KAMATI YA MGONGOLWA YAAMUA SIMBA, YANGA NA AZAM ZIKAE MEZA MOJA KESHO KUMALIZA MATATIZO YAO YA USAJILI


Mgongolwa


KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa, kesho saa 6:00 mchana itakukutana itakutana na klabu zilizoweka na zilizowekewa pingamizi za usajili wa wachezaji kwa ujumla kuelekea msimu wa Ligi Kuu ya Bara 2012/2013.
Habari za ndani kutoka TFF, ambazo  zimesema kwamba, viongozi tu wa klabu zilizoweka na kuwekewa pingamizi, ndio watakaohudhuria kikao cha kesho, makao makuu ya TFF, Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam.
Hatua hiyo inafuatia kikao cha Kamati ya Mgongolwa tangu jana asubuhi hadi usiku, kumalizika bila kupata suluhisho la pingamizi hizo na sasa inaamua kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata suluhu.
Katika pingamizi hizo, Azam inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani na ili kumuachia kiungo huyo iliyemsajili kutoka Simba miaka mitatu iliyopoita, inataka dola za Kimarekani 50,000 ingawa Simba wamefika dola 20,000 ambazo pia wameomba kulipa kwa awamu.
Habari zaidi zinasema kwamba, Simba nayo inataka dola 60,000 kutoka kwa Yanga, ili wawauzie beki Kevin Yondan. Simba imepinga Yondan kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.
Vilevile Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.
Nayo Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Pingamizi nyingine ambazo jumla zinahusu wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu ni Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlington aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.

No comments:

Post a Comment