Spika Anne Makinda
Kufuatia taarifa
kuwa ripoti ya Kamati ndogo ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge huenda isiwasilishwe na kujadiliwa katika Mkutano wa 10 wa Bunge,
baadhi ya wabunge waliochunguzwa na kamati hiyo kwa tuhuma za rushwa
wamekuja juu na kusema lazima iwasilishwe ili kuweka mambo hadharani kwa
sababu ripoti hiyo siyo mali ya watu binafsi.
Ripoti ya kamati hiyo kama itajadiliwa bungeni itaweka hadharani ukweli
juu ya tuhuma za baadhi ya wabunge kutuhumiwa kwa rushwa ambazo
ziliibuka wakati wa Mkutano wa Nane wa Bunge.
OLE SENDEKA
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, akizungumza na
NIPASHE alisema ripoti hiyo lazima iwasilishwe bungeni ili ibainishe
ukweli wa tuhuma za rushwa kwa Wabunge waliotuhumiwa na kusababisha
Kamati ya Nishati na Madini ivunjwe.
“Hatuoni sababu kwanini ibaki kuwa ripoti ya watu binafsi, tunamshauri
Spika wa Bunge kama kweli kuna njama za kutaka isiwasilishwe bungeni
ailete ili wabunge waijadili kubainisha ukweli,” alisema Sendeka.
Sendeka alilaumu kitendo cha Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo, kutokana na kuanza kujadili suala la ripoti hiyo nje ya bunge
na kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha sheria na haki za Bunge.
SELEMAN ZEDI
Mbunge wa Bukene, Seleman Zedi, alisema ripoti hiyo ni muhimu
ikawasilishwa bungeni isomwe wazi kwa umma ili wapate kufahamu nini
kilichomo ndani ya ripoti hiyo.
Zedi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini,
iliyovunjwa na Spika Anne Makinda, alisema Watanzania wanasubiri kwa
hamu kujua kilichopo ndani ya ripoti hiyo hivyo kutowasilishwa bungeni
itakuwa siyo kuwatendea haki.
CATHERIN MAGIGE
Mbunge wa Viti Maalum, Catherin Magige, alisema ana imani ripoti hiyo
itawasilishwa bungeni na kwamba hawezi kutoa maoni yeyote kwa sababu
hajui kilichomo ndani yake.
YUSUF NASIR
Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Yusuf Nasir, alisema wananchi wasubiri
ripoti hiyo isomwe na maamuzi yatakayotolewa na kwamba isipowasilishwa
bungeni na kujadiliwa, yatakuwa ni maamuzi ya Kamati ya Uongozi ya
Bunge.
MUNDE ABDALLAH
Mbunge wa Viti Maalum Munde Abdallah, alisema anachofahamu ni kuwa
ripoti hiyo itawasilishwa bungeni kwasababu wabunge waliahidiwa na Naibu
Spika, Job Ndugai, baada ya kushindikana kuwasilishwa katika mkutano
uliopita.
“Ripoti isipowasilishwa tutahoji kwanini iwe hivyo wakati tumeahidiwa,
tuna hamu sana ya kutaka kujua ukweli wa jambo hilo la rushwa,” alisema
Abdallah.
Kamati ndogo ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, iliyokuwa
chini ya Mwenyekiti, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, ilipewa jukumu
la kuchunguza tuhuma za baadhi ya wabunge kutuhumiwa kwa rushwa.
Hata hivyo tangu kamati hiyo imalize kazi yake na kuwasilisha ripoti
Ofisi ya Spika, umeibuka utata kutokana na kile kinachoelezwa kuwako
kwa jitihada za kuikwamisha isiwasilishwe ili isiichafue serikali.
Hali hiyo inatokana na mgawanyiko ulioibua makundi mawili makubwa
yanayovutana kuhusu ripoti hiyo. Moja ukiongozwa na wabunge
waliotuhumiwa na upande wa pili ukijumuisha wale wanaoipigia debe
serikali katika sakata zima la sekta ya nishati nchini.
Ingawa kuna hali ya kutokueleweka kama ripoti hiyo itawasilishwa kwa
ajili ya kujadiliwa au la, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, juzi
aliiambia NIPASHE kuwa Kamati ya Uongozi ya Bunge inatarajia kukutana
Jumatatu ijayo, ikiwa ni siku moja tu kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Kamati uongozi inaundwa pamoja na watu wengine, Spika wa Bunge, Naibu
wake, Waziri Mkuu, wenyeviti wa kamati za bunge na Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Kwa mwelekeo wa mambo, moto mkubwa unatarajia kuwashwa juu ya ripoti
hiyo kwa kuwa wapo wabunge wanaotaka kusafishwa dhidi ya tuhuma ambazo
wanaamini wamevalishwa kwa makusudi, ilahali upande wa serikali ukiamini
kwamba kulikuwa na hujuma za chini kwa chini zilizosukumwa na
vishawishi vya rushwa kukwamisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya
Nishati na Madini ya mwaka 2012/13 Julai mwaka huu.
Ripoti hiyo inasubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania ili kuweka mambo
hadharani kuhusu wabunge wanaotuhumiwa kuhongwa na kampuni za mafuta ili
wakwamishe Bajeti hiyo na kutaka kuwajibishwa kwa viongozi wa wizara
hiyo Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim
Maswi.
Habari ambazo NIPASHE imezipata kutoka vyanzo mbalimbali zinasema kuwa
kumekuwa na juhudi nyingi za pande mbili zinazohusika na ripoti ya
kamati ya Ngwilizi, mmoja ukitaka kombe lifunikwe, na mwingine ukitaka
kila kitu kiwekwe wazi ili kulinda hadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kwa
rushwa.
Kabla na hata baada ya kuundwa kwa kamati hiyo kumekuwa na mgawanyiko
mkubwa ndani na nje ya Bunge na serikali kuhusu kashfa hiyo hali ambayo
iliibuka wakati wa mkutano wa nane wa Bunge la Bajeti na kusababisha
mvutano mkubwa wa wabunge na ndani ya serikali.
Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa ambazo zinaeleza kuwa huenda
ripoti hiyo isiwasilishwe na kujadiliwa bungeni kutokana na baadhi ya
mambo kutokuwa sawa baada ya kamati ya Ngwilizi kukamilisha uchunguzi
wake.
Habari zinasema kuwa baada ya kukamilika kwa ripoti hiyo, yameibuka
makundi mamwili yanayovutaka. Moja linaitetea serikali ili ripoti hiyo
iisafishe na lingine linataka haki itendeke kwa ukweli kuwekwa wazi na
kujulikana.
Kundi linalotaka haki itendeke linaamini kama kuna waliohongwa
wajulikane na kama siyo ukweli ujulikane kwa kuwa baadhi ya wabunge
walilalamika na kutaka ripoti hiyo itolewe mapema kabla ya kuahirishwa
kwa Mkutano wa Nane wakisema kuwa bila hivyo watakutana na hali ngumu
katika majimbo yao kwa kuwa wamevunjiwa haki zao.
Ripoti ya kamati hiyo kama itawasilishwa na kujadiliwa mjadala mkali
hautauepukika kutokana na kuwapo kwa mgawanyiko kwa kuwa kila upande
utataka kuhakikisha kuwa unatendewa haki.
Ingawa majina ya wabunge hao bado haijatajwa rasmi na mamlaka
zinazohusika na kupambana dhidi ya rushwa, lakini wakati wa mkutano wa
Nane wa Bunge ilielezwa kuwa wabunge wanaotuhumiwa kupewa rushwa ni
watano, kati yao watatu wanatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wawili
wanatoka vyama vya upinzani.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment