MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim
Seif Sharif Hamad amepinga kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel
Nchimbi kuwa mauaji ya viongozi wa dini Zanzibar ni ugaidi na kusema
kuwa wanaofanya hivyo ni watu wenye nia ya kuvunja umoja wa Wazanzibari.
Baada ya mauaji ya Padre Evarist Mushi,
akizungumza na wandishi wa habari,Nchimbi alielezea kusikitishwa na
mauaji hayo akisema kuwa ni ya kigaidi na yana lengo la kuingiza nchi
katika machafuko. Amesema kuwa tukio hilo si tukio la ujambazi bali
tukio la kigaidi kwani limelenga zaidi katika kuwashambulia viongozi
kidini.
Padre Evaristus Mushi aliuawa Februari 17,
mwaka huu kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa katika
pikipiki aina ya Vespa wakati akienda kuongoza misa katika Kanisa la
Mtakatifu Theresia la Beit el Rass.
“Watu hawa wameamua kuyatumia matukio ya kuuawa na
kujeruhiwa kwa viongozi wa kidini ili kuvunja umoja wa Wazanzibari,
lakini nasema hakuna ugaidi Zanzibar,” alisema Maalim Seif juzi usiku
alipohutubia kwenye hafla ya Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad
(S.A.W) mjini Kiuyu, Wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba.
Alisema hivi sasa Wazanzibari ni wamoja na watu
hao wenye nia mbaya wanayachukulia matukio hayo kwa kutaka kuwagawa na
kuwaletea mtafaruku kwa kuonyesha kuwa kuna tofauti za kidini Zanzibar
wakati siyo kweli.
Alisema inasikitisha kuona wapo baadhi ya viongozi
wenye nia chafu dhidi ya Zanzibar wenye tabia ya kutoa kauli za kujenga
chuki na fitina miongoni mwa Wazanzibari chini ya kivuli cha matukio
hayo.
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais alisema,
kinachoonekana kuna ajenda imetayarishwa ya kutaka kulazimisha chuki za
kidini Zanzibar, licha ya kuwapo kwa historia ya miaka mingi ya watu
kuvumiliana na kuishi kwa pamoja na kuwapo watu wa imani tafauti.
Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar hivi sasa kuwa
macho na ajenda zinazolengwa kuwavuruga na waendelee kuishi kwa
mshikamano na umoja kama ambavyo wamekuwa wakiishi.
Maalim Seif alisema vitendo vya kuuawa na
kujeruhiwa viongozi wa kidini Zanzibar ni mambo mageni na kwa miaka
mingi Zanzibar imekuwa ni mfano bora wa uvumilivu wa kiitikadi za
kidini, licha ya kuwa asilimia 98 ya wananchi wake ni Waislamu.
Alisema Katiba ya Zanzibar imeweka wazi haki ya mtu kuabudu kwa mujibu wa imani yake na uhuru wa mtu kuabudu umelindwa.
“Ni Sultani wa Zanzibar ambaye alikuwa Muislamu
ndiye aliyetoa ardhi kwa Wakiristo kujenga Kanisa. Juzi nilipokwenda
kutoa salamu za rambirambi kwa Baba Askofu Shayo, baada ya kifo cha
Padri Mushi, aliweka bayana kuwa lililotokea lisihusishwe na tofauti za
kidini,” alisema Maalim Seif.
Hata hivyo, Maalim Seif alisema inasikitisha kuona
wakati Rais Jakaya Kikwete katoa maelekezo uchunguzi wa kina ufanyike
na Kamishna wa Polisi Zanzibar ameshaweka wazi kuwa uchunguzi
unaendelea, baadhi ya viongozi na vyombo vya habari vinachochea chuki za
kidini na kusema kuwa Zanzibar kuna ugaidi.
Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar kwa wakati huu kuwa watulivu
na wasitawaliwe na jazba na wala wasichokozane, pia wasikubali
kuchokozeka.
Akizungumzia matokeo ya mtihani wa kidato cha nne
yaliyotolewa hivi karibuni, Makamu wa wa Kwanza wa Rais alisema ni
matokeo mabaya na ya kuliza, kwa sababu hayaonyeshi mustakabali mwema
kwa watoto wetu na nchi yetu hapo baadaye.
Alisema ni wakati mwafaka Serikali, Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, walimu na jamii nzima kujiuliza nini sababu
ya matokeo hayo mabaya, na kujiuliza pia nchi inaelekea wapi?
Maalim Seif alisema sasa si wakati tena wa
kutupiana lawama, lazima pande zote zikae zijadili wapi pamekosewa, ili
ufumbuzi uweze kupatikana na hali kama hiyo isitokee tena siku zijazo.
No comments:
Post a Comment