Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk
Abdallah Kigoda, amesema Tanzania itakuwa nchi ya viwanda vya kati
ifikapo mwaka 2025 ikiwa wawekezaji watajengewa mazingira mazuri ya
kuwekeza.
Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda cha
kuzalisha wa ‘gypsum’ cha Kampuni ya Sunshine ya China kilichopo katika
Kata ya Visiga, Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani juzi, Dk Kigoda alisema
kuwa sekta ya viwanda inakuwa kwa kasi nchini.
“Kiwanda hiki ni muhimu kwa uchumi wa kata ya
Visiga na taifa kwa jumla. Uchumi wetu hauwezi kutegemea kilimo peke
yake, tunataka nchi yetu iwe ya viwanda vya kati ifikapo mwaka 2025,”
alisema Dk Kigoda.
Dk Kigoda alisema kwa sasa sekta ya viwanda
inachangia pato la Taifa kwa asilimia 30, hivyo ukuaji wa viwanda
utakuza pato hilo ikiwa wawekezaji watajengewa mazingira mazuri.
“Nimeambiwa kuwa tangu uamuzi wa kulifanya eneo
hilo la Visiga kuwa la viwanda tayari kuna viwanda vitano vya chuma,
kusafisha mafuta, kutengeneza nondo na hiki cha gypsum. Sekta ya viwanda
inachangia pato la Taifa kwa asilimia 30 na asilimia 40 ya ajira,’’
alisema.
hia Sunshine kuwa soko la bidhaa zao lipo kubwa,” alisema Dk Kigoda.
Alisema uwekezaji wa kampuni hiyo ambayo pia ina
kiwanda cha baruti kilichopo wilayani Kibaha na madini wilayani Chunya
Mkoa wa Mbeya, utazingatia wajibu kwa jamii (corporate social
responsibility)
Licha ya kuipongeza kampuni hiyo, Dk Kigoda
aliwataka wawekezaji hao katika sekta ya viwanda kuzingatia ubora wa
bidhaa wanazozalisha ili kukuza uchumi wa nchi.
Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hun Xue Hui,
alisema kampuni hiyo ambayo ni tanzu ya kampuni za Sunshine ya China
itatoa ajira rasmi kwa watu 60 na ajira nyingine zisizo rasmi na itakuwa
ikizalisha gypsum tani 700,000 kwa mwaka.
Aliongeza kuwa, wananchi wanaozunguka kiwanda hicho watafaidika kwa kupewa kipaumbele cha ajira na huduma za jamii.
Kwa upande wake mwakilishi wa Ubalozi wa China
nchini anayeshughulikia masuala ya siasa, Li Xuhang, alisema uwekezaji
wa viwanda unaendeleza uhusiano kati ya Tanzania na China uliodumu tangu
wakati wa uhuru.
“Mmefanya vizuri kuwekeza katika eneo hili kwani
wananchi nao watafaidika. Tanzania na China zimekuwa marafiki kwa zaidi
ya miaka 50, hivyo kwa niaba ya Balozi wa China nchini tunawaunga
mkono,” alisema Xuhang.