Mtuhumiwa namba moja wa mashtaka 24 ya kuua bila kukusudia, Raza Hussein
Ladha (kushoto) akipelekwa chini ya ulinzi wa polisi kuingia katika
chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara Radha Hussein
Ladha wa jijini Dar es Salaam, Diwani katika Manispaa ya Kinondoni,
Ibrahim Mohamed maarufu kama Kisoki (59) na wenzao 9, jana walifikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 24 ya
kuua bila ya kukusudia.
Katika kundi hilo pia wamo vigogo wa Manispaa
ya Ilala ambao ni Mhandisi Mkuu, Mhandisi Charles Salu (48), Mhandisi wa
Majengo Godluck Sylivester (35) Mbaga na Mkurugenzi Mkuu wa Mkaguzi wa
Majengo, Willibrod Wilbard (42).
Washtakiwa wengine ni Mhandisi Mohamed Swaburi
(61), Mhandisi Mshauri, Zonazea Oushoudada (60), Mkadiriaji Majenzi,
Vedasto Nziko (59), Msanifu Majengo, Michael Hema (59), Msajili Msaidizi
AQRB, Albert Mnuo na Ofisa Mkuu Mtekelezaji OQRB, Joseph Ringo.
Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu
Mkazi, Devotha Kisoka, Wakili wa Serikali, Tumain Kweka akisaidiana na
mawakili wenzake watano, alidai kuwa washtakiwa walifanya makosa kinyume
na kifungu cha 195 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16
iliyofanyiwa marekebisho 2002.
Kweka anasadiana na wenzake Benard Kongora, Ladslaus Komanya, Neema Haule, Joseph Maugo na Mutalemwa Kishenyi.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao
kwa pamoja Machi 29, mwaka huu katika Mtaa wa Indira Gandhi, Wilaya ya
Ilala waliwaua bila ya kukusudia Yusuph Mohamed, Kulwa Khalfan na Hamada
Mussa.
Mbali na watu hao, pia wanadaiwa kuwaua bila
ya kukusudia Kessy Manjapa, Khamis Mkomwa, Boniface Benard, Suhail Ally,
Salmani Akbar, Seleman Haji, Seleman Mtego, Sikudhani Mohamed, Ahmed
Milambo, Salum Mapunda, Suleiman Rashid na John Majewa.
Wengine ni Mussa Mnyamani, David Severin
Herman, William Joackim, Abdulrahman Mwiha, Emmanuel Christian, Mmanyi
Ngadula, Adivai Desiki, Emmanuel Greyson na Augustino Kasiri.
Washtakiwa
wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mashtaka yanayowakabili
Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza hadi Mahakama Kuu.
Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili wa
Kujitegemea, Jerome Msemwa waliiomba mahakama kutoa dhamana kwa wateja
wao kwa sababu mashtaka ya kuua bila ya kukusudia yanayowakabili
yanadhaminika.
Wakili wa Serikali, Kongora alipinga maombi
hayo, huku wakili mwenzake Komanya akisema kuwa wakati huu si wa kutoa
dhamana kwa kuzingatia mazingira ya tukio lililosababisha kuwepo kwa
kesi hiyo.
Kutokana na hoja hizo, Hakimu Kisoka
aliiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 16, mwaka huu atakapotoa uamuzi iwapo
washtakiwa wapate dhamana ama la.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ametangaza kiama dhidi ya
wamiliki wenye maghorofa yaliyojengwa kinyume cha utaratibu jijini Dar
es Salaam.
Akizungumza kwenye Ofisi ndogo ya Bunge, Profesa
Tibaijuka alisema kwa kuanzia angesaini hati ya kuamuru kubomolewa kwa
jengo lililokuwa karibu na lile lililoanguka wiki iliyopita na kuua
idadi kubwa ya watu.
Alimwonya mmiliki wa jengo hilo anatakiwa kufanya ubomoaji mara moja tena kwa gharama zake.
“Serikali ikibomoa jengo hilo ina maana
atatakiwa kulipia gharama za zoezi hilo,” alionya Profesa Tibaijuka,
ambaye aliapa kuanza leo ukaguzi wa maghorofa mbalimbali ya jijini Dar
es Salaam.
No comments:
Post a Comment