Kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana
NI BADA YA KUWA MJUMBE NEC, KAMATI KUU KWA MIAKA 25, AZUNGUMZIA UCHAGUZI 2015, HATIMA YAKE BAADA YA SIASA
KADA
maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana ametangaza
kung’atuka rasmi katika siasa baada ya kukitumia chama chake kwa miaka
25 akiwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Kamati Kuu (CC) na
Kamati ya Maadili.
Kinana ambaye amekuwa Meneja wa Kampeni za mgombea urais wa CCM tangu
mwaka 1995 ulipoanza uchaguzi wa vyama vingi, alisema kwamba baada ya
kutumikia chama katika nyadhifa za juu kwa robo karne sasa, ameamua
kupumzika ili kuwaachia vijana waendelee kukijenga chama hicho kikongwe
nchini na barani Afrika.
“Nimekuwa
Mjumbe wa NEC kwa miaka 25, bila shaka muda huu unatosha, kwani wanaCCM
wamenipa heshima ya kuwa katika vikao vya juu vya chama kwa robo karne.
Sasa ni wakati wa kung’atuka, nimetoa mchango kwa kadri nilivyoweza
katika vikao mbalimbali na katika shughuli nyingi,” alisema.
Alisema anaamini kuachana kwake na siasa hakutakuwa na madhara kwa chama
chake, kwani CCM ina hazina kubwa ya viongozi ambao wana sifa na
wanaweza kuongoza chama hicho kuelekea Uchaguzi wa 2015.
“Uongozi
ni kupokezana vijiti. Wako wanaCCM wazuri, walio na uwezo mkubwa na
sifa za kutosha kuongoza. Nawashukuru wanaCCM na viongozi kwa heshima
waliyonipa wakati wote huu,” alisema Kinana ambaye alikuwa Meneja wa
Kampeni wa Rais Benjamin Mkapa kwa vipindi viwili na Rais Jakaya Kikwete
kwa vipindi viwili vya uchaguzi.
Kinana alisema anajivunia kufanya kazi na marais wote wa Tanzania
kuanzia Mwalimu Julius Nyerere hadi Rais Kikwete kwa uadilifu mkubwa na
kuheshimiana.
”Ushauri
wangu katika vikao umekuwa ukiheshimika sana. Nimekuwa nikiheshimiwa na
uongozi wote wa CCM na hata wapinzani nao tunaheshimiana. Nimesimamia
kampeni za kistaarabu na ambazo zimeleta ushindi mkubwa kwa CCM tangu
kuanza kwa mfumo wa vyama vingi,” alisema.
Kinana ambaye pia alikuwa Spika wa Kwanza wa Bunge la Afrika Mashariki
(EALA), ameshauri vijana ndani ya CCM watangulize masilahi ya taifa
mbele na wasikilize wananchi.
Ni muhimu washikamane, wabuni mikakati ya kusaidia kukuza uchumi kwa
haraka zaidi na kuendeleza umoja na undugu wetu,” alisema.
Ushauri
wa viongozi wapya CCM
Kinana alishauri viongozi wapya ambao wanatarajiwa kuchaguliwa ndani ya
chama chake, iwapo wataona upungufu wake wausahihishe.
“Ni matumaini yangu kuwa watakaopata uongozi wataona upungufu na
watasahihisha makosa yangu,” alisema.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2015, Kinana aliwaasa viongozi wasiwaze nani
anafaa kuwa mgombea urais bali washughulikie kero za wananchi.
“Bado
tuna kazi kubwa ya kutekeleza Ilani. Tusiwasumbue Watanzania kuwa ni
nani anafaa kuwa Rais bali tushughulikie matatizo yao. Kwa sasa ajenda
ya CCM ni kutekeleza ahadi zetu katika sekta zote siyo kutafuta nani
atakuwa Rais 2015," alisema na kuongeza:
"Hata
wapinzani wawaeleze Watanzania yale ambao wamedhamiria kutekeleza.
Kueleza upungufu wa CCM ni mtaji mdogo kwa wapinzani, ajenda kubwa ni
watafanya nini? Hapa bado wana kazi kubwa. Wanapoona upungufu wasisite
kutusema,”
Kinana ambaye ana shahada ya uzamili katika utawala na masuala ya sera
kutoka Chuo Kikuu cha Harvad nchini Marekani, alisema anatarajia
kufundisha na kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika moja ya vyuo vikuu
vya hapa nchini.
“Baada
ya kustaafu kuna mambo mawili ambayo natarajia kufanya. La kwanza ni
kuona kama naweza kufundisha. Pili kusoma katika mojawapo ya vyuo vikuu
vyetu,” alisema.
Mbali na nyadhifa zilizotajwa huko juu, Kinana ametumikia Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa muda mrefu na kupanda cheo hadi kufikia
Kanali.
Amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Arusha Mjini.
Nape
alisema Kinana ni miongoni mwa wanasiasa waadilifu wa CCM ambao
wamekitumikia chama kwa muda mrefu na kwa uaminifu wa hali ya juu.
Ni kweli hajagombea, lakini kutokugombea kwake hakujafungwa milango kwa
CCM kumtumia au kutumia uzoefu wake pale watakapomhitaji.
Alisema "Kwa mfano Mwenyekiti wa CCM ana nafasi alizopewa kikatiba
kuteua wajumbe wa NEC, huwezi kujua anaweza akamwona anafaa na
akamteua,"
Chanzo: www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment