Chadema Wamlima Barua JK
WAMTAKA ACHUKUE HATUA DHIDI YA MAUAJI YA RAIA KINYUME CHAKE SERIKALI INAHUSIKA
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemwandikia barua Rais Jakaya
Kikwete kikimtaka achukue hatua dhidi ya matukio kadhaa ya mauaji ya
raia yaliyotokea kwa nyakati tofauti katika mikutano yake ya hadhara
kwenye Mikoa ya Singida, Tabora, Arusha, Morogoro, Iringa.
Hatua kilichopendeza ni pamoja na kuwawajibisha viongozi wenye dhamana;
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Polisi,
IGP Said Mwema; Mkuu wa Operesheni Maalumu Polisi, Paul Chagonja,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile na Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Barua hiyo ya Septemba 10, mwaka huu iliyoandikwa na Mwenyekiti wake,
Freeman Mbowe baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, imemtaka
Rais Kikwete kuwafukuza kazi watendaji hao katika Serikali yake kwa kuwa
wameshindwa kazi.
Kimesema kwamba mauaji mengi miongoni mwa hayo, yametokea bila hatua
stahiki za kisheria kuchukuliwa na kusema kwamba ukimya huo unaweza
kutoa picha potofu kwa umma kwamba Serikali yake inaunga mkono au
imewatuma polisi au watu wengine waliosababisha mauaji hayo.
Matukio
ya vifo ambayo chama hicho kimetaka yachunguzwe ni pamoja na lile la
Januari Mosi, mwaka jana mkoani Arusha, Igunga (Novemba, mwaka jana) na
Arumeru Mashariki (Aprili, mwaka huu).
Mengine ni lile la Iramba lililotokea Julai 14, mwaka huu, Morogoro
(Agosti 27, mwaka huu) na Iringa Septemba 2, mwaka huu ambalo hata
hivyo, shauri lake limeshafikishwa mahakamani.
Kimedai kwamba katika Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, Kiongozi wa
Kata wa chama hicho, Msafiri Mbwambo alichinjwa huku chanzo cha kifo
hicho kikielezwa kuwa ni masuala ya kisiasa.
Pia
kilielezea mauaji yaliyotokea katika Kijiji cha Ndago, Wilaya ya
Iramba, Singida na kudai kwamba kikundi cha watu kilivamia mkutano wa
Chadema kwa mawe na kwamba licha ya polisi kuwapo eneo hilo,
hawakuchukua hatua zozote.
Chama hicho pia kimekumbusha mauaji ya mfuasi wake mkoani Morogoro, Ally
Zona kikisema kifo hicho pia kina utata kwani taarifa ya polisi imesema
alikufa kwa kugongwa na kitu kizito wakati chama hicho kikidhani kwamba
alipigwa risasi.
Kimesema
pamoja na matukio yote hayo, viongozi wote hao hawakuchukuliwa hatua
zozote za kuwajibika kwa matukio hayo.
Pia Chadema kimeonya kuwa hali hiyo ikiachwa inaweza kujenga dhana
potofu kwa wananchi kuwa Jeshi la Polisi liko mikononi mwa CCM na kazi
yake ni kulinda masilahi ya chama hicho kwa gharama yoyote ile jambo
ambalo Mbowe alisema ikiwa Rais Kikwete atachukua hatua za kinidhamu
dhidi ya viongozi hao, atakuwa ameudhihirishia umma kwamba Serikali yake
haifumbii macho mauaji yanayofanywa na vyombo vya usalama nchini.
Kimemtaka Rais Kikwete kuunda tume ya kijaji au kimahakama kuchunguza
vifo vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano au mazingira
ya kisiasa yanayokihusisha Chadema.
Ikulu yajibu
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipoulizwa juu ya barua
hiyo alisema haijafika ofisini kwake, huku akisisitiza kuwa kama
imeandikwa kwa Rais si lazima ifike kwake.
“Sijaiona, ila kama wamemwandikia Rais barua sidhani kama itakuja
kwangu. Itakwenda kwake moja kwa moja,” alisema Balozi Sefue.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakutaka kuzungumzia
hatua hiyo ya Chadema akisema, “Siwezi kusema chochote kwa kuwa barua
yenyewe sijaiona pia ni barua ya Rais.”
Kauli ya Bavicha
Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), limemtaka Rais Kikwete kuunda
tume huru yenye wataalamu wa sheria ili kuchunguza mauaji, utekaji,
vurugu na unyanyasaji wa wananchi unaotokea kwenye mikutano ya siasa
hasa inayokihusisha chama hicho.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini Morogoro baada ya kikao cha baraza
hilo taifa, Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alisema kwamba kama Rais
Kikwete atashindwa kufanya hivyo, baraza lake kwa kutambua kuwa matukio
mengi ya mauaji yamehusisha vijana, litahamasisha maandamano nchi nzima
na kuishtaki Serikali yake.
Habari hii imeandikwa na Fidelis Butahe na George Njogopa, Dar na Hamida Sharif, Morogoro. www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment