Balozi Msuya : Vijana acheni kukimbilia Sauzi si peponi

Balozi Radhia Msuya 


Pretoria. Kwa siku za karibuni limetokea wimbi kubwa la vijana  wa Kitanzania kukimbilia nchi mbalimbali duniani ikiwamo Afrika Kusini kwa madai ya kusaka maisha bora.

Baadhi ya vijana hao wamekuwa wakikamatwa na hata kurudishwa nchini baada ya kukosa uhalali kisheria wa kuendelea kuishi katika nchi hizo.

Wengine kati yao wamejikuta matatani kwa kuhusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya pamoja na maovu mengine baada ya  kuingia katika nchi hizo kwa njia halali na zisizo halali.

Kwa upande wa Afrika Kusini, baadhi ya vijana hao wemeamua kuhamishia shughuli zao za kibiashara nchini humo.

Balozi wa Tanzania nchini humo, Radhia Msuya  anasema vijana wengi wanadanganyika kwa kufikiri kuwa maisha katika nchi hiyo ni rahisi na kuwa baada ya kufika huko mambo yatakuwa rahisi na kinyume chake mambo huwawia magumu na baadhi yao kuhitaji msaada wa kurudishwa nyumbani.

Vijana 200 kwa mwezi

Balozi Msuya anasema kila mwezi wastani wa vijana  200 hurudishwa nyumbani Tanzania kutoka nchini humo kutokana na sababu mbalimbali wakiwamo wale walioingia katika nchi hiyo bila vibali.

 ‘’Huku siyo peponi, maisha bora yanafanyiwa kazi kama ilivyo huko nyumbani. Kila mwezi tunarudisha nyumbani vijana  200 wanaokamatwa mitaani hapa wakiuza  bidhaa ndogo ndogo huku wengi wao wakiwa hawana vibali,’’ anasema Balozi Msuya.

 Anasema shughuli ndogo ndogo za biashara wanazofanya vijana hao kutoka Tanzania haziwawezeshi kumudu gharama kubwa za maisha nchini humo na baadhi yao hudaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha, balozi  huyo  anawataka vijana wasiamini kuwa majibu yote ya changamoto zote zinazowakabili yanapatikana serikalini.

Anasema  baadhi ya majibu ya changamoto hizo yako mikononi mwao na utatuzi wake siyo lazima kukimbilia nchini humo.

 Anasema ni kweli  Afrika Kusini imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo maendeleo  ya kiuchumi, ingawa  pia yapo matatizo mengi  ambayo vijana hukumbana nayo baada ya kufikiri kwamba kukimbilia nchini humo litakuwa ni suluhisho la matatizo yote waliyoacha nyumbani.

 

“Ni kwamba  changamoto kubwa iliyopo ni vijana wetu kuacha kukimbilia nchini humu kwa dhana kwamba ‘wataukata’ tena bila ofisi za ubalozi wetu kuwa na taarifa za ujio wao. Baadhi ya vijana hao kupata matatizo ndipo hukumbuka  hukimbilia katika ofisi  yetu kwa ajili ya kupatiwa msaada,” anaeleza Balozi Msuya.

 Kifo cha Mangwea

Mathalan, Balozi Radhia Msuya  anasema ofisi za ubalozi wake hazikuwa na taarifa za ziara au safari ya msanii maarufu wa Tanzania, Albert  Mangwea kwenda nchini humo miezi michache iliyopita na hata alipofariki ghafla wao walipata wakati mgumu sana katika kufuatilia na kupata taarifa zake.

 Anasema baada ya taarifa za kifo cha msanii huyo kusambaa kwenye mitandao watu wengi  kutoka Tanzania  walipiga simu katika ofisi za ubalozi mjini Pretoria ili wapewe ukweli wa tukio hilo,ilihali ofisi za ubalozi hazikuwa na taarifa za msanii huyo kuwamo nchini humo.

Balozi huyo anabainisha kuwa huo ni mfano mmoja wa Watanzania wanaoingia nchini humo bila taarifa.

Anaeleza kuwa hivi sasa ni vigumu kufahamu Watanzania wanaoingia na kutoka nchini humo baada ya kufutwa kwa viza kati ya nchi hizo na hivyo kukata mkondo wa mawasiliano ambao ungewalazimisha kufika katika ofisi za ubalozi.

