Dar/Dodoma. Mvutano kuhusiana
na mchakato wa kupata Katiba Mpya unaozigonganisha Serikali na Chadema
ulizidi kupamba moto bungeni jana wakati wa mjadala wa kuhitimisha
hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alitumia muda
wake karibu wote wa saa moja kujibu maoni na kumshambulia Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyoyatoa kuhusu hotuba
ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hoja za Mbowe zilizoonekana kumsumbua Pinda ni
malalamiko dhidi ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi na kauli yake kwamba serikalini hakuna weledi wa kuwezesha
kupanga mipango ya maendeleo.
Hata hivyo, baada ya kuhitimisha hotuba hiyo,
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisimama kuomba mwongozo wa Spika chini
ya kanuni ya 68 (7) akidai kuwa Pinda alikuwa ametoa kauli ya uongo kuwa
Chadema haikuwasilisha mapendekezo yake juu ya muundo wa Mabaraza ya
Katiba, badala yake walilalamika tu kwenye mkutano wa hadhara.
Akizungumzia, Pinda alieleza kumshangaa Mbowe
kwa kudai kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba haina weledi wakati kuna
maprofesa na kati ya hao ni Profesa Mwesiga Baregu wa Chadema.
“Hivi
kweli hawa wazee na maprofesa ni mambumbumbu kweli au ni kauli ambayo
hakuipangilia. Haiwezekani kwa mjumuiko wa wazee wote waliomo mle ndani.
“Tuwatendee haki Watanzania na tusiwakatishe
tamaa wazee wetu ambao wamezunguka nchi nzima na kufanya kazi kubwa,
kama haya ndiyo Mbowe ametumwa basi nadhani aliteleza.”
Pinda alisema kama kuna tatizo kwenye mchakato ni kutokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa na Bunge.
Wakati anazungumzia suala hilo ilisikika sauti
kuwa wakati sheria hiyo inapitishwa Chadema walitoka bungeni, na Pinda
alirudia, “Nasikia kuwa mlitoka bungeni.”
Pinda alisema kutakuwa na
Bunge la Katiba na wabunge wote ni wajumbe, pia kwa Zanzibar kuna Baraza
la Wawakilishi, hivyo Mbowe kuanza kutoa maoni hayo inaonyesha wana
hofu.
“Kama Chadema wana hofu basi ni jambo lingine,
nilipoisoma `speech’ (hotuba) ya Mbowe mawazo yake yanaonyesha anawaza
uchaguzi wa 2015 na si kitu kingine,” alisema Pinda na kupigiwa makofi
na wabunge wa CCM.
Alisema Mbowe alimtisha zaidi pale aliposema kuwa wataitisha maandamano nchi nzima kupinga suala hilo, kitu ambacho si sawa.
“Wananchi msiambiwe mwandamane, kama mnapinga
basi mpinge wenyewe, kwani akili za kuambiwa inabidi uchanganye na
zako,” alisema Pinda na kuongeza:
“Tume haiwezi kufanya kazi kisiri na tume
haitoi taarifa kwa Rais kama ilivyodaiwa na Mbowe, bali inatoa taarifa
kwa umma wote. Alichosema Rais Jakaya Kikwete ni ratiba ya tume ambayo
imo kwenye sheria na ilikuwa imeshatolewa na Mwenyekiti wa Tume Jaji
Joseph Warioba kwenye vyombo vya habari.”
Kuhusu suala la Mabaraza ya Katiba kukaa
ki-CCM, alisema kama ni hivyo basi Bunge ndiyo lililofanya makosa kwa
kuwa ndiyo lililopitisha kuwa wajumbe watapitishwa na Mkutano wa
Maendeleo wa Kata (WADC).
“Bado tuna mwanya mkubwa sana huko mbele wa kurekebisha mambo haya na kufika mahala pazuri,” alisema Pinda.
Alisema kinachowatia hofu Chadema ni kuwa
mikutano ya WADC ina wenyeviti wengi wa CCM, jambo alilosema ni zuri kwa
kuwa ndiyo wameaminiwa na wananchi.
Pinda alisema kuwa hata hiyo
Tume ya Katiba ilipotaka wadau watoe mapendekezo ya mfumo wa mabaraza
hayo Chadema haikuwasilisha lakini baada ya muundo uliopo kupangwa ndipo
chama hicho kilitoa maoni kwenye mkutano wa hadhara.
Kauli hiyo ndiyo ilimfanya Mnyika aombe mwongozo wa Spika
akisema Pinda alitoa kauli ya uongo kwa kuwa chama hicho kiliwasilisha
mapendekezo yake lakini hayakuzingatiwa.Kabla ya kuanza kutoa
mashambulizi kwa Mbowe, Pinda alianza kutuma ujumbe kwa wabunge wawili
wa CCM waliotangaza wazi kuwa wasingeunga mkono bajeti yake.
