Waandishi wafa ajalini

Mwandishi wa gazeti la NIPASHE wilayani Handeni, Sonyo Mwankale.

Mwandishi wa gazeti la NIPASHE wilayani Handeni, Sonyo Mwankale, ni miongoni mwa watu watatu waliofariki dunia wakiwa kwenye msafara wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, baada ya gari walilokuwa wakisafiria la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuacha njia na kupinduka.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 3:30 katika kijiji cha Misima wakati wakielekea katika kijiji cha Nzundu kwenye zoezi la upandaji miti lililokuwa likifanyika kiwilaya kijijini hapo.

Aliwataja waliofariki papo hapo baada ya ajali kutokea kuwa ni Hamis Bwanga ambaye ni mwandishi wa gazeti la Uhuru na Mzalendo na Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Handeni, Mariamu Hassani.

Rweyemamu alisema mwandishi wa gazeti la NIPASHE, Sonyo Mwankale (Hussein Semdoe), alifariki dunia akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni akipatiwa matibabu.

Katika ajali hiyo, Mwankale ambaye alijeruhiwa vibaya sehemu za kichwani, baada ya kupelekwa hospitalini hapo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni alimuomba helkopita Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Said Mwema, kuwachukua majeruhi hao, lakini kabla haijafika mwandishi huyo akafariki dunia.

Wengine waliyojeruhiwa katika ajali hiyo na kulazwa kwenye hospitali hiyo ni Mshauri wa Mgambo Wilaya, Athanas Paulo, Ofisa Misitu Wilaya, Natorin Mloe na dereva wa gari hilo lenye namba za usajili STK 4673, Mlawa Makata.

Awali, taarifa ambazo NIPASHE ilizipata zilieleza kuwa tukio hilo limetokea wakati msafara huo ukitokea Mjini Handeni kuelekea Misima ambako Mkuu huyo wa Wilaya alikwenda kuhamasisha upandaji wa miti.

Habari zilieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni gari hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Handeni, kupasuka gurudumu la nyuma na kuacha njia kisha kupinduka. Hata hivyo Mkurugenzi huyo hakuwamo katika gari hiyo.

Wakizungumzia ajali hiyo, kwenye eneo la tukio, mashuhuda hao alisema watu hao walipoteza maisha muda mfupi mara baada ya tukio hilo na kwamba wananchi waliyojitokeza kutoa msaada walishuhudia hali za majeruhi hao zikiwa mbaya.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Rweyemamu akizungumzia tukio hilo alisema kifo cha Afisa Uhamiaji huyo ni pigo kwa wilayani kwani ni hivi karibuni alisaidia kukamatwa kwa wahamiaji haramu 74.

Ofisa misitu Wilaya ya Handeni, Mloe akizungumzia jinsi ajali hiyo ilivyotokea akiwa katika hospitali ya Wilaya Handeni alikolazwa, alisema wakiwa safarini mbele alijitokeza mwendesha pikipiki (bodaboda) akitaka kujaribu kuwapita.

Alisema dereva wa gari lililobeba alimkwepa dereva wa bodaboda na kusababisha gari kuyumba na kusababisha kupinduka upande wa pili wa barabara na hivyo kusababisha kifo cha Afisa Uhamiaji na mwandishi wa gazeti la Uhuru papo hapo.

No comments:

Post a Comment