‘’Kifo cha Ngwea (Albert) kwa upande wetu kimetupa uzoefu, tunakosa  taarifa kamili za Watanzania wote wanaofika na kuondoka hapa nchini baada ya kufutwa kwa viza. Hata hivyo, hilo haliondoi wajibu wetu kama ofisi za ubalozi,’’ anabainisha Balozi Msuya.

 Anatahadharisha kuwa ni muhimu raia yeyete anayefika nchini humo kutoa taarifa kwenye ofisi za ubalozi huo ili kujenga uwezekano wa kupata msaada haraka endapo atapata matatizo tofauti na sasa ambapo wengi wao hawaoni ulazima wa kufanya hivyo.

Mtazamo wa Bushoke

Naye Maxmilian Bushoke, msanii Mtanzania anayefanya shughuli za muziki jijini Johannesburg anasema vijana wengi wanakimbilia katika nchi hiyo kubwa kiuchumi barani Afrika wakidhani kuwa nyumbani  hakuna mazingira rafiki ya kazi wanazofanya.

Anasema wapo vijana wengi kutoka nyumbani katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Johannesburg wanaofanya shughuli ndogo ndogo za biashara na kukiri wengi wao kuhusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya. 

Utalii Afrika Kusini

 Akizungumzia nafasi ya vivutio vya utalii nchini Afrika Kusini, Balozi Radhia Msuya anasema kuwa miongoni mwa kazi za ubalozi huo ni kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania na fursa za uwekezaji zilizopo ili kuongeza idadi ya watalii.

 Anasema kupitia ofisi za  ubalozi huo wamefanikiwa kushawishi watalii wengi nchini humo kutembelea Tanzania  hasa maeneo mbalimbali ya vivutio kama  Hifadhi za Taifa na kuwa matarajio ni kufanya vizuri zaidi kuwashawishi watalii wengi zaidi kutoka Afrika Kusini kutembelea nchi yetu.

 Hata hivyo, Balozi  Msuya anasema kuwa Tanzania haijapiga hatua kubwa katika masuala ya kuhifadhi mambo ya kale ikilinganishwa na nchi hiyo ya kusini mwa Afrika ambayo inapata fedha nyingi za utalii ikiwa ni matokeo ya kuhifadhi vyema maeneo muhimu ya  kihistoria. Anasema kwamba yapo mambo ambayo Watanzania wanafikiri ni madogo ingawa yana umuhimu mkubwa katika historia ya nchi.

Anasema kuwa yanayofikiriwa kuwa madogo ni vivutio vikubwa ambavyo huingiza fedha nyingi katika nchi zinazotunza vizuri historia. ‘’Wapo ambao hawana hata kumbukumbu ya cheti cha darasa la saba,hapo ndipo uhifadhi unapoanzia,kuna  vijana wengi ambao hawajui mambo muhimu  yanayohusu historia ya nchi yao,’’ anabainisha Balozi Msuya.

 Anatoa mfano wa eneo la Mnara wa Saa jijini Dar es Salaam analosema kuwa ni eneo muhimu katika historia ya nchi kwani hapo ndipo lilitolewa tamko rasmi  la kutangaza jiji hilo kuwa makao makuu ya nchi, lakini anahoji ni wangapi wanaojua jambo hilo. Hata hivyo, balozi huyo anasema eneo hilo limesahauliwa na hazionekani  dalili za kulihifadhi na kutangaza ‘mnara wa saa’ kama eneo muhimu la historia ya nchi.

Anasema eneo hilo limeendelea kuachwa kama lilivyo huku likisahauliwa na historia ya nchi, jambo ambalo ni hatari.

“Mambo mengi  yamesahaulika. Kwa mfano, njia alipopita Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa mguu wakati wa matembezi ya kuunga mkono Azimio la Arusha akitokea kijijini Butiama hadi Mwanza hazijulikani. Hakuna utambulisho wa  tukio hilo la kihistoria katika maeneo  aliyopita,” anaeleza na kutoa changamoto kwa mamlaka za umma nchini kushughulikia jambo hilo kama kivutio cha utalii.

