Taarifa Ya Jukwaa La Wahariri Kuhusu Kuuawa Kwa Mwandishi Daudi Mwangosi
TAARIFA YA JUKWAA LA WAHARIRI (TEF) KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU KUUAWA KWA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI
UTANGULIZI:
1.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limepokea kwa masikitiko makubwa
kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten,
mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.
2.
Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari
mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa akiwa kazini jana, Septemba 2, 2012,
wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema).
3.
Tukio hili linaiingiza Tanzania katika historia mbaya ya ukiukwaji na
ukandamizwaji wa uhuru wa habari, kwani ni kwa mara ya kwanza
tunashuhudia mwandishi wa habari AKIUAWA WAKATI AKITEKELEZA MAJUKUMU
YAKE YA KIHABARI.
4.
Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Mwangosi kabla ya kufikwa na mauti
saa 9.30 alasiri katika kijiji cha Nyololo, Mufindi, alizingirwa na
kushambuliwa na polisi waliokuwa katika eneo la tukio. Na hata alipopiga
kelele za kuomba msaada, hakusikilizwa na matokeo yake aliuawa na kitu
kinachodhaniwa kuwa ni bomu.
5.
Kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania, TEF tumechukua hatua za
haraka za kuunda timu ya uchunguzi wa suala hilo, ambayo itakwenda
mkoani Iringa mapema kadri itakavyowezekana, ili kubaini ukweli wa tukio
hilo. Lengo la uchunguzi huo ni kuweka kumbukumbu sahihi
(documentation) ya tukio hilo la aina yake katika historia ya nchi yetu.
6.
Matokeo ya uchunguzi huo pamoja na mwingine unaofanywa na Umoja wa
Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ndiyo yatakayotoa mwelekeo
wa hatua ambazo TEF inachukua dhidi ya Jeshi la Polisi katika siku
chache zijazo.
MTIZAMO NA MSIMAMO WA TEF
Kwa
kuzingatia taarifa kutoka Iringa na zile za vyombo vya habari vya jana
(Jumapili, Septemba 02, 2012) na leo (Jumatatu, Septemba 03, 2012), TEF
ina mtizamo na msimamo kama ifuatavyo:
1.
Kwanza tunalaani vikali tukio la kupigwa, kisha kuuwawa kwa mwandishi
Daudi Mwangosi ambalo limeigusa tasnia ya habari kwamba sasa pengine
waandishi wa habari ni malengo “target ya polisi” wanapokuwa kwenye kazi
zao.
2.
Ieleweke wazi kwamba matukio haya siyo yanaondoa imani ya waandishi wa
habari kwa jeshi la polisi tu, bali yanaweza kuwa chanzo cha uhasama na
ufa mkubwa ambao utawanyima wananchi nafasi ya kutumikiwa na pande mbili
ambazo zinategemeana.
3.
Kwa matukio ya aina hii, tunadhani wakati mwafaka kwa uongozi wa Jeshi
la Polisi nchini kuwajibika, kuazia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa na
uongozi wa Makao Mkuu, akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi
Mwema.
4.
Tunasema hivi kwani kuna kila dalili kwamba polisi wanahusika kwa namna
moja au nyingine na tukio au/na matukio yaliyosababisha kifo cha
Mwangosi, kwani kitendo cha kumzingira tu na kumshambulia kinathibitisha
kwamba hawakuwa na nia njema hata kidogo dhidi ya mwandishi huyu.
5.
Taarifa ambazo TEF tunazo, pia zinadai kwamba kulikuwa na mpango wa
polisi wa “kuwashughulikia waandishi wa habari watatu” (Mwangosi) akiwa
mmojawapo na hilo lilionekana likitekelezwa kwa polisi kumshambulia
mwandishi huyo, baadaye alipoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha
6.
Hili linatiliwa nguvu na tukio jingine la polisi kumpiga na kumjeruhi
mwandishi mwingine, Godfrey Mushi ambaye ni mwakilishi wa gazeti la
Nipashe mkoani Iringa. Mwandishi wa tatu ambaye hadi tunapoandika
taarifa hiyo yumo katika mpango wa ‘kushughulikiwa na polisi’ ni Francis
Godwin ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea.
7.
Vitendo vya aina hii havivumiliki na havipaswi kuachwa kuendelea kwani
ni hatari kwa ustawi wa demokrasia na uhuru wa habari nchini. Hatuwezi
kuendelea katika mazingira ambayo polisi wanageuka kuwa chombo cha
mauaji ya raia badala ya kuwa walinzi wa raia.
8.
Kwa maana hiyo, mbali na uchunguzi ambao utafanywa na polisi, tunatoa
wito kwa Serikali kuunda chombo huru, ambacho kitabaini ukweli, na
matokeo yake yatangazwe kwa umma, huku wahusika wa aibu hiyo
wakichukuliwa hatua za kisheria. Tunasema hivyo, tukifahamu kwamba
tayari kuna jitihada za kuficha ukweli na kueneza propaganda za uongo
kuhusu tukio zima.
9.
Mwenendo wa aina hii wa chombo cha dola kuamua kutumia silaha kuua na
baadaye kupanga mbinu chafu za kuficha ukweli ni hatari kwa Taifa, na
unaiweka demokraisia ya nchi yetu njia panda, huku tukielekea katika
hatari ya Taifa kutumbukia katika uovu.
IMETOLEWA NA:
NEVILLE MEENA,
KATIBU MKUU – JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF) SEPTEMBA 3, 2012
No comments:
Post a Comment