POLISI wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, limewanasa
watu wanne akiwamo mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana,
wilayani Bunda, mkoani Mara, baada ya kukutwa wakiiba fedha Benki ya NMB
tawi la Tukuyu kupitia mashine za kutolea fedha (ATM).
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispin Meela alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku.
Meela
aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni mkazi wa mjini Tukuyu, Mfanyabishara
wa Mbozi, mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana wilayani
Bunda na mkazi wa Msasani Tukuyu.
Alisema akiwa nyumbani kwake usiku, alipigiwa simu
na msamaria mwema na kuambiwa taarifa za kuwapo watu wakiwa kwenye
mashine hizo za kutolea fedha, huku wakiwa wanatoa fedha mfululizo na
aliwatilia shaka.
“Jana usiku saa 2:30 nilipigiwa simu na msamaria
mwema na kuniambia kuwa, kuna watu wapo Benki ya NMB wanatoa fedha ATM
tena mfululilo huko wakiwa na kadi nyingi za ATM,” alisema Meela na
kuongeza:“Baada ya kuambiwa hivyo nilimpigia simu OCD (Mkuu wa polisi
wilaya), akatuma timu ya makachero eneo ta tukio na wakabahatika
kuwakuta na kuwatia nguvuni.”
Meela alisema watuhumiwa walikutwa wakiwa na kadi
bandia za ATM 150 za watu tofautitofauti na kwamba, hadi wanatiwa
mbaroni tayari walikuwa na Sh20.5 milioni mkononi. Alisema kadi zote ni
za NMB na kwamba, zilikuwa zinaonyesha wateja wote ni walimu kutoka
wilayani Mbozi.
Alisema baada ya watuhumiwa kuhojiwa walidai ni
wafanyabiashara wanajihusisha na kukopesha fedha walimu, hivyo katika
kuzirejea fedha hizo walimu waliwapatia kadi zao ili waende kutoa
benki.
“Kinachotupa hofu hapa ni kwamba, kadi zote hizi
zinaonyesha wateja kutoka wilayani Mbozi, sasa swali kwa nini waje
kutolea fedha hizo wilayani kwetu?” alihoji Meela.
Alisema watuhumiwa wote wapo Kituo cha Polisi Tukuyu kwa mahojiano zaidi.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alikiri kupata taarifa hizo,
lakini alikataa kulitolea ufafanuzi kwa sababu wanaendelea na
uchunguzi.
No comments:
Post a Comment