Tanzania yajitosa kumsaidia Ruto

 

Serikali ya Tanzania, imeiomba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuruhusu Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto kutohudhuria baadhi ya mashauri ya kesi yake ili kuweza kutimiza majukumu mengine ya kiserikali.

Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Jaji Fredrick Mwita aliandika barua kwenda ICC Jumatatu wiki hii akitetea hoja ya Ruto kutaka asihudhurie baadhi ya vikao vya kesi hiyo.

Katika barua yake, Jaji Werema alisema kuruhusu Ruto kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi kutaimarisha ushirikiano baina ya ICC na washirika.

Hata hivyo, maombi hayo yanayotaka Ruto kuruhusiwa kutohudhuria kesi hiyo binafsi yamesimamishwa baada ya mwendesha mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda kuyawekea pingamizi na sasa yanasubiri uamuzi wa majaji.

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania, kuwasiliana na ICC kwani iliwahi kuwasilisha ombi la kutaka kesi hiyo ya kina Ruto isikilizwe Tanzania au Kenya.

Hata hivyo, mpango huo ulikwama baada ya majaji kuupinga kwa kura za hapana.

Mwandishi Sang ajitetea

Mwandishi wa habari wa kituo cha KASS FM Joshua Arap Sang, amekamilisha ungwe ya kwanza ya utetezi wake kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na kueleza kuwa hakuhusika kwa namna yoyote kuchochea machafuko yaliyojiri baada ya uchaguzi nchini Kenya.

Sang aliwasilisha utetezi wake katika hali ya kujiamini huku akionyesha sura yenye matumaini na kuiambia mahakama kuwa, kesi inayomkabili imetengenezwa ili kukatiza ndoto yake ya kuwa mtangazaji bora duniani .

Mwandishi huyo ambaye anatetewa na mawakili wanaoongozwa na Wakili Katwa Kigen, alipangua hoja zilizowasilisha na upande wa mashtaka kwa kutumia historia ya maisha yake aliyoyaelezea kuwa ni ya kumcha Mungu na uadilifu.

Kama ilivyo kwa washtakiwa wengine, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, Sang anadaiwa kuratibu na kupanga mashambulizi na kusababisha zaidi ya watu elfu moja kupoteza maisha.

Pia anadaiwa kuendesha kampeni ya uchochezi kupitia vipindi mbalimbali vya redio baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Mbele ya jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Sang alisema historia ya maisha yake inaeleza vyema namna alivyokuwa msaada kwa jamii, ikiwamo kushiriki kikamilifu shughuli za kanisa hivyo kutuhumiwa kuwa alihusika kwenye mauwaji ni dhihaka kubwa kwake.

“Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu ambaye kwake yeye nimepata nguvu na kusimama hapa. Nafahamu fika ipo siku mahakama hii itasimama katika haki na kuniachia huru. Itamwachia huru mwandishi wa habari.

“Lakini pia napenda niiarifu mahakama hii kuwa mimi ni kiongozi wa kwaya tena nategemewa sana na wenzangu, sasa kuambiwa kuwa nimeratibu mauaji ya raia ni jambo linalonisononesha sana tena limenivuruga mno,” alieleza Sang.

Katika kile kilichoonekana kama njia ya kuupa nguvu utetezi wake, Sang mbali ya kuelezea uzoefu wa kazi yake lakini alirudia mara kadhaa kutamka maneno yaliyotafsiri hisia zake dhidi ya kesi hii.

“Kusema kweli haya mashtaka yamenisononesha na kunivuruga. Mimi ni mzazi na pia ni mume mwema, itakuwaje sasa nithubutu kufanya jambo hili la kuua wenzangu, haiwezekani. Nimesikitika na kusononeka sana”.

Uzoefu wake

Baadaye aligeukia kipengele kilichohusu uzoefu wa kazi yake ambapo alitetea utendaji wake akisema; wakati wote alikuwa akifanya kazi kwa kuzingatia miiko na madili.

