|
Akuffo |
SIMBA SC imelazimishwa sare ya 1-1 na Sony Sugar ya Kenya, Uwanja
wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha jioni hii, katika mchezo wa kirafiki
kujiandaa na mechi ya Ngao ya jamii dhidi ya Azam FC, Septemba 11, mwaka huu,
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, bao la Simba lilifungwa na Daniel Akuffo,
wakati Komabil Keita alijifunga katika jitihada za kuokoa na kuwapa Wakenya bao
la kuongoza.
Awali, Simba ilicheza mechi mbili Arusha, dhidi ya Mathare
United ya Kenya na JKT Oljoro ya Arusha, ambazo zote ilishinda 2-1,
mshambuliaji mpya Daniel Akuffo kutoka Ghana akifunga bao moja kila mechi,
Kiggi Makaasy na Mrisho Ngassa wakifunga mabao mengine.
Simba inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 11, mwaka
huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo kihistoria hiyo itakuwa mechi ya
tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kukutanisha timu nje ya
wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na
ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu
ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia
bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba
na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na
mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga
Yanga mabao 2-0.
No comments:
Post a Comment