SIMBA: HATUOMBI MSAADA YANGA WALA KWA MANJI, TUNADAI HAKI YETU NA KAMA NOMA NA IWE NOMA SASA

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Hans Poppe akizungumza na BIN ZUBEIRY leo asubuhi ofisini kwake, Mbezi

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba hawawezi kumuomba radhi Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Mehboob Manji ili warejeshewe dola za Kimarekani 30,000 wanazodai kutapeliwa na beki Mbuyu Twite, kwa sababu wanadai haki yao.

Akizungumza leo ofisini kwake, Mbezi, Tangi Bovu, Dar es Salaam, Hans Poppe ambaye ni Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema kwamba madai ya Manji kutaka kuombwa radhi, hayahusiani na suala la Twite.

Kauli hiyo, inafuatia kikao cha jana baina ya klabu hizo mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa, kushindwa kufikia makubaliano kwa sababu ya Yanga kugoma kulipa fedha, hadi waombwe radhi na Simba.

Katika kikao hicho kilichoanza majira ya saa 7:00 mchana, upande wa Yanga uliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga na Katibu, Celestine Mwesigwa wakati kwa Simba walikuwepo Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Hans Poppe.

Ikumbukwe, Simba iliwasilisha malalamiko ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa Twite. Ilidai Twite alisaini mkataba na klabu yao Agosti 1, mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine 2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo, mchezaji huyo akahamia Yanga.

Katika mjadala huo, Simba ilikubali kurudishiwa fedha zao, lakini viongozi wa Yanga wakasema hawawezi kutoa hadi waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alisema viongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.

Simba wakasema kauli yake ya Rage ilikuwa sehemu ya utani wa jadi, kama ambavyo Yanga walimvalisha jezi Twite yenye jina la Rage.

Kufikia hapo, Simba wakasema hawawezi hata kujadili suala la Kevin Yondan na Kamati ya Mgongolwa ikasema itapitia maelezo ya pande zote, watatoa majibu kwa mujibu wa kanuni na sheria Septemba 10, mwaka huu.

Katika kesi ya Yondan, walalamikaji ni Simba, ambao wanadai beki huyo alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba na klabu yao.

“Tulikuwa tayari kuzungumza nje ya utaratibu wa sheria, fedha alizochukua Twite zirudishwe, lakini pia tulitaka kitendo cha yeye kusaini mara mbili, lazima kikomeshwe, tulitaka kuiachia TFF imfungie, ili ajue alifanya makosa na kutoa fundisho kwa wachezaji wengine,”alisema Hans Poppe.

“Lakini katika kikao cha jana, inaonekana wawakilishi wa Yanga (Sanga na Mwesigwa), hawakuwa na madaraka, kwani pamoja na kukiri Mbuyu alipewa dola 30,000 na Yanga wakachukua dhamana ya kuzirudisha, baadaye wakasema wamezungumza na Mwenyekiti wao, Manji, anataka kwanza aombwe radhi, kwa sababu aliambiwa fedha zake chafu,”.

“Sisi hatuombi fedha kwa Yanga, wala hatuombi fedha kwa Manji, sisi hatuombi msaada. Tunadai haki yetu, tumeweka pingamizi Mbuyu asichezee sehemu yoyote hadi arudishe fedha zetu. Sasa wanaopokuja na masharti ya kuombwa radhi tunashindwa kuwaelewa, na kama ni hivyo waache sheria ichukue mkondo wake,”alisema.

Hans Poppe alisema kwa kuwa sheria iko wazi kwamba mchezaji atakayesaini klabu mbili tofauti kwa wakati mmoja, anatakiwa kufungiwa miaka miwili, hawana wasiwasi na wanasubiri kuona TFF itafanya nini kwa kuwa hata Yanga wanakiri Mbuyu amesaini Simba na mchezaji mweyewe hajawahi kukana.

Aidha, Hans Poppe alisema kwamba kama Yanga hawataki kulipa hizo fedha, badi wawaache Simba watumie njia wanazojua kumdai mchezaji mwenyewe ili kuhakikisha wanalipa.

No comments:

Post a Comment