Chadema yatishia kujitoa kwenye mchakato wa Katiba
Msemaji wa kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHadema),
kimesema hakitashiriki katika mchakato wa Katiba Mpya endapo serikali
haitapeleka bungeni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ili kufuta vifungu
mbalimbali kikiwamo kinachowaruhusu wajumbe wa Bunge Maalum kutoka
Zanzibar kushiriki katika mijadala ya mambo yasiyo ya muungano.
Chama hicho kinataka marekebisho hayo kupelekwa bungeni kabla ya mwisho
wa Aprili na isipofanya hivyo kitajitoa katika ushiriki wake katika
mchakato huo.
Hayo yalisemwa jana na Msemaji wa kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe,
alipokuwa akitoa maoni ya kambi hiyo kuhusiana na hotuba ya bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2013/2014.
Pia Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai, alisema chama chake kitajitoa katika
ushiriki ikiwa serikali haitafuta uteuzi wa wajumbe wa mabaraza ya
Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za kata.
Alisema wajumbe hao wafutwe na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba
ya wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila
kuchujwa na WDC.
Pia alisema wanataka kufutwa kwa vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya
Rais kuitisha tena Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa
limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho
katika Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni.
Aidha, alisema wanataka kufutwa kwa vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya
kikatiba na ya kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kuendesha na kusimamia kura ya maoni.
Alisema Tume hiyo imeonekana kutoa taarifa kwa Rais Jakaya Kikwete na
kutangaza wazi wazi kwamba haiwajibiki kwa Bunge kuhusu utekelezaji wa
majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.
“Zaidi ya kumtuma Naibu Katibu wa Tume, viongozi wa Tume kama vile
Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume wamekataa kuhudhuria
vikao vya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ili kuieleza
Kamati juu ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na
Katiba ya Nchi,” alisema Mbowe.
Kwa upande wa wanafunzi waliofeli mitihani ya kidato cha nne mwaka jana,
Mbowe alisema kambi hiyo inaitaka Serikali kueleza bungeni inampango
gani wa kupunguza idadi hii ya watoto wanaobaki mitaani bila shughuli
rasmi ya kufanya.
No comments:
Post a Comment