KINYANG’ANYIRO cha kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepamba moto baada ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne kujitosa kuwania nafasi hizo. Pazia la uchukuaji na urejeshaji wa fomu lilifungwa Alhamisi iliyopita na mpambano mkali upo katika kuwania uongozi wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia kapu maalumu maarufu kundi la kifo.
Kundi hili limegonganisha mawaziri kadhaa pamoja na makada wa CCM maarufu wakiwania nafasi 10. Waliojitosa katika kinyang’anyiro hicho kupitia kundi la kifo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi, Ofisi (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Nafasi nyingine zenye ushindani katika uchaguzi huo ndani ya chama hicho ambazo baadhi ya mawaziri wamejitosa ni jumuiya za chama hicho, Umoja wa Vijana (UVCCM), Wanawake (UWT) , Wazazi na ujumbe wa Nec kupitia wilaya.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa baadhi ya mawaziri na vigogo, wamelikimbia kundi la kifo na kugeukia ama jumuiya hizo au wilaya zao. Hatua hiyo imetokana na mabadiliko ya Katiba yaliyofanywa na CCM ambayo yanaonyesha kwamba kundi hilo sasa litakuwa na viti 10 tu badala ya 20 vya awali.
Vigogo wengine waliojitosa katika uchaguzi huo ni pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya aliyechukua fomu kuwania ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Rungwe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi ambaye anawania ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Songea na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa anayewania nafasi ya uenyekiti wa UWT taifa.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment