Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema mpaka wa Tanzania na
Malawi ni salama, hivyo hakuna sababu kwa wananchi kuingiwa na hofu kwa
kuwa jeshi lipo eneo hilo kuimarisha ulinzi.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema hayo jana wakati
akihojiwa na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One,
kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa kuna mabomu yamerushwa upande wa
Tanzania toka nchi jirani ya Malawi.
“Hali ya mpakani ni shwari na jeshi liko huko, kama hali ingekuwa mbaya
tayari Mbeya ingekuwa imehamwa, wananchi wasiwe na wasiwasi kabisa
hakuna mabomu yeyote yaliyorushwa,” alisema Mgawe.
Alisema taarifa zilizosambazwa kwamba kuna mabomu yamerushwa toka Malawi
ni jambo ambalo limetengenezwa ili kuwatia hofu wananchi kwasababu tu
kulikuwa na kutofautiana kati ya Tanzania na Malawi. Alisema suala hilo
kwa sasa linashughulikiwa na viongozi wa nchi hizo kwa njia ya
mazungumzo.
“Sidhani kama Malawi wanaweza wakafikia hatua ya kurusha mabomu, taarifa
hizi ni za uzushi, hata namba zilizoandikwa siyo za jeshi ni mtu
ametunga tu,”alisema Mgawe.
Mgawe alisema hata hivyo JWTZ lipo katika harakati za kufanya utafiti
kubaini mmiliki wa namba iliyotumika kusambaza ujumbe huo na kwamba pia
inawezekana watu wakafanya hivyo kwa ajili ya kufanya biashara zao.
Kuhusu ushirikiano kati ya JWTZ na makampuni ya simu, alisema
watawasiliana na wenye mitandao ya simu na kwamba hata hivyo wananchi
wasiogope na kujenga hofu katika jambo ambalo siyo la ukweli na badala
yake waendelee na shughuli zao kama kawaida.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment