Kesi ya kukutwa na sare za polisi yaahirishwa


Dar es Salaam. Kesi inayomkabili James Hassani (45),anayekabiliwa na mashtaka ya kujifanya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani na kukutwa na sare za jeshi hilo imeahirishwa hadi Machi 26 mwaka huu.

Kesi hiyo imeahirishwa baada ya mshtakiwa kuugua ugonjwa wa mafindofindo na kudai kuwa hataweza kufika mahakamani. Hii ni mara ya tatu kwa kesi hiyo kuahirishwa baada ya Februari 26 mwaka huu Mahakama kuiahirisha kesi hiyo baada ya shahidi wa pili katika kesi hiyo kuwa mgonjwa.

Hakimu Janeth Kinyage aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 26, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa na mshtakiwa alirudishwa rumande. Kesi hiyo ipo katika hatua ya kutoa ushahidi na tayari shahidi wa kwanza ameshatoa ushahidi wake.

Hata hivyo, Mahakama ya Wilaya ya Ilala ilimfungia dhamana Hassani, baada ya kubaini kuwa mshtakiwa huyo alikuwa na kesi nyingine iliyosababisha kutoroka katika Gereza la Msanga lililopo mkoani Dodoma alipokuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela.

No comments:

Post a Comment