Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Duwani Nyanda akizungumza
na viongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Misheni Mashariki ambapo
polisi walizuia ibada kufanyika jana katika Kanisa la Moravian Ushirika
wa Tabata jijini Dar es Salaam kwa madai kuwa ingehatarisha amani kwa
waumini hao. Picha na Pamela Chilongola
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi Dar es Salaam,
imetupilia mbali ombi la Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Moravian Jimbo
la Kusini, la kutaka kufunguliwa makufuli yaliyofungwa katika Kanisa la
Usharika wa Tabata, ili waweze kumsimika mchungaji mpya, ambaye ni Lawi
Mwankuga.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Mathew
Mwaimu,baada ya bodi hiyo ya wadhami wa Kanisa la Moravian Kusini chini
ya Mchungaji Clement Mwaitebele, kupitia wakili wao, Henry Chaula wa
Kampuni ya Uwakili ya C&M, kufungua kesi namba 12 ya mwaka 2013 na
kuomba isikilizwe chini ya hati ya dharura.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, Mchungaji Gervas
Mwakafwila, Mchungaji Silas Mwakibinga, Tukuswiga Mwakabur, Atuganile
Mbombo, Isakwisa Ernest na Sekela Mukisele ambao wanatetewa na Wakili
Benjamin Mwakaganda wa Kampuni ya uwakili ya BM, wanadaiwa kufunga
makufuli kwenye Kanisa la Usharika wa Tabata, ili kuzuia bodi hiyo
kumsimika mchungaji mpya.
Akitoa uamuzi, Jaji Mwaimu alikataa ombi la bodi
hiyo ya wadhamini la kutaka kufunguliwa kwa makufuli yaliyokuwa
yamefungwa kwenye kanisa hilo, ili kupisha kumsimika mchungaji mpya.
Pia
jaji huyo aliruhusu shughuli za kawaida za kanisani hapo kuendelea na
kusisitiza kwamba kilichozuiwa ni usimikaji wa mchungaji ili kuondoa
uvunjifu wa amani.
Baada ya kutoa uamuzi huo, Jaji Mwaimu aliwataka
wadaiwa kupeleka kiapo pinzani mnamo au kabla ya Februari 5, mwaka huu
ambapo kesi hiyo imepangwa kusikilizwa.
Bodi hiyo ya wadhamini wa Kanisa la Moravian Jimbo
la Rungwe ni wadaiwa namba 4 katika kesi namba 222 iliyofunguliwa
mwaka 2012 katika Mahakama Kuu, ambayo inaendelea kusikilizwa Februari
6, mwaka huu mbele ya Jaji Augustini Mwarija.
Katika kesi hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Jimbo la Mashariki na Pwani ya Kanisa la Moravian Tanzania, Clement
Fumbo na wenzake saba wanapinga kuondolewa madarakani na kusimamishwa
kazi.
Katika kesi hiyo, Fumbo na wenzake hao saba wanaiomba Mahakama iamuru walipwe Sh500 milioni kama fidia na gharama ya kesi.
No comments:
Post a Comment