mwanamke anayedaiwa kufariki miaka mitano iliyopita
Geita: Mji wa Geita na maeneo ya jirani
juzi ulikumbwa na taharuki ya aina yake, pale mwanamke ambaye anadaiwa
kwamba alifariki miaka mitano iliyopita alipoonekana akiwa hai katika
eneo la Kasamwa.
Inadaiwa kwamba Flora Onesmo (45) alifariki
Februari 28, 2008 katika Hospitali ya Wilaya ya Geita na kuzikwa katika
Kijiji cha Nakasenya, Kata ya Butundwe, lakini juzi alfajiri alikutwa
ameketi nje ya nyumba ya dada yake aitwaye Monica James, anayeishi
Kasamwa.
Aliyekuwa wa kwanza kumwona Flora ni mdogo wake
aitwaye Monica Onesmo ambaye baada ya kuamka saa 11:00 alfajiri nyumbani
kwa dada yake, alimwona mwanamke aliyekuwa ameketi nje ya nyumba hiyo,
lakini alimfananisha mwanamama huyo na marehemu dada yake.
“Baada ya kumwona nilimwita mtoto wake tunayekaa
naye na nikampigia simu dada (Monica) ambaye alikuwa amelala chumba
kingine nikamwambia kwamba nimeamka na kumkuta mwanamke amekaa hapa nje,
lakini kila nikimwangalia anafanana na marehemu dada yetu,”alisema
Jubili na kuongeza kwamba alipowaita wote walitoka nje.
Alisema mtoto wa Flora (marehemu anayedaiwa
kufufuka) anaitwa Rebeka Elisha (16) na kwamba walimchukua tangu 2008
wakati mama yake huyo alipofariki dunia katika Hospitali ya Geita ambako
alikuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa ini.
Rebeka ambaye ni mtoto wa nne wa Flora alisema:
“Mama mdogo alituita sisi tulikuwa tumelala akasema kwamba nje kuna
mwanamke ambaye anafanana na marehemu mama yetu, ndipo na sisi tukatoka
na kweli kumwangalia alikuwa ni yeye kabisa.”
Alisema walipomuhoji mama yake huyo kwamba
ametokea wapi, aliwaeleza kuwa ametoka eneo la Katoro kwa mganga na
aliletwa na watu ambao hakuwatambua Alhamisi saa 1:30 usiku ndani ya
gari na watu hao walimshusha kwa mtu aitwaye Juma Luchunga ambaye ni
jirani na dada zake hao.
Kauli ya Flora
Akizungumza na waandishi wa habari, Flora alisema
yeye ni mkazi wa Katoro na kwamba alitokea Katoro nyumbani kwa mganga wa
jadi ambaye hata hivyo hakumtaja kwa maelezo kwamba wataalamu wake
(majini) wamemkataza.
“Nilikuwa naishi kwa mganga wa kienyeji ila
alikuja mwanaume wakati nikiwa pale akaninywesha dawa kisha tukapakizwa
kwenye gari na watu wawili ambao sikuwatambua, mmoja mwanamke na
mwingine mwanaume mpaka hapa Kasamwa tukashushwa saa 1:00 jioni,”alisema
Flora.
Alisema alipofika Kasamwa alikwenda kunywa uji kwa
mama mmoja ambaye pia hakumtaja na kwamba baadaye alipelekwa nyumbani
kwa mtu mwingine saa nne usiku, lakini watu wa nyumba hiyo walipomwona
walimwambia: “Hapa si kwako twende tukupeleke kwa ndugu yako” na ndipo
wakampeleka kwa dada yake ambako aliketi nje hadi alfajiri.
Flora alisema kabla ya kuishi kwa mganga alikuwa
akiishi porini ambako alitupwa na watu asiowafahamu na baadaye aliokotwa
na wasamaria wema ambao ndiyo walimpeleka kwa mganga ambako alikuwa
akiishi muda wote.
Kuhusu ndugu, Flora alisema ana ndugu zake Sengerema na Geita kwamba Sengerema ndiko alikokuwa akiishi kabla ya kwenda porini.
Kadhalika mwanamke huyo anayedaiwa kufufuka
alisema ana watoto watano, (idadi ambayo ni sawa na ile aliyoacha
marehemu Flora), lakini alipoambiwa awataje alikuwa akichanganya majina.
Ndugu wapishana
Baba mzazi wa mwanamke huyo, James Tunge ambaye
aliitwa baada ya kutokea tukio hilo alisema kuwa mwanaye alifariki,
lakini anashangaa kuona leo anaonekana tena.
Hata hivyo, Tunge alisema alipomwona mwanamke huyo
juzi asubuhi alikuwa akifanana kabisa na mwanaye Flora, lakini
alipoondoka kwenda kufuata picha yake na kurejea alikuta amebadilika,
kwani kovu alilokuwa nalo kabla ya kifo halikuwa likionekana.
“Kwa sasa naweza kusema huyu siyo ila asubuhi
wakati namwona ni kweli alikuwa mwanangu marehemu, najua mwanangu
alikuwa na kovu kubwa puani na shavu la kushoto, lakini sasa hivi
anaonekana ana kovu moja la shavuni ila sehemu zingine za mwili
wanafanana kabisa,”alisema Tunge.
Kwa upande wake Jubili alisema kuna kila dalili
kwamba mwanamke huyo ni mdogo wake, kwani anavyojieleza maelezo yake
yanafanana. Alisema anawatambua watoto wake na ndugu japo wakati
mwingine ni kama anapoteza kumbukumbu na kubadilika badilika sura.
“Wakati tunamwona asubuhi alikuwa akifanana na
dada yangu marehemu, kwani dada alikuwa na kovu kubwa puani na shavuni
na kweli alikuwa nalo na baadaye tulipoendelea kumuhoji alianza
kubadilika sura na mara kovu likawa halionekani tena, “alisema Jubili.
Kwa ujumla ndugu wa mwanamke huyo wanahusisha
tukio hilo na ushirikina kwa kusema kwamba huenda ndugu yao alichukuliwa
kwa njia za giza, lakini Mungu amemwezesha kurejea katika maisha ya
kawaida.
Jubili alisema kifo cha Flora miaka mitano
iliyopita kilikuwa cha mazingira ya kutatanisha, kwani aliugua ghafla
baada ya kula viazi vitamu kwenye mji wa jirani na hapo kuanza kuvimba
tumbo.
Kwa kuzingatia mazingira hayo, juzi Flora
alipelekwa wilayani Sengerema kwa mganga wa jadi aliyejitambulisha kwa
jina la Dk. Mkonogi Masendena .
Kabla ya kupelekwa Sengerema, suala hilo
lilifikishwa polisi ambao baadaye waliruhusu Flora kuondoka na wanaodai
kwamba ni ndugu yao na hata walipofika Sengerema walilazimika kwenda
polisi kwanza.
Polisi mkoani Geita walithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba ndugu zake waliondoka naye.
No comments:
Post a Comment