HUU HAPA NI MWENDELEZO WA TUKIO LA NYOLOLO, MUFINDI


KAMA ILIVYOTOLEWA NA VYOMBO MBALIMBALI VYA HABARI


Picture

Daudi Mwangosi (picha via ChangamotoYetu.blogspot.com)

Picture

Habari zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa, Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi (pichani) wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten amefariki dunia katika ghasia zilizozuka kati ya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na polisi katika mkutano wa chama hicho mkoani Iringa jioni hii. 


Pia askari polisi mmoja wa Wilaya ya Igowole anasemekana yuko mahututi kutokana na kipigo. Taarifa kamili kuhusiana na tukio hili zitawajia baadaye. 


Inaripotiwa kuwa, kabla ya kuanza kwa vurugu hizo, viongozi wa CHADEMA na wafuasi wake walikuwa katika mkutano wa kufungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho. Wakiwa katika eneo la tukio, Polisi walifika katika tawi hilo na kuwataka wafuasi wa chama hicho kutawanyika kwa kuwa mikutano ya vyama vya siasa imepigwa marufuku kupisha kazi ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo imeongezewa siku saba baada ya muda wake wa awali kukamilika.


Kutokana na amri hiyo, wafuasi hao walikataa kutawanyika na kuwalazimu polisi kutumia mabomu ya machozi kwa nia ya kuwatawanya. Wakati wakipiga mabomu hayo, inadaiwa mwandishi mmoja wa habari, aliwafuata polisi na kuhoji sababu za kutumia nguvu hiyo kutawanya wananchi. Ndipo mwandishi huyo alikamatwa na kusababisha Mwangosi kwenda kujaribu kumnasua mwandishi mwenzake kutoka mikononi mwa polisi. Polisi walimsihi Mwangosi aondoke katika eneo hilo ili waendelee na kazi yao na alipokaidi, walimkamata na yeye. Wakati Mwangosi akiwa amezungukwa na askari polisi wanaokaribia watano, kulisikika mlio wa mlipuko na baadae Mwangosi na mmoja wa askari aliyekuwa amemshika walianguka chini. --  Kutoka kwenye blogu ya Ziro na Tina

 Mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel TEN cha Iringa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoani Iringa, (IPC) AMEUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA ASKARI POLISI, WAKATI POLISI WALIPOFYATUA MABOMU WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikiwa katika Tawi katika Kijiji cha Nyororo, wilayani Mufindi, mkoani Iringa. -- Kutoka kwenye blogu ya Mkwinda                                                                                     
                                           _______________


Daud Mwangosi ameuwawa leo katika vurugu za Polisi na wafuasi wa CHADEMA katika kijiji cha Nyololo, Mufindi, Iringa.

Mwangosi aliuwawa majira ya saa 10 jioni katika ofisi za CHADEMA Nyololo huku askari mmoja akijeruhiwa vibaya kwa risasi.

Kabla ya kuuawa kwa mwanahabari huyo, mabomu yalipigwa eneo hilo ili kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA ambao walikuwa wakigoma kutawanyika eneo hilo na kuamua kukaa chini kuwa hawapo tayari kuondoka katika ofisi yao.

Chanzo cha mwanahabari Mwangosi kuuwawa kilitokana na kukamatwa kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe mkoa wa Iringa, Godfrey Mushi na hivyo mwanahabari huyo kutaka kuhoji polisi sababu ya kukamatwa kwa mwanahabari huyo ndipo askari hao walipoanza kumshambulia kwa kichapo na baadaye mlio kama wa bomu ulisikika eneo hilo na mwandishi huyo na askari mmoja waliaguka chini.

Ndani ya dakika tano ilisikika sauti kutoka kwa askari huyo kuwa afande nimekufa ndipo walipomchukua na kumpeleka Hospitali ya wilaya ya Mufindi huku mwili wa mwanahabari huyo ukipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti.

Katika vurugu hizo zilizodumu kwa takribani dakika 30 kwa askari na wafuasi wa CHADEMA kurushiana mawe kwa mabomu, zaidi ya magari matano ya CHADEMA na ya wananchi yameharibiwa, huku watu kadhaa wakiachwa wamejeruhiwa hali mwanahabari mmoja, Godfrey Mushi akijeruhiwa vibaya. --- Kutoka kwenye blogu ya FrancisGodwin, Iringa. (pamoja na picha zinazoonekana hapo chini, bofya picha moja moja kusoma malezo yaliyopo chini yake).

                                                          _____________

Taarifa za awali za Polisi, zilieleza kuwa  wakati wa vurugu zikiendelea na polisi wakijaribu kuytawanya wafuasi wa CHADEMA, Mwangosi aliamua kukimbia kutoka upande ambao kulikuwa na kikundi cha watu waliokuwa wakitawanywa na kwenda upande ambao walikuwepo askari Polisi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa wakati Mwangosi anakaribia walipokuwepo Polisi hao, kitu kama bomu kilirushwa kutoka upande ulipokuwepo kikundi hicho cha watu ambacho kililipuka na kumuua Mwangosi na kujeruhi askari kadhaa.

Taarifa hiyo ilitaja kuwa Polisi aliyejeruhiwa vibaya katika tukio hilo ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCS), ambaye hata hivyo hakutajwa jina lake wala wilaya anayofanya kazi. --- Kutoka kwenye blogu ya Lukwangule


No comments:

Post a Comment