Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema
Muswada wa
marekebisho ya sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambao unatarajiwa
kuwasilishwa katika mkutano wa Kumi wa Bunge, umewaacha solemba
wanachama wa mifuko mingine baada ya marekebisho hayo kurejesha fao hilo
kwa mfuko mmoja pekee.
Sheria ya mafao ilipitishwa katika mkutano wa Bunge wa Aprili mwaka huu
na kuwazuia wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kuruhusiwa kuchukua
mafao yao hadi wafikishe umri kati ya miaka 55 na 60.
Baada ya wanachama wa mifuko hiyo na wadau wengine wakiwamo wabunge
kuipinga sheria hiyo, serikali iliahidi kuwa itaifanyia marekebisho na
kuwasilisha muswada kwa hati ya dharura.
Tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema,
amekwishawasilisha muswada huo katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar
es Salaam, ikiwa na maana kuwa utajadiliwa kwenye Mkutano wa Bunge
unaotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Muswada huo unakusudia kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali.
Kwa mujibu wa muswada huo, ambao NIPASHE imeuona, sehemu ya sita
inapendekeza marekebisho kwenye Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Mashirika
ya Umma (PPF), sura ya 372 kwa kuongeza kifungu kipya cha 44 ili kutoa
fursa kwa mfuko huo kutoa fao la kujitoa kwa mwanachama wake.
Kwa maana nyingine ni kwamba wanachama wa mifuko mingine kama NSSF
itaendelea kutumia sheria ambayo imelalamikiwa na wafanyakazi.
HOJA YA JAFO YAZIKWA
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mbunge wa Kisarawe (CCM), Seleman
Jafo, ambaye wakati wa mkutano wa Bunge wa Bajeti, alitaka kuwasilisha
muswada binafsi, alisema amepata barua kutoka kwa Katibu wa Bunge, Dk.
Thomas Kashillilah, ikimtaarifu kwamba, serikali itawasilisha muswada wa
marekebisho hayo, hivyo hana sababu ya kuandika muswada mpya.
Jafo alisema kwa kuwa alikwishawasilisha hoja ya kutaka marekebisho
kwenye sheria ya hifadhi ya jamii, Bunge lilimweleza kwamba ni fursa kwa
serikali au Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii; hivyo serikali
imeazimia kuiwasilisha kwenye mkutano ujao.
“Lakini kwa hali hii ni kwamba serikali haitatatua matatizo ya msingi ya
hoja yangu, muswada unatakiwa uguse mifuko yote kwa sababu malalamiko
ni ya wafanyakazi wote,” alisema.
SUGU AIONYA SERIKALI
Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi
maarufu kama Sugu, aliionya serikali kutochezea wafanyakazi kwa kuwa
kufanya hivyo ni kuhamasisha fujo.
Alisema ni vyema marekebisho yatakayowasilishwa bungeni yakarejesha fao
la kujitoa kwa mifuko yote kwa kuwa wafanyakazi wengi hawana usalama
kazini.
“Tunajua faida ya pensheni uzeeni kwa sababu ni msaada mtu anapostaafu,
lakini kwa mfumo wa nchi yetu ambayo wafanyakazi hawana usalama wa kazi
haiwezi kufanyakazi ipasavyo,” alisema.
Sugu alisema wafanyakazi kama wa migodini au hostelini wanafanyakazi
katika mazingira magumu na wanaweza kuachishwa kazi wakati wowote hivyo
fao la kujitoa litawasaidia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Dk. Ramadhan Dau, alisema fao la kujitoa katika mifuko ya
hifadhi ya jamii halimo katika sheria za kimataifa.
Dk. Dau, alisema hayo alipokuwa akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) katika kikao kati ya kamati
hiyo na bodi na menejimenti ya shirika hilo, katika Ofisi Ndogo za
Bunge, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema pia ni Tanzania Bara pekee ndiko ambako kuna fao la kujitoa
katika mifuko hiyo, lakini katika nchi za Kenya, Uganda, duniani kote,
hata Zanzibar, suala hilo halipo.
Hata hivyo, alisema mwanachama wa NSSF anapoamua kujitoa, anaupunguzia
Mfuko mzigo wa kumtunzia pensheni yake ya uzeeni, badala yake na
kujiumiza mwenyewe.
Shinikizo la kutaka serikali kuirekebisha sheria hiyo ili wanachama wa
mifuko walipwa mafao wakati wanapoacha kazi, liliilazimisha serikali
kukubali yaishe na kuahidi kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria
ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa mwaka 2012.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, aliliambia Bunge la bajati
kwamba kabla ya kuwasilishwa, muswada huo utapelekwa kwa wadau ili watoe
maoni na pia Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) itatoa elimu kuhusu fao
la kujitoa.
Hata hivyo, alisema wapo baadhi ya watu waliotafsiri kuwa kusitishwa kwa
fao la kujitoa kwamba mifuko ya hifadhi ya jamii imefilisika kwa kuwa
imewekeza kwenye miradi mibaya, jambo alilosema sio la kweli.
Kabaka alisema kuwa mifuko hiyo haina hali mbaya kifedha wala
haijafilisika na kwamba kuzuia fao la kujitoa ni utekelezaji wa sheria.
Waziri Kabaka alisema mchakato wa kuwasilisha muswada huo utaanza mara
moja kwa kuwashirikisha wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.
Kabla ya kauli ya Kabaka, Bunge lilipitisha Azimio lililowasilishwa na
Jafo, la kuletwa bungeni muswada wa dharura wa marekebisho ya Sheria Na.
5 ya mwaka 2012 inayozungumzia marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii ambayo ndani yake inaelezea kuzuiwa kwa fao la kujitoa
kwa wafanyakazi.
Kutokana na mapendekezo ya muswada huo kutowatuhusu wanachama wa mifumo
kingine kuchukua mafao kabla ya miaka 55 au 60, wanachama hao huenda
wakashinikiza kwa njia za maadamano na migomo.
Aidha, upo uwezekano wa kuzuka mjadala mkali bungeni kwa kuwa na wabunge nao ni wanachama wa mifuko hiyo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment