|
Mbuyu Twite akiwa amevaa jezi yenye jina Rage, baada ya kutua Dar es Salaam jana |
Na Prince Akbar
KLABU
mbalimbali zimewasilisha pingamizi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
kupinga usajili wa wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi
Kuu.
Toto
Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton
aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal
Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.
Pia
Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday
Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu
za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa
beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho
haijalipwa.
Super
Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake
wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert
Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union)
kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho
hazikufuatwa.
Mchezaji
Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT
kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo
Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili
wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya
kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.
Azam
inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo
bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani. Nayo Simba inapinga
Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye
uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.
Vilevile
Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika
usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na
klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la
Soka Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine
2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu
hiyo.
Nayo
Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte,
Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za
kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la
Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile
ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi
lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa
kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati
wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo,
Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng,
Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti
wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu)
kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa
2012/2013.
No comments:
Post a Comment