Waasi watawala kimabavu DRC
Mkuu wa harakati za kudumisha amani wa Umoja wa
mataifa Herve Ladsous ameliambia baraza la usalama la Umoja huo kwamba
waasi wameidhinisha kile anachokiita kuwa ni utawala wa kimabavu
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Bwana Ladsous amesema waasi wa M23 wanadhibiti idadi kubwa ya maeneo ya Mashariki mwa Congo na wanawatoza kodi wananchi .
Umoja wa Mataifa unaishutumu Rwanda
kuwaunga mkono waasi wa M23. Wakati huo huo Maafisa wa Congo wanataka
Rwanda iwekewe vikwazo biashara ya madini .
Waziri wa Madini wa Congo, ameziandikia nchi za
Marekani na Uingereza akizitolea wito kampuni katika nchi hizo ziache
kununua madini kutoka Rwanda, ambayo mengi anasema yanachimbwa katika
ardhi ya Congo.
Zaidi ya watu 200,000 wameachwa bila makao kufuatia mapigano Mashariki mwa nchi.
Mkutano wa maafisa wa ngazi ya juu watakaojadili
mzozo huo unatarajiwa kufanyika katika baraza la usalama la Umoja wa
mataifa mjini New York wiki ijayo.
"waasi wa M23 wako katika pembe moja ya mkoa wa
Kivu Mashariki ambao unapakana na Rwanda na Uganda'' alisema bwana
Ladsous wakati akiwahutubia waandishi wa habari mjini New York.
Waasi wanaotoroka vita
"ni kama ambao wanatawala kwani wanawatoza kodi
wenyeji wa mkoa huo , jambo hili halikubaliki hata kidogo'' aliongeza
bwana Ladsous.
Wakati huohuo, maafisa wa utawala nchini DRC wanataka vikwazo kuwekewa biashara ya madini yanayotoka nchini Rwanda.
Wadadisi wanasema kuwa madini mengi yanayotoka
nchini Rwanda huenda yalitoka nchini DRC na kuchimbwa na makundi ya
waasi walio na uhusiano na Rwanda.
"namna tunavyoweza kukomesha kabisa mzozo huu ni
Rwanda kuwekewa vikwazo vya kibiashara kwa madini yanayotoka nchini
humo hadi tutakapoweza kupata suluhu la kudumu kwa mzozo katika mikoa ya
Kaskazini na Kusini ma Kivu.'' alisema waziri wa madini wa DRC Martin
Kabwelulu. .
No comments:
Post a Comment