na mwandishi wetu
MIKAKATI na kampeni za majitaka zenye lengo la kumchafua Mbunge wa
Jimbo la Busega mkoani Simiyu, Dk. Titus Kamani, zimeanza kubainika kwa
kumhusisha na tena na tuhuma za mauaji.
Dk. Kamani, ambaye ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitosa kuwania nafasi ya
Mwenyekiti
wa Mkoa mpya wa Simiyu, ameanza kuchafuliwa akihusishwa na tuhuma za
kutaka kumuua aliyekuwa mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, aliwahi
kueleza bayana kuwa wamefanya uchunguzi wa kina na kubaini Dk. Kamani
hahusiki na tuhuma hizo na kwamba, waliotuhumiwa wameshafikishwa
mahakamani.
“Hatumtafuti Dk Kamani, tukimhitaji tutampata lakini katika uchunguzi
wetu tumebaini tuhuma hizo hazimuhusu," alikaririwa Kamanda Barlow baada
ya kuibuka kwa uvumi kuwa mbunge huyo alikuwa akisakwa na polisi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es
Salaam, jana, Dk. Kamani amesema kumekuwepo na kampeni chafu za
kuhakikisha jina lake linachafuka ili kudhoofisha harakati zake za
kukitumikia Chama.
Amesema kuwa tangu alipojitosa kuwania nafasi hiyo, kumekuwepo na
mikakati ya kumchafua inayofanywa na baadhi ya wanasiasa wakiwemo
waliopo ndani ya CCM na kwamba, hilo
amelibaini na atalifikisha kwenye vikao husika.
Dk. Kamani katika taarifa yake amesema kuwa, mbinu chafu hizo zimekuwa zikisukwa na
wanasiasa hao kwa lengo la kumchafua na kumchonganisha na wapigakura wake pamoja na jamii imuone kuwa hafai.
“Makovu na visasi vya kushindwa katika uchaguzi uliopita kamwe
havitaiharibu Busega wala kunidhoofisha kuwatumia wananchi wangu.
Nafahamu hizi ni mbinu chafu kwa ajili ya kuniharibia katika harakati
zangu za kuwania nafasi ndani ya Chama," alisema katika taarifa hiyo.
Tayari watu wanaotuhumiwa kuhusika katika njama za kutaka kumuua Dk. Chegeni
wameshapandishwa kizimbani kujibu mashitaka hayo.
Na Bashir Nkoromoh
No comments:
Post a Comment