“Mimi ni mtangazaji wa siku nyingi tena nimefanya kazi hii katika vituo zaidi ya vitatu ambavyo vyote ni vya kidini, sasa huko kote nisifanye hilo la kuchochea mauaji nije kulifanya hapa Kass FM. Hiyo siyo kweli kabisa na hii kesi imeletwa kwa ajili kunivurugia tu safari yangu ya kuendelea kuwa mtangazaji.

Aliongeza: “Potelea mbali najua Mungu yupo na ataendelea kunipigania. Natambua kuwa mimi nilizaliwa kuwa mtangazaji na hadi leo nitabakia kuwa hivyo.”alisema

Aliiambia mahakama hiyo kuwa kazi ya utangazaji alianza kuipenda alipokuwa kijana mdogo na wakati fulani alilazimika kufuatilia matangazao yaliyokuwa yakirushwa na kituo cha BBC kwa ajili ya kujifunza na kupata taarifa za dunia.

“Waheshimiwa majaji mimi ni msikilizaji mzuri wa redio na kituo nilichokuwa nikikifanyia kazi Kass FM kinasikika kimataifa, hata hapa Netherland mimi nasikiliza redio hii, hivyo nina ufahamu wa kutosha wa kazi hii.

Napenda tu niseme haya mashtaka hayana ukweli wowote kabisa,”alisema.

Kuhusu vipindi alivyokuwa akiviendesha ambavyo vinadaiwa kupendelea kambi ya ODM, Sang alipuuza hoja hiyo kwa kueleza kuwa, wakati wa kampeni vyama vya siasa ndivyo vinavyolipia matangazo kwa ajili ya kutangaza sera zao.

“Pale Kass FM mimi ni mtu mdogo kabisa, sina uwezo wa kuamua jambo lolote lile mbali ya kufuata utaratibu uliowekwa na mmiliki wa kituo, lakini pia kusema mimi nilipendelea kambi ya ODM kwa kuwapa vipindi vingi hili siyo kweli kabisa, lazima tujue kwamba wakati wa kampeni vituo vingi huuza muda kwa wanasiasa ili watangaze sera zao ndivyo ilivyokuwa kwetu,” alieleza.

Sang pia alikanusha tuhuma za kuendesha vipindi vya redio vinavyodaiwa kurushwa kwa kipindi cha siku tatu kuanzia mwanzoni mwa Januari, 2008 vilivyokuwa vikiwahimiza wananchi wa kabila la Kilinjini kuanzisha machafuko.

Wanusurika kufa kwa pombe


Iringa. Zaidi ya watu 19 katika Kijiji cha Imega, katika Wilaya ya Kilolo, wamenusurika kufa baada ya kunywa pombe ya kienyeji inayodhaniwa kuwa na sumu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema tukio hilo lilitokea juzi wakati watu hao walipokwenda kuhudhuria sherehe iliyoandaliwa na mzee mmoja. Kwa mujibu wa kamanda huyo, sherehe hizo zilikuwa ni za kumuaga binti yake aliyekuwa akiolewa.

Alisema baada ya kazi hiyo, watu hao walianza kunywa pombe ya kienyeji na ilipofika jioni watu 19 walipatwa na ugonjwa wa tumbo. Kamanda huyo alisema baadaye watu hao walipelekwa katika Zahanati ya kijiji hicho kwa matibabu.

Alisema wakati wakiendelea kupata matibabu ,mmoja wa watu hao, alizidiwa na kukimbizwa katika Hosptali ya Itunda kwa matibabu zaidi. Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa huenda pombe walioitumia ilikuwa na sumu.

“Pombe hiyo inatokana na mahindi na inasemakana mahindi hayo yalikuwa na dawa. Tunafanya uchunguzi,” alisema Mungi.

WAHAMIAJI HARAMU 133 MBALONI JIJINI DAR ES SALAAM


Jijini Dar es Salaam hekaheka za wahamiaji haramu zimeendelea, baada ya watu 133 kutoka mataifa mbalimbali kutiwa mbaroni.

Hatua hiyo, inatokana na msako mkali uliopewa jina la ‘Endelevu’ unaoendelea katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Naibu Kamishna wa Idara ya Uhamiaji na Msemaji Mkuu, Abbas Irovya, alisema msako ambao ulianza mwanzoni mwa mwezi huu umekuwa na mafanikio.

