Hofu
imetanda kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma baada ya mkimbizi mmoja toka
nchini Burundi kufariki kwa ugonjwa wenye dalili zinazofanana na ugonjwa
wa Ebola.
Hofu hiyo imetokana na mkimbizi Buchumi Joel kufariki baada ya
kuugua kwa zaidi ya wiki moja na kuzikwa mjini Kigoma kwa kuzingatia
taratibu za afya, ambapo wamesema ni muhimu serikali kudhibiti raia toka
nchi jirani ambao wamekuwa wakiingia bila kuzingatia au kupimwa afya zao
hali ambayo ni hatari.
Akizungumzia tukio hilo, kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma, Shija
Ganai ambaye pia ni afisa afya wa mkoa, amesema mkimbizi huyo alianza
kuugua akiwa katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu na baadaye kupelekwa
katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kigoma baada ya kuugua ugonjwa
wenye dalili za ugonjwa huo hasa baada ya kuanza kutokwa damu katika
sehemu zote za matundu ya mwili.
Ameeleza kuwa kutokana na hali yake na licha ya kwamba
hawajathibitisha kama ameugua ugonjwa wa Ebola, tahadhari zote
zimechukuliwa na serikali na mashirika ya afya kimataifa ili kuhakikisha
ugonjwa wowote aliokuwa nao hausambai.
No comments:
Post a Comment