Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akiwa ameongozana na mlinzi wake dakika
chache baada ya kuapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo jana.
Ataanza kwa ahadi ya matibabu bure kwa wanawake wanaofuata huduma za uzazi
Nairobi. Rais wa Kenya, Uhuru
Kenyatta amesema kwamba atatumia siku 100 tu kutekeleza ahadi zake
zote ambazo ameziahidi kipindi cha kampeni.
Alisema kwanza atatumia miezi mitatu tu kuondoa
kabisa malipo ya Afya ya uzazi kwa kina mama katika zahanati zote na
hospitali za umma.
Alisema kwamba Serikali yake itatoa kiasi cha Sh6 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mfuko wa vijana na wanawake .
Pia alikumbushia ahadi ya kutoa ‘laptop’ kwa wanafunzi wote wa shule za msingi watakaojiunga na shule za serikali mwakani.
Uhuru alisema kwamba kutekeleza ahadi hizo ni katika suala la utekelezaji wa sera na misimamo wa Muungano wa Jubilee.
“Mimi nina fahari kubwa kuwajali wanyonge
waliokubali kunipa nafasi hii ya uongozi na nimekubali kulivaa vazi hili
la uongozi hivyo nitasimamia sera za Jubilee kama tulivyoahidi Wakenya
wakati wa kampeni,’’ alisema Uhuru.
Aliongeza kwamba yupo kwa ajili ya Wakenya wote waliompigia kura na hata wale waliowapigia wapinzani wake.
Uhuru alisema atawasaidia Wakenya pamoja na taifa
zima kuelekea katika mizizi imara ya kiutajiri kwa njia ya amani, hali
ambayo alisema inawezekana ikafanikiwa kwa kiasi kikubwa baadaye.
Naye mtaalamu wa Uhusiano wa Kimataifa, Profesa
Munene Macharia alipokuwa akifanya mahojiano na Kituo cha Habari cha
Xinhua ,alisema kwamba kuchaguliwa kwa Rais Uhuru Kenyatta, kuna
uwezekano mkubwa kubadilika kwa sera za kiuchumi.
Alisema kwamba Rais
huyo ambaye awali alikuwa katika Baraza la Mawaziri la awamu
iliyopita akiwa Waziri wa Fedha anatakiwa kujenga uhusiano wa karibu na
mataifa ya nje ili aweze kubadili sera za kiuchumi.
Pia alimtaka waziri huyo kuangalia suala la kuimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi jirani za Afrika na Afrika Mashariki.
Profesa Macharia alisema baada ya kuitumikia Serikali ya Kibaki, Kenyatta ana uwezo mkubwa wa kudumisha sera hiyo ya kiuchumi.
“Lengo
la msingi kwa Serikali ya Kenyatta inatakiwa kuimarisha mahusiano yake
na Jumuiya ya Afrika Mashariki nchi wanachama (EAC) Kama majirani wa
karibu,” Macharia alibainisha.
Wakati huohuo Rais mstaafu Mwai
Kibaki aliwahakikishia raia wa Wakenya kuwa, wapo katika mikono salama
baada ya yeye kustaafu rasmi juzi.
Alisema kwamba yeye anaanza maisha yake ya
kustaafu, hivyo raia wote wa nchi hiyo wanatakiwa kufahamu kwamba
wanabaki katika mikono salama wasiwe hivyo wasiwe na hofu yoyote ile.
No comments:
Post a Comment