“Nawashukuru sana kwa michango yenu Lugola
(Kangi Lugola) na Filikunjombe (Deo) kwa kukataa kuunga mkono hoja,
tutafanyia kazi maoni yenu, lakini nimeshindwa kumwelewa Filikunjombe
aliposema tuchukue hoja za wapinzani tuzifanyie kazi,” alisema Pinda.
Kadhalika Waziri Mkuu alisema hoja ya Chadema
ya kutaka Waziri wa Elimu na Mafunzo, Dk Shukuru Kawambwa kuwajibika
halina tatizo ila ni baada ya tume aliyoiunda kujua tatizo la wanafunzi
kufeli mitihani.
“Endapo ikibainika kuna uzembe ambao
ulijitokeza suala la Kawambwa kuwajibika hilo halina shida hivyo
tusubiri tume itakuja na taarifa gani,” aliongeza Pinda.
Maoni ya Mbowe
Wakati
Waziri Mkuu akisema hayo, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe alisema mchakato huo wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba hauko sawa na watajitoa kama walivyokwisha kusema.
“Utaratibu wa mabaraza ya katiba
haukuzingatiwa,tunataka kulifumbia macho hili tunataka kujenga ufa wa
wananchi na huu mpango ukiendelea hivi tutawaachia ninyi muendelee.
“Kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
isipoletwa Bungeni tukiomba rejeo ya mambo mawili ya sheria hiyo
hatutakuwa na uhalali wa kuendelea kushiriki mchakato huu kwani kinyume
cha utawala bora na mabaraza haya hatuyakubali na tutajitoa mwishoni mwa
mwezi huu”.
Alisema kupatikana kwa Katiba Mpya na
iliyoshirikisha wananchi itasaidia kutibu majeraha ya wananchi
waliyokwisha yapata kutokana na ubovu wa Katiba iliyopo.
Mawaziri 10 tu wachapakazi
Mbunge
wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) amesema Tanzania inashindwa kupiga
hatua kimaendeleo kwa kuwa asilimia kubwa ya mawaziri wa Serikali ya
Awamu ya Nne hawafanyi kazi.
Akizungumza wakati akichangia Hotuba ya
Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma jana, Filikunjombe
alisema kati ya mawaziri 55 wa Serikali ya Awamu ya Nne, wanaofanya kazi
zao kikamilifu hawazidi 10.
Filikunjombe alitishia kuwa hahofii chochote
na ana uwezo wa kuwataja mawaziri wachapakazi na wale ambao hawafanyi
kazi kwa kuzingatia viapo na maadili ya uongozi.
Alitoa mfano huo kwa maelezo kuwa hoja
mbalimbali zinazotolewa na wabunge na wananchi kuhusu wizara husika,
nyingi zimekuwa hazifanyiwi kazi na badala yake ahadi na uundwaji wa
tume ambazo ripoti zake zinakaliwa.
“Viongozi wa Serikali wanafanya mambo
wanavyojua wao, mawaziri wakati wanaapishwa wakiahidi kuwa watailinda
Katiba ya nchi, badala yake wanalindana wao wenyewe na badala ya
Katiba,” alisema Filikunjombe.Imeandikwa na Reginald Miruko, Boniface
Meena, Ibrahim Yamola na Fidelis Butahe.
“Kiwango cha elimu
kinazidi kushuka na tume zilishaundwa miaka iliyopita kuchunguza suala
hilo na kuja na majibu mazuri, lakini badala ya kufanyia kazi
mapendekezo hayo sisi tunaunda tume nyingine,” alilalamika Filikunjombe.
Alisema kuwa mawaziri hao kila wanapoelezwa
mambo mbalimbali wengi husema kuwa mchakato unaendelea, tutafuatilia kwa
kina suala hilo, kwamba majibu hayo hayajibu hoja za msingi
zinazowasilishwa.
Mbali na kutounga mkono hoja za Waziri Mkuu
wakati akiwasilisha bajeti yake, alisema Serikali imekuwa ikiunda tume
kwa kigezo cha kuzima hoja.
“Tume zikishaundwa ujue kuwa mambo ndiyo
yamekwisha, tufike mahali sisi kama viongozi tubadilike jamani,
tunaelezwa kuwa elimu ya msingi ni bure, sasa mbona wazazi wanatoa fedha
nyingi kuchangia michango.”
Alisisitiza kuwa huo ndiyo udhaifu mkubwa kwa baadhi ya
viongozi, na kuongeza kuwa hata hoja zinazotolewa na vyama vya upinzani
kuhusu utendaji mbovu wa viongozi wa Serikali nyingine zina ukweli ndani
yake.
“Tusipinge kila hoja ya wapinzani bali
tuzifanyie kazi, nasema hivi kwa sababu hata kobe ukimkuta juu ya mti
ujue kapandishwa,” alionya Filikunjombe.
Aliwataka watendaji wa Serikali kutimiza malengo na wajibu na kwamba hiyo ndiyo njia nzuri ya kuwanyamazisha wapinzani.
No comments:
Post a Comment