Rais wa Zanzibar,
Dk Ali Mohamed Shein, amesema serikali haitavumilia tena vurugu
zinazofanywa na wafuasi wa Uamsho ili kulinda amani na umoja wa kitaifa
visiwani humo.
Tamko hilo amelitoa alipokuwa akihutubia Baraza la Idd-El Haji katika
ukumbi wa Bwawani mjini Zanzibar jana katika hafla iliyohudhuriwa na
Makamu wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.
Alisema serikali itahakikisha inafanya kila linalowezekana ili
kuhakikisha wanaohatarisha usalama, amani na umoja wa kitaifa
wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
“Serikali haitowavumilia na ustahamilivu na uvumilivu wa serikali umefikia kiwango cha mwisho,” alionya Dk Shein.
Alisema serikali itatumia sheria kupambana na kikundi chochote
kinachofanya vitendo vya uchochezi dhidi ya wananchi na kuhatarisha
amani na mshikamano wa wananchi.
“Hapa tulipofika basi tena” alisema Dk Shein na kuongeza kuwa “vyombo
vya dola havikumteka Kiongozi wa Uamsho Sheikh Farid,” alisema.
Alisema Zanzibar inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria
na hapana hata mtu mmoja alie juu ya sheria kwa mujibu wa Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984.
Alisema serikali imeamua kuimarisha ulinzi mkali wa doria ili kupambana
na watu wanaotishia uvunjifu wa amani na vikundi vya uharibfu
vilivyoibuka tangu kuanza kwa vuguvugu la Uamsho.
“Tutazitumia sheria na taratibu zilizopo kuvishughulikia vitendo vya
uvunjaji wa amani vitakavyofanywa au kuchochewa na kikundi chochote
Zanzibar,”alionya Rais wa Zanzibar.
Alisema hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kuwakamata
viongozi wa Uamsho wanane na kuwafikisha katika vyombo vya sheria lakini
alisema “Ni Jukumu letu sote tushirikiane na serikali kwa kuwakana kwa
kutoa tamko zito kwa kila mmoja wetu dhidi ya watu wanaofanya vitendo
vya kuhatarisha amani na kurudisha nyuma maendele ya Zanzibar.
Alisema kwamba vikosi vya ulinzi na usalama vikiongozwa na Jeshi la
Polisi vitaendelea kuimarisha ulinzi na kuwataka wananchi, wageni na
wawekezaji kuondoa hofu juu ya usalama wa Zanzibar baada ya serikali
kufanikiwa kuwakamata watu wakorofi na kuwafikisha katika vyombo vya
sheria.
Aliwataka wananchi wachache wenye nia ya kufanya fujo na vurugu waache
kujiingiza kwenye vitendo hivyo kwani serikali haitovumilia misingi ya
amani na umoja wa kitaifa kuchezewa kwa maslahi ya watu binafsi.
Hata hivyo alivipongeza vyombo vya ulinzi kwa kufanikisha kurejesha hali
ya amnai na utulivu na kuwataka wananchi kuendelea kutoa mashirikiano
dhidi ya vyombo vya Ulinzi kwa kuwafichua wote waliohusika na vurugu
hizo.
Dk Shein alisema vitendo vya vurugu vina athari kubwa katika ukuaji wa
uchumi hasa kwa kuzingatia asilimia 25 ya pato la taifa na asilimia 83
ya fedha za kigeni Zanzibar zinatokana kupitia sekta ya utalii visiwani.
Kuhusu Kilimo, Dk Shein alisema kwamba serikali katika msimu wa mwaka
huu imepanga kulima hekta 40,000 za mpunga na tayari serikali
imeshaagiza matrekta mapya 20 ili kuinua sekta ya kilimo visiwani humo.
No comments:
Post a Comment