Mjane wa marehemu Hussein Semdoe akiwa amempakata mtoto wake wamiezi mitatu
Kilindi. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk
Abdallah Kigoda ameongoza mamia ya watu katika kumzika mwandishi wa
habari wa gazeti hili, Hussein Semdoe aliyefariki dunia Alhamisi
iliyopita kutokana na ajali ya gari iliyotokea wilayani Handeni na
kusababisha vifo vya watu watatu.
Dk Kigoda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Handeni
alisema alilazimika kuacha kikao cha baraza la mawaziri na kuruhusiwa
na Rais Jakaya Kikwete kuhudhuria mazishi hayo.
Alisema Rais Kikwete amestushwa na vifo hivyo vilivyosababisha vya waandishi wa habari wawili na Ofisa Uhamiaji.
Semdoe alizikwa katika shamba la baba yake Kijiji
cha Mafureta wilayani hapa katika mazishi yaliyohudhuriwa na umati wa
watu kutoka mikoa mbalimbali wakiwamo wawakilishi wa klabu za waandishi
wa habari za mikoa ya Pwani na Morogoro na Tanga.
Mwakilishi wa Kampuni ya Mwananchi Mkoa wa Tanga,
Burhani Yakub aliwasilisha kwenye mazishi hayo salamu za Mkurugenzi na
wafanyakazi wa MCL.
Alisema: “Mkurugenzi, wahariri, waandishi wa
habari pamoja na wafanyakazi wa Mwananchi Communications Ltd kwa ujumla
wamestushwa na kifo cha Semdoe na kwamba ameacha pengo kubwa ambalo
halitaweza kuzibika kirahisi.”
Alisema wakati wa uhai wake alikuwa tegemeo la kampuni katika kuandika habari za wilaya za Kilindi na Handeni.
Burhan aliwasilisha kwa familia ya marehemu ubani wa Sh 621,000.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa alifika
kwenye mazishi hayo akiwa ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya mkoa kuwafariji wafiwa.
Akizungumza katika msiba huo, Gallawa alisema,
Semdoe na wenzake wamekufa wakati wakilitumikia taifa kwa sababu
walikuwa wakienda kupanda miti.
Hata hivyo, Gallawa alilazimika kwenda pia kwenye
mazishi ya mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru na Mzalendo, Hamis
Bwanga aliyezikwa Muheza. Baadaye pia alienda kuhudhuria mazishi ya
Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Handeni, mjini Handeni. Wote walikumbwa na
mauti katika ajali hiyo.
Marehemu Semdoe ameacha mjane, Mariam Semdoe
pamoja na watoto watano; Najma, Hussein, Saadam, Saada na Shakira ambaye
ana umri wa miezi mitatu.
No comments:
Post a Comment