WAHAMIAJI HARAMU 133 MBALONI JIJINI DAR ES SALAAM


Jijini Dar es Salaam hekaheka za wahamiaji haramu zimeendelea, baada ya watu 133 kutoka mataifa mbalimbali kutiwa mbaroni.

Hatua hiyo, inatokana na msako mkali uliopewa jina la ‘Endelevu’ unaoendelea katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Naibu Kamishna wa Idara ya Uhamiaji na Msemaji Mkuu, Abbas Irovya, alisema msako ambao ulianza mwanzoni mwa mwezi huu umekuwa na mafanikio.

Alizitaja nchi wanazotoka na idadi yao kwenye mabano kuwa ni Burundi (41), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (30), Kenya (11), Uganda (6), Pakistan (3), Somalia (7), Nigeria (4) na Cameroon (1).

Nchi nyingine ni Afrika Kusini (1), Malawi (11), Rwanda (44) na Msumbuji (7).

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA mjini Dar es Salaam katika maeneo ya Mwananyamala, Mikocheni, Tegeta, Msasani, Sinza na Temeke umebaini kuwapo na idadi kubwa ya wahamiaji haramu.

Juzi katika eneo la Mikocheni B, MTANZANIA ilishuhudia raia kadhaa wa Malawi wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya kufanya kikao cha dharura, kwa ajili ya kuchangishana fedha waondoke nchini.

Mmoja wa raia hao (jina tunalo), alisema hivi sasa hawaishi kwa amani hata kidogo kutokana na jamaa zao wengi kukimbia makazi na kutelekeza familia zao.

“Tunaishi maisha ya shaka mno, naona ni bora nitafute mtu nimuuzie vyombo vyangu ili nirudi nyumbani haraka, maisha Malawi ni magumu mno tofauti na Tanzania,” alisema

Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment