Kada wa Chadema Mkoani Dodoma, Arnold Swai akikimbizwa na wafuasi wa CCM
jana, baada ya kutokea vurugu katika eneo la Mwanga baa, Dodoma
SHEREHE za miaka 36 za kuzaliwa kwa CCM jana
ziliingia dosari, baada ya kuibuka vurugu kubwa kati ya wafuasi wa chama
hicho na Chadema mkoani Dodoma wakati wakigombea eneo na mti wa
kutundika bendera za vyama vyao.
Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza
Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na
Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo
uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa
sehemu ya maadhimisho hayo.
Vurugu zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema
kuwataka wenzao wa CCM waendelee na mkutano katika eneo hilo kwa sharti
la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa. Wafuasi wa vyama hivyo wakiwamo
wabunge wa CCM walionekana wakivutana kunyang’anyana mti wa bendera.
“Baada ya CCM kugoma, Chadema walijaribu kurudisha
bendera hiyo kwa nguvu, jambo ambalo lilifanya wafuasi wa CCM waanze
kuokota mawe na kuwarushia wapinzani wao hao, huku Chadema nao walianza
kujibu mapigo,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Baadhi ya wabunge wa CCM walioshiriki katika
vurugu hizo na majimbo yao kwenye mabano ni Ismail Aden Rage (Tabora
Mjini), Nyambari Nyangwine (Tarime), Seleman Jafo (Kisarawe), Said
Mtanda (Mchinga) na Mary Chatanda (Viti Maalumu).
Baadhi ya wafuasi wa CCM walionekana wakibeba mawe
na kuwapiga wenzao wa Chadema na kusababisha tafrani kubwa katika eneo
hilo la mkutano.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Jellah
Mambo alisema kuwa tukio hilo limetokana na wafuasi wa CCM kung’oa
bendera ya Chadema iliyokuwa ikipepea eneo la Mwanga Baa kulikofanyika
sherehe za chama chao (CCM).
“Kwanza wamechukua bendera yetu. Halafu
tumeshangazwa na CCM kuruhusiwa kufanya maadhimisho yao wakati kuna
agizo la Mkuu wa Mkoa na polisi kukataza mikusanyiko ya kisiasa wakati
wa Bunge.
“Kwa nini sisi (Chadema) tuzuiwe mikutano yetu
wakati wenzetu wanafanya? Huku si kutenda haki....Tulikuwa na mikutano
ya kuimarisha chama katika kata kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili,
lakini tumezuiwa na tukaheshimu mamlaka,” alisema katibu huyo.
Pia tulikuwa tufanye mkutano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, lakini tukazuiwa na tuliheshimu amri hiyo, alisema.
Mambo alisema katika vurugu hizo wafuasi wawili wa Chadema; Idd Kizota na Anord Swai waliumizwa na kushonwa nyuzi saba usoni.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Mpuya alisema hana taarifa za majeruhi hao.
“Ni vigumu kujua, unless (isipokuwa) wafike hospitalini
wakisindikizwa na kundi la wafuasi wenzao waliokuwa kwenye sare. Kama
walikuja kama wagonjwa wengine sio rahisi sana kwangu kujua,” alisema Dk
Mpuya.
Kumi mbaroni
Vurugu hizo zilizosababisha watu wawili kuumizwa
vibaya, zililazimisha Jeshi la Polisi kuwatia mbaroni watu kumi
wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chadema
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alikiri kutokea vurugu hizo, lakini akasema bado anafanyia kazi suala hilo.
Kamanda Misime alikiri Serikali mkoani Dodoma
kuzuia mikutano ya kisiasa wakati wa Bunge, lakini akasema kwa CCM ni
tofauti kwa kuwa hizo ni sherehe zao za kuzaliwa kwa chama.
“Ninasoma hapa magazeti yenu, mmeandika wenyewe
maadhimisho ya miaka 36. Sasa hawa wanaadhimisha hiyo miaka 36 na siyo
mkutano wa kisiasa...Tulichokataza ni maandamano, misafara ya pikipiki
na kufanya mikutano ya siasa,” alisema Misime.
Akihutubia katika mkutano huo baada ya hali
kutulia mgeni rasmi, Mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyangwine aliwakandia
wapinzani na kusema kuwa wanachokifanya ni kuendeleza vurugu nchini na
hawana sera ya maendeleo.
“Hivi jamani, hii leo hawa jamaa watasema nini?
Kama suala la barabara, leo hii unaweza kutoka Mtwara hadi Mwanza kwa
baiskeli, kama maji, michakato inafanyika, kama umeme ndiyo usiseme,
hivi wanataka nini?
“Hawa jamaa wamezoea kufanya vurugu...Si mmeona
wenyewe hapa, hawana lolote zaidi ya kufikiria vuru, wananchi msikubali
kuhadaiwa,”alisema.
JK akemea mifarakano
Akizungumza mkoani Kigoma kulikofanyika
maadhimisho hayo kitaifa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete,
alikemea siasa za makundi ndani ya chama, akisema tabia hiyo haijengi.
“Mifarakano ndani ya chama inayopaliliwa na
viongozi ndani ya chama, inakibomoa chama na ndiyo maana tumepoteza
majimbo matano katika uchaguzi uliopita,” alisema.
Aliendelea:“Ninasoneneka sana kuona viongozi wetu wanajiingiza
katika makundi, tabia hii haijengi, turejee katika maazimio
yaliyopitishwa katika mkutano mkuu uliopita, ambayo yalisisitiza kuwapo
kwa umoja na mshikamano.”
Rais Kikwete alisema angetamani umoja na
mshikamano wa chama hicho ungeendelea kudumu, ili amalize muda wake
akikiacha chama kikiwa imara na kuendelea kushika dola.
“Mimi sasa ninaelekea kwenye ungwe ya mwisho ya
uongozi, nataka nikabidhi kijiti kwa mwana-CCM…Nataka niondoke nikiwa
nimeicha CCM imara “ alisema Rais Kikwete .
Katika hotuba hiyo Rais Kikwete pia aligusia
maendeleo yaliyofikiwa katika kipindi cha utawala wake akitaja maeneo
kama ujenzi wa barabara, madaraja na uimarishaji sekta ya maji kuwa ni
baadhi ya maeneo yaliyopiga hatua.
Alisema atapondoka madarakani jambo kubwa ambalo
angependa Watanzania wakumbukuke kwalo ni kuitwa bwana maendeleo na
hivyo sasa anaendelea kuisimamia vyema ilani ya chama chake ili
kuendelea kukamilisha miradi iliyobaki.
Mapema Rais Kikwete aliongoza mamia ya wakazi wa
Mji wa Kigoma katika matembezi ya mshikamano ikiwa ni ishara ya kuhimiza
umoja na mshikamano kwa Watanzania.
Kikwete aliungana na viongozi wenzake Makamu
Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho
Abdulrahman Kinana, lakini katika hali isiyo ya kawaida baadhi ya
viongozi wa chama hicho hawakushiriki, akiwemo wenyeviti wastaafu,
Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi.
Wengine ambao hawakuwepo katika matembezi hayo ni
pamoja na makatibu wakuu wa zamani; Yusuph Makamba na Willison Mukama na
wajumbe wote wa sekretarieti ya chama hicho iliyoteuliwa Novemba mwaka
jana.
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na viongozi wa
vyama vya siasa vya PPRD cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na
kile cha CNDD-FDD ambavyo vilisindikizwa na vikundi vya sanaa kutoka
katika nchi hizo jirani.
No comments:
Post a Comment