Rais Jakaya Kikwete
Dar es Salaam. Ni nadra kutokea lakini wafuasi
wa vyama vya siasa vya CCM na Chadema, wameungana kumweleza Rais Jakaya
Kikwete kuhusu kero ya maji eneo la Kimara-Golani, Dar es Salaam.
Rais Kikwete alikutana na hali hiyo wakati
akifungua Daraja la Kimara jana, tukio hilo liliwakusanya watu wengi
hasa wanachama wa CCM na Chadema waliokuwa wamevalia sare za vyama vyao.
Wafuasi wa Chadema waliongozwa na Mbunge wa
Ubungo, John Mnyika ambao walikuwa wakipeperusha bendera za chama chao
na kuimba nyimbo mbalimbali huku wakidai maji. Hata hivyo, kutokana na
hali hiyo, wafuasi wa CCM waliungana na wenzao wa Chadema, kupiga kelele
juu ya suala hilo kiasi cha kugusa hisia za Rais Kikwete.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa daraja hilo,
Rais Kikwete aliahidi kuitisha kikao Jumatatu ijayo kitakachomhusisha
Profesa Maghembe na maofisa wa wizara yake, wabunge wa Dar es Salaam,
Mkuu wa Mkoa, wakuu wa wilaya ili kuweka mikatati ya pamoja kutafuta
ufumbuzi wa suala hilo.
“Ninaomba Machi 25... tukutane ili tuweke mikakati ya pamoja kutafuta ufumbuzi wa suala hili,” alisema Rais Kikwete.
Akiwa Hospitali ya Mwananyamala, Rais Kikwete
alizindua maabara ya kisasa kwa ajili ya uchunguzi na akazungumzia suala
la dawa za kulevya kwa kusema atahakikisha mapambano yanaendelea kwani
dawa hizo zinaua nguvu kazi ya taifa ambayo ni vijana.
No comments:
Post a Comment