 walipata sifuri, wakati
waliopata daraja la nne ni 85, waliopata Daraja la Tatu ni 18 wakati
waliopata daraja la pili ni watano. Hakukuwa na daraja la kwanza na
wanafunzi 36 hawakufanya mtihani.
“Baada ya kuona utoro umekithiri shuleni hapo,
nilikwenda kutoa taarifa kituo kidogo cha Polisi Stakishari, lakini
hawakuonyesha ushirikiano matokeo yake wanakwenda kwa wenyeji hao na
kuchukua rushwa.
“Hili inaonekana kama ni dili la hawa askari,
kwani wapo walionifuata na kunieleza niache kufuatilia, lakini mimi
niliwaambia nitafuatilia tu na ilifikia hatua nikatishiwa maisha.
“Baada
ya kuona nazidi kutishiwa maisha, niliogopa, nikaacha...na hivi
ninavyoongea na wewe, najua tu watanifuata kwani nimeshaambiwa nikipita
peke yangu eneo wanakofanyia biashara zao watanifanyia kitu kibaya,”
alisema Assey.
Mwalimu huyo alisema kwamba, wanafunzi wa kidato cha nne
wanaosoma masomo ya sanaa wapo 54, lakini wakati mwingine utakuta
wanafunzi watano tu darasani na waliobakia wanakwenda kuvuta bangi na
kufanya vitendo vya ngono.
Assey alisema kuwa iliwahi kutokea wasamaria
wema waliwapelekea baadhi ya nguo na viatu vya wanafunzi wa shule hiyo
vilivyokutwa eneo wanakofanya biashara hiyo ya haramu.
“Hili darasa linaongoza kwa utovu wa nidhamu
na limeshindikana...Nilikuwa nawategemea sana polisi, lakini hawaonyeshi
ushirikiano wowote ule...Unaona hizi nguo za wanafunzi zililetwa na
mama mmoja baada ya kuzikuta kwenye danguro ‘bubu’,” alisema Assey huku
akionyesha sare hizo za shule.
No comments:
Post a Comment