Alizitaja nchi wanazotoka na idadi yao kwenye mabano kuwa ni Burundi (41), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (30), Kenya (11), Uganda (6), Pakistan (3), Somalia (7), Nigeria (4) na Cameroon (1).

Nchi nyingine ni Afrika Kusini (1), Malawi (11), Rwanda (44) na Msumbuji (7).

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA mjini Dar es Salaam katika maeneo ya Mwananyamala, Mikocheni, Tegeta, Msasani, Sinza na Temeke umebaini kuwapo na idadi kubwa ya wahamiaji haramu.

Juzi katika eneo la Mikocheni B, MTANZANIA ilishuhudia raia kadhaa wa Malawi wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya kufanya kikao cha dharura, kwa ajili ya kuchangishana fedha waondoke nchini.

Mmoja wa raia hao (jina tunalo), alisema hivi sasa hawaishi kwa amani hata kidogo kutokana na jamaa zao wengi kukimbia makazi na kutelekeza familia zao.

“Tunaishi maisha ya shaka mno, naona ni bora nitafute mtu nimuuzie vyombo vyangu ili nirudi nyumbani haraka, maisha Malawi ni magumu mno tofauti na Tanzania,” alisema

Chanzo: Mtanzania

Tanzania kuwa ya viwanda

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda, amesema Tanzania itakuwa nchi ya viwanda vya kati ifikapo mwaka 2025 ikiwa wawekezaji watajengewa mazingira mazuri ya kuwekeza.

Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda cha kuzalisha wa ‘gypsum’ cha Kampuni ya Sunshine ya China kilichopo katika Kata ya Visiga, Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani juzi, Dk Kigoda alisema kuwa sekta ya viwanda inakuwa kwa kasi nchini.

“Kiwanda hiki ni muhimu kwa uchumi wa kata ya Visiga na taifa kwa jumla. Uchumi wetu hauwezi kutegemea kilimo peke yake, tunataka nchi yetu iwe ya viwanda vya kati ifikapo mwaka 2025,” alisema Dk Kigoda.

Dk Kigoda alisema kwa sasa sekta ya viwanda inachangia pato la Taifa kwa asilimia 30, hivyo ukuaji wa viwanda utakuza pato hilo ikiwa wawekezaji watajengewa mazingira mazuri.

“Nimeambiwa kuwa tangu uamuzi wa kulifanya eneo hilo la Visiga kuwa la viwanda tayari kuna viwanda vitano vya chuma, kusafisha mafuta, kutengeneza nondo na hiki cha gypsum. Sekta ya viwanda inachangia pato la Taifa kwa asilimia 30 na asilimia 40 ya ajira,’’ alisema.

hia Sunshine kuwa soko la bidhaa zao lipo kubwa,” alisema Dk Kigoda.

Alisema uwekezaji wa kampuni hiyo ambayo pia ina kiwanda cha baruti kilichopo wilayani Kibaha na madini wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya, utazingatia wajibu kwa jamii (corporate social responsibility)

Licha ya kuipongeza kampuni hiyo, Dk Kigoda aliwataka wawekezaji hao katika sekta ya viwanda kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha ili kukuza uchumi wa nchi.

Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hun Xue Hui, alisema kampuni hiyo ambayo ni tanzu ya kampuni za Sunshine ya China itatoa ajira rasmi kwa watu 60 na ajira nyingine zisizo rasmi na itakuwa ikizalisha gypsum tani 700,000 kwa mwaka.

Aliongeza kuwa, wananchi wanaozunguka kiwanda hicho watafaidika kwa kupewa kipaumbele cha ajira na huduma za jamii.

Kwa upande wake mwakilishi wa Ubalozi wa China nchini anayeshughulikia masuala ya siasa, Li Xuhang, alisema uwekezaji wa viwanda unaendeleza uhusiano kati ya Tanzania na China uliodumu tangu wakati wa uhuru.

“Mmefanya vizuri kuwekeza katika eneo hili kwani wananchi nao watafaidika. Tanzania na China zimekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka 50, hivyo kwa niaba ya Balozi wa China nchini tunawaunga mkono,” alisema Xuhang.

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI AGOSTI